Serikali
wilayani Nkasi mkoani Rukwa, imeagiza kukamatwa kwa wazazi wa
mwanafunzi wa darasa la tatu katika Shule ya Msingi Mkinga aliyepata
ujauzito kwa kosa la kuandaa mpango wa kumuoza mwanafunzi huyo.
Agizo
hilo lilitolewa jana na Mkuu wa Wilaya hiyo, Said Mtanda, wakati
akikabidhi pikipiki 28 zenye thamani ya Sh. milioni 98 zilizotolewa na
Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, kwa kushirikiana na
Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi).
Fedha hizo zilitolewa kwa ajili ya mpango wa kukuza stadi za kusoma, kuandika na kuhesabu kwa waratibu kata wa wilaya hiyo.
Alisema
katika kijiji cha Mkinga kuna mwanafunzi wa darasa la tatu amepata
ujauzito na wazazi wake walikuwa wanaandaa mkakati wa kumuozesha, lakini
walishindwa baada ya Mwalimu Mkuu wa shule hiyo kuingilia kati na
kuvuruga mpango huo.
"Naagiza
wazazi wote wa mwanafunzi huyo wakamatwe mara moja, mwanafunzi huyo
pamoja na aliyempa mimba wafikishwe katika vyombo vya dola, ili sheria
ichukue mkondo wake na ninyi waratibu elimu kata tambueni mna jukumu
kubwa la kuhakikisha mimba hizi zinakwisha, " alisema.
Mtanda
alisema hali hiyo inaonyesha kuwa bado tatizo la mimba ni kubwa kwa
sababu katika mwezi uliopita jumla ya wanafunzi 27 walipata ujauzito,
hivyo bado kuna kazi kubwa ya kufanya.
Kwa
upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Misana Kwangula,
alisema lengo la serikali kuwapatia pikipiki hizo ni kuwawezesha
kutembelea shule zilizopo katika kata zao kwa kuwa walikuwa wanalalamika
kuwa hawana vitendea kazi vya kuwawezesha kufanya ukaguzi katika shule
wanazozisimamia.
No comments:
Post a Comment