MAGONJWA
yasiyoambukiza yanachangia kwa kiasi kikubwa katika kupunguza kasi ya
maendeleo yetu kwani gharama za matibabu yake ni kubwa mno, si kwa kaya
zinazoathirika tu bali kwa Taifa zima.
Lishe
duni pamoja na ulaji usiofaa na mitindo ya maisha vinachangia kwa kiasi
kikubwa katika ongezeko la magonjwa yasiyo ya kuambukiza hususan kwa
vijana na watu wazima; ambao ndiyo nguvu kazi kwa Taifa letu.
Kauli
hiyo ilitolewa hivi karibuni na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wakati
akifungua mkutano wa tano wa wadau wa masuala ya lishe, jijini Dodoma.
Alisema ni muhimu wadau hao kuweka mikakati kupunguza kasi ya ongezeko
la magonjwa sugu yasiyo ya kuambukiza.
Waziri
Mkuu alisema magonjwa hayo yanapaswa kudhibitiwa kwa kuzingatia ulaji
unaofaa na mtindo bora wa maisha. Ni jambo lisilopingika kuwa hatua za
kukabiliana na magonjwa ya kusendeka (mfano matatizo ya moyo, saratani,
kisukari na shinikizo kubwa la damu), zinapaswa kuchukuliwa.
Alisisitiza
dhamira ya Serikali ya Awamu ya Tano, inayoongozwa na Rais Dkt. John
Magufuli ni kujenga uchumi wa viwanda ambao utatuwezesha kufikia uchumi
wa kati ifikapo mwaka 2025, hivyo ni muhimu suala la lishe bora likapewa
kipaumbele.
Alisema
kauli mbiu ya mkutano huo “Kuelekea Uchumi wa Viwanda: Lishe Bora ni
Msingi wa Kuendeleza Nguvu Kazi yenye Tija” inatoa hisia chanya ya
kufikia azma hiyo kwa kuwa maendeleo ya Taifa yanategemea sana uwepo wa
nguvu kazi ya kutosha na madhubuti.
Alifafanua
kuwa miongoni mwa matatizo ya lishe duni ni pamoja na upungufu mkubwa
wa vitamini na madini kwa watoto walio chini ya umri wa miaka mitano
(5), wanawake walio katika umri wa kuzaa na wajawazito, vijana balehe
pamoja na wakina baba.
Waziri
Mkuu alisema kuwa ni dhahiri kuwa tunahitaji kuanzisha viwanda
vitakavyozalisha vyakula vilivyoongezwa virutubishi muhimu ili
kurahisisha upatikanaji wa vyakula hivyo katika jamii zetu.
“Nitoe
wito kwa wadau wote hususan sekta binafsi kutumia fursa zilizopo na
kuwekeza katika viwanda vya usindikaji wa vyakula vinavyozingatia
viwango vya ubora. Niwahakikishie kuwa Serikali imeandaa mazingira
mazuri ya uwekezaji, kwa hiyo, tumieni kikamilifu nafasi hiyo.” alisema
Waziri Mkuu, Majaliwa
Alisema
kwa pamoja, wanaweza kuimarisha mikakati yao ya kuivusha nchi na watu
wake kutoka katika lindi la umaskini na kujenga nguvu kazi imara
itakayoweza kuhimili changamoto za maendeleo ya viwanda.
Waziri
Mkuu anatumia fursa hiyo kutoa rai kwa wadau wote, waendelee kuiunga
mkono Serikali kwa kuwekeza katika utekelezaji wa sera na mikakati
mbalimbali ambayo inalenga kuboresha hali ya chakula na lishe miongoni
mwa jamii, hususan kwa watoto, wanawake walio katika umri wa kuzaa,
vijana balehe na watu wenye mahitaji maalum kilishe.
“Kwa
msingi huo, Serikali imejumuisha masuala ya lishe katika Mpango wake
Jumuishi wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano (2016/2017 – 2020/2021),
kama eneo la kipaumbele katika kuboresha na kuendeleza nguvu kazi ya
Taifa.”
Waziri
Mkuu aliongeza kuwa “dhamira ya Serikali ni kutokomeza aina zote za
utapiamlo kwa kuwekeza na kuweka mazingira wezeshi kwa wadau wote
kushiriki katika kuchangia utekelezaji wa afua za lishe nchini ambazo
zina matokeo ya haraka miongoni mwa makundi yote yanayoathirika.”
Alisema
jitihada hizo zinalenga kutimiza azma ya Baraza la Umoja wa Mataifa la
“Muongo wa Kuchukua Hatua katika Masuala ya Lishe – Decade of Action on
Nutrition” ya mwaka 2016 hadi 2025 na pia kuwezesha kufikiwa kwa Malengo
yote 17 ya Umoja wa Mataifa ya Maendeleo Endelevu (United Nations
Sustainable Development Goals).
Alibainisha
kuwa Serikali inaendelea kutilia mkazo suala la uhamasishaji miongoni
mwa watunga sera na viongozi katika ngazi mbalimbali kuhusu masuala yote
yanayohusiana na lishe kwa lengo la kuwa na uelewa wa pamoja kuhusu
masuala hayo.
Alisema
juhudi hizo zinaenda sambamba na utoaji wa elimu sahihi ya lishe kwa
umma kwani tunaamini kuwa Watanzania wakielimishwa vizuri kuhusu masuala
haya itachangia kuleta mabadiliko chanya katika jamii pamoja na taasisi
zetu kwa ujumla.
Alisema
Serikali imeendelea kuongeza rasilimali kila mwaka kwa ajili ya
kutekeleza masuala ya lishe hususan katika ngazi za mikoa na
halmashauri, ambapo takwimu zinaonesha kuwepo kwa ongezeko kutoka
wastani wa sh. milioni 65 mwaka 2011/2012 hadi kufikia sh. milioni 219
mwaka 2016/2017.
Kwa
mwaka 2017/2018 Serikali ilikadiria kutumia jumla ya sh. billioni 11
katika utekelezaji wa masuala ya lishe katika ngazi ya halmashauri,
hivyo hadi kufikia robo ya tatu ya mwaka 2017/2018, kiasi cha sh.
bilioni mbili zilitolewa na kutumika.
Kadhalika,
Waziri Mkuu aliendelea kuhimiza kuhusu suala la kutenga kiasi cha
shilingi 1,000 kwa idadi ya watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano
katika Halmashauri zetu kupitia mapato ya ndani ili ziweze kutumika
katika kutekeleza Afua hizo kwenye Halmashauri husika.
Aliwahakikishia
wadau hao kuwa, Serikali itaendelea kutenga fedha kwa ajili ya
kugharamia utekelezaji wa Afua za Lishe kama zilivyoainishwa katika
Mpango wa Taifa wa Utekelezaji wa Masuala ya Lishe 2016/2017 –
2020/2021; kwa kadiri hali itakavyoruhusu.
“Nitoe
rai kwa Watendaji Wakuu wote katika Wizara husika, Idara, Wakala na
Taasisi za Serikali, wadau wa maendeleo, asasi za kijamii; kila mmoja
kwa nafasi yake au mamlaka yake, kuendelea kutenga fedha kwa ajili ya
utekelezaji wa Mpango wa Taifa wa Utekelezaji wa Masuala ya Lishe.”
Alisema
mikoa na halmashauri zihakikishe kuwa afua zilizoainishwa katika mpango
huo zinajumuishwa katika mipango na bajeti zao za kila mwaka, sambamba
na kutoa fedha zilizopangwa kwa ajili ya utekelezaji.
Waziri
Mkuu alisisitiza tena kuwa kila mdau anayeshiriki katika utekelezaji wa
shughuli za lishe nchini aoneshe bayana mchango wake katika kukabiliana
na utapiamlo nchini ili Taifa liweze kufikia malengo tuliyojiwekea.
Alisema
ili wahakikishe hatua tunazochokua katika mapambano dhidi ya utapiamlo
zinaleta matokeo kama walivyopanga na zinawanufaisha au zinawafikia
walengwa, aliwaagiza viongozi wa Serikali katika ngazi mbalimbali
kutambua wajibu wao na kushiriki kikamilifu katika kudhibiti na
kukabiliana na athari za utapiamlo katika maeneo yao.
Pia,
Waziri Mkuu aliwataka viongozi hao wa Serikali katika ngazi za
mbalimbali wafanye tathmini ya ufanisi wa hatua wanazochukua na watoe
taarifa za ufanisi au changamoto mara kwa mara.
Kwa
upande wake,Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi,
Vijana, Ajira na Walemavu, Jenista Mhagama alisema ushirikishwaji wa
wadau kwenye masuala ya lishe umeongezeka na wanashuhudia wadau wengi wa
maendeleo wakionesha nia na wengine kuwekeza katika masuala ya lishe
nchini.
Aidha,
Waziri Jenista alisema wameweza kuratibu wa uanzishwaji wa mabaraza
mbalimbali yanayojadili masuala ya lishe likiwemo baraza la sekta
binafsi ambao wana mchango mkubwa katika kuhakikisha azma ya Serikali ya
kutokomeza utapiamlo inafikiwa.
Alisema
hatua hizo kwa kiasi kikubwa zimechangia kupunguza viwango vya
utapiamlo pamoja na idadi ya vifo kwa watoto wenye umri chini ya miaka
mitano. “Mfano mzuri ni pale tulipopunguza udumavu kutoka asilimia 42
mwaka 2010 hadi asilimia 34.4 mwaka 2016.”
Alisema
Taifa linahitaji nguvu kazi imara itakayohimili ushindani katika soko
la ajira na kuendeleza Tanzania ya Viwanda. Nguvu kazi hiyo inaanza
kujengwa kwa kuimarisha lishe bora hususan kuanzia pale mama anapokuwa
mjamzito hadi mtoto anapofika miaka miwili.
Awali,Waziri
wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu,
alisema viwango vya matatizo ya lishe vimepungua kwa baadhi ya viashiria
ingawa si kwa kiasi cha kuridhisha.
Alitaja
moja ya viashiria vya kupungua kwa matatizo ya lishe ni kushuka kwa
tatizo la udumavu, ambapo kwa sasa kuna wastani wa watoto watatu wenye
udumavu kati ya watoto 10 walio katika umri chini ya miaka mitano.
Waziri
Ummy alisema kuwa udumavu huathiri ukuaji wa mtoto kimwili na kiakili,
hivyo kupunguza uwezo wa kufanya vizuri shuleni na kupunguza ufanisi
wake katika maisha yake ya utu uzima.
Alitaja
mikoa ambayo imeathiriwa zaidi na tatizo hilo la lishe ni pamoja na
Rukwa, Njombe, Ruvuma, Iringa, Kagera, Mwanza na Geita, ambayo ina
wastani wa zaidi ya asilimia 40. Mikoa hiyo ni kati ya mikoa yenye
uzalishaji mkubwa wa chakula nchini.
“Ni
dhahiri kuwa, utatuzi wa suala hili unahitaji mbinu na hatua za haraka
pamoja na ushirikiano wa kila mmoja wetu. Kulingana na takwimu za
kidemografia na afya ya mwaka 2015/2016, watoto 106,000 wana utapiamlo
mkali ukilinganisha na watoto 340,000 wenye utapiamlo wa kadiri.”
Alisema
idadi hiyo inaashiria kuwa watoto hao wenye utapiamlo mkali wapo kwenye
hatari kubwa ya kupoteza maisha, ambapo hadi sasa changamoto kubwa
waliyonayo ipo katika utambuzi wa tatizo, utoaji wa rufaa, upatikanaji
wa chakula dawa na utoaji wa matibabu sahihi kwa watoto wenye tatizo
hilo.
Kadhalika,
Waziri Ummy alisema bado kuna hospitali chache zenye uwezo wa kutoa
huduma ya matibabu ya utapiamlo mkali. Juhudi zinaendelea kuhakikisha
hospitali zote nchini zinajengewa uwezo wa kutoa huduma hizo muhimu ili
kuokoa maisha ya watoto walioathirika na utapiamlo mkali.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU
No comments:
Post a Comment