UFAFANUZI KUHUSU SUALA LA HASSAN MWAKINYO
Kama
 mnavyokumbuka, majuma mawili yaliyopita nchi yetu ilipata sifa kubwa 
sana kwenye tasnia ya michezo hususan mchezo wa ngumi za kulipwa baada 
ya Hassan Mwakinyo kumpiga Sam Eggington kwa TKO raundi ya pili katika 
pambano la raundi 10 lisilo la mkanda lililofanyika tarehe 8 Septemba, 
2018 huko Birmingham, Uingereza. Ushindi wa Mwakinyo, uliipeperusha 
vyema bendera ya nchi yetu.
Aliporejea
 kutoka Uingereza, Mwakinyo alipata mwaliko wa kufika katika bunge la 
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania siku ya ijumaa tarehe 14 Septemba, 2018.
 Pamoja na kumpa pongezi, wabunge walimpatia zawadi kwa kulitangaza 
vyema taifa letu.
Mara
 baada ya kutoka bungeni, akiwa katika viwanja vya bunge, Mwakinyo 
alifanya mkutano na waandishi wa habari, pamoja na mambo mengine, 
alizungumzia safari yake ilivyokuwa mpaka amefanikiwa kupata ushindi. 
Mwakinyo aliueleza umma kwamba alipata changamoto nyingi kwenye safari 
hiyo kama vile kulazimika kukopa hela ya viza kutoka kwa mwanafunzi na 
kusafiri bila ya kibali na hivyo kulazimika kusafiri kama mkimbizi.
Kamati
 inapenda kutolea ufafanuzi suala la kibali na kwa uchache kuhusu suala 
la viza. Kwanza si kweli kwamba Mwakinyo amesafiri bila ya kupata 
kibali, wakala aliyekwenda na Mwakinyo aliwasilisha maombi yake ya 
safari hiyo ndani ya siku 7 kabla ya safari. Kamati iliyajadili na 
kupitia kumbukumbu mbalimbali za Mwakinyo pamoja na mpinzani wake na 
iliridhia kumwombea kibali ili aweze kusafiri kwa ajili ya pambano hilo.
 Maombi ya kibali toka katika Kamati kwenda katika Baraza la Michezo la 
Taifa (BMT) yaliwasilishwa tarehe 3 Septemba, 2018 kwa “maombi ya 
dharura” na tarehe 5 Septemba, 2018 Kibali kilitolewa na nakala yake 
kutumiwa wakala aliyewasilisha maombi hayo ndugu Rashid Nassor ambaye 
ndiye aliyesafiri naye siku hiyo hiyo.
Ndugu
 waandishi wa habari, naomba ikumbukwe kwamba, kwa mujibu wa Kanuni za 
BMT, maombi ya vibali vya kusafiri nje ya nchi kwa shughuli za kimichezo
 yanapaswa kuwasilishwa siku 14 kabla ya safari. Inapoonekana kwamba 
safari hiyo ina tija kwa mchezaji na taifa kwa ujumla, BMT hutumia 
busara na kutoa kibali nje ya muda kama ilivyofanya kwa Mwakinyo ambaye 
alipata kibali ndani ya siku 2 tu. Hivyo, napenda kusisitiza kwamba, 
Hassan Mwakinyo alipata kibali kama nilivyoeleza hapo juu na nichukue 
fursa hii kumwomba radhi Katibu wa BMT pamoja na watendaji wote kwa 
kadhia hii.
Vilevile,
 kwa kifupi, napenda ifahamike kwamba, suala la viza ni jukumu la 
promota na wakala/bondia mwenyewe na pesa hiyo huwa inarudishwa na 
promota wanapofika huko kwenye pambano. Hivyo, tunasikitika kwa 
changamoto hiyo aliyopitia kupata visa lakini tunaamini kuwa 
wamerudishiwa na labda wakala aliyekwenda naye ndugu Rashid Nassor 
anaweza kulitolea ufafanuzi zaidi.
Mwisho,
 Kamati inapenda kuchukua fursa hii kumpongeza tena Hassan Mwakinyo kwa 
ushindi wake na iko tayari kumshauri kuhusu mustakbali wake mara baada 
ya ushindi huo kama ataona inafaa.
Imetolewa na:
Yahya Poli
Katibu – Kamati ya Kusimamia Ngumi za Kulipwa Tanzania.
17 Septemba, 2018






No comments:
Post a Comment