Wakazi Mtaa wa Majengo Kahama waiomba serikali kuimarisha mitaro ya maji kukinga nyumba zao kuharibiwa

Related image

Baadhi ya Wananchi wa Mtaa wa Majengo katika Halmashauri ya Mji wa Kahama wameiomba halmashauri hiyo kujenga na kuiimarisha mitaro ya maji katika barabara zote za mitaa ili kuzuia maji ya mvua yasielekee kwenye makazi ya watu.

Wakizungumza leo kwenye kipindi cha Raha ya leo, kinachorushwa na Kahama Fm baadhi Wananchi hao wamesema bado barabara nyingi za mitaa hazipitiki kutokana na kuharibiwa na mvua wakati wa masika na kwamba hali hiyo pia inahatarisha afya zao.

Katika hatua nyingine wananchi hao wameishauri serikali kuiangalia kwa jicho la pili kata ya Majengo katika suala la utiririshaji wa maji machafu yanatoa harufu mbaya na kuhatarisha afya za wananchi wa mtaa huo.

Diwani wa Kata ya Majengo BERNAD MAHONGO amesema ujenzi wa mitaro katika kata ya Majengo unaendelea kufanyika katika maeneo yote korofi ili kuzuia maji yasituame na kusambaa kwenye makazi ya watu.

Kata ya Majengo ni miongoni mwa Kata za halmashauri ya Mji wa Kahama ambazo zimekuwa zikikumbwa na athari ya maji ya mvua kuingia kwenye makazi ya watu jambo ambalo limekuwa likileta hofu na kuhatarisha usalama na afya za wananchi.
Share:

Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga lakamata wawili kwa kujifanya Usalama wa Taifa

Image result for SIMON HAULE IMAGES



Jeshi la polisi Mkoa wa SHINYANGA linawashilikia watu wawili GOGADI SULEIMAN (62) na KILIMA MBWILIZA (49) kwa tuhuma ya kujifanya watumishi wa umma katika idara ya usalama wa taifa na kuwakuta na baadhi ya vitambulisho bandia vya usalama wa taifa.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa SHINYANGA SIMON HAULE amesema watuhumiwa hao wamekamatwa majira ya saa 1:30 usiku mjini shinyanga na kukutwa na vitu feki mbalimbali ambavyo ni vya kiserikali.

Vitu walivyokutwa navyo watuhumiwa hao ni pamoja na fomu za maombi ya kazi idara ya usalama wa taifa, picha mbalimbali za watu, vipimo vya nguo (Suti), na Nyaraka mbalimbali za serikali

Kamanda HAULE amesema watuhumiwa hao wakati wanakamatwa walikutwa na binti mmoja ambaye walikuwa katika mazungumzo naye ya kumtaka awapatie Tsh. Mil 1 ili apewe kazi katika idara ya usalama wa taifa.

Jeshi la polisi Mkoa wa SHINYANGA linatoa wito kwa wanancho wote kuwa shughuli zote za serikali hufanyika katika ofisi za serikali zinazotambulika kisheria na sio katika maeneo mengine.

Share:

Meli mbili za Mv Nyakibare na Orion II, zawasili kukinasua kivuko Mv Nyerere kisiwani Ukara

Mitambo na vifaa maalum vya kunyanyua, kubeba na kuvuta vitu vizito imewasili katika gati ya Bwisya kisiwa cha Ukara wilayani Ukerewe tayari kufanya kazi ya kunyanyua na kugeuza kivuko cha Mv Nyerere kilichopinduka katika ziwa Victoria.

Mpaka kufikia jana wataalam wa uokoaji na masuala ya majini walifanikiwa kukilaza ubavu kivuko hicho ambacho awali kililala kifudifudi tangu kilipopinduka Septemba 20.

Mitambo na vifaa hivyo vimewasili asubuhi ya leo vikiwa ndani ya meli mbili kubwa binafsi za Mv Nyakibaria ya kampuni ya Mkombozi and Fisheries na Mv Orion II inayomilikiwa na kampuni ya Kamanga Ferry, zote za jijini Mwanza.

Akizungumza na waandishi wa habari jana jioni, Mwenyekiti wa Kamati ya Maafa ya Mv Nyerere, Isaac Kamwelwe alisema mitambo na vifaa hivyo vitarahisisha kazi ya kunyanyua, kugeuza na kukivutia ufukweni kivuko hicho.
Share:

Waziri Lugola Afuta Utaratibu Wa Utoaji Vibali Kwa Wananchi Wanaolima Jirani Na Kambi Za Wakimbizi Nchini

WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola amewataka wananchi wa Kakonko wanaolima jirani na Kambi ya Wakimbizi ya Mtendeli, pamoja na kambi zingine zote zilizopo mkoani Kigoma waendelee kulima bila kuomba kibali chochote kama ilivyoagizwa awali.

Waziri Lugola amefuta utaratibu huo wa utoaji wa vibali kwa ajili ya kuruhusiwa kwenda kulima katika maeneo hayo, baada ya wananchi wilayani humo kuulalamikia utaratibu huo ambao walisema unawafanya wasiwe huru na unawachelewesha kuendeleza shughuli zao za kilimo kama ilivyokua awali.

Akizungumza katika mkutano wa hadhara uliohudhuriwa na mamia ya wananchi mjini Kakonko, Mkoani Kigoma, jana, Lugola alisema Serikali ya Awamu ya Tano haitaki wananchi wake wanyanyaswe, wananchi wanapaswa kua huru katika nchi yao.

 “Naagizia huu utaratibu ufutwe na wananchi wawe huru kwenda kulima katika maeneo ambayo yapo jirani na hiyo kambi pamoja na kambi zinginezo, na pia wasisumbuliwe na mtu yeyote, ” alisema Lugola.

Pia Waziri Lugola alielekeza baadhi ya wananchi ambao hawajalipwa fidia wakati mashamba yao yalipochukuliwa kwa ajili ya kuanzisha kambi hiyo wafanyiwe uhakiki ili waweze kulipwa haki zao.

Hata hivyo, Mratibu wa Idara ya Wakimbizi Kanda ya Kigoma, Tony Laiser ambaye alikuwepo katika mkutano huo alipokea maagizo hiyo na kuahidi kuyatekeleza.

Aidha, kabla ya mkutano huo wa hadhara, Waziri Lugola alizungumza na  watendaji waliopo katika wizara yake mkoani humo na alisema Serikali imepeleka mafunzoni vijana 1,500 kwaajili ya kujiunga na Jeshi la polisi pamoja na kuagiza magari kwa ajili doria.

Pia aliwataka watendaji hao kufanya kazi kwa bidii kwani serikali yao ipo na inawajali na pia itahakikisha inatatua kero zao ambazo zinawakabili ikiwemo ukosefu wa majengo, upungufu wa vitendea kazi na uhaba wa askari katika sehemu mbalimbali nchini.
Share:

Rais Magufuli Katengua Uteuzi wa Naibu Waziri wa Mambo ya Nje, Susan Kolimba




Share:

Serikali Kuendelea Kushirikiana Na Wadau Kuboresha Elimu Nchini.

 
Serikali imesema itaendelea kushirikiana na wadau wa maendeleo nchini ili kuhakikisha kila mtoto wa kitanzania anapata elimu bora.

Hayo yameelezwa leo Jijini Dodoma na Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia, Mhe. Prof. Joyce Ndalichako alipokuwa akifungua Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Wadau wa Elimu wa kujadili mafanikio na changamoto za elimu nchini.

“Mkutano huu ni muhimu sababu unapitia na kujadili mafanikio na changamoto katika sekta ya elimu na kutoa mapendekezo ya changamoto hizo ili kuboresha sekta hii,” amesema Prof. Ndalichako.

Aidha, amesema Serikali itaendelea kutumia mapendekezo yanayotolewa na wadau wa maendeleo ya elimu nchini ili kuhakikisha hakuna mtoto wa Kitanzania anaachwa nyuma katika kupata elimu bora mijini na vijijini.

Amesema, Serikali ya Awamu ya Tano imekuwa na mafanikio makubwa katika sekta ya elimu ambapo imefanikiwa kutoa elimu bila malipo kwa shule za msingi na sekondari, mafunzo kwa mbalimbali kwa walimu, walimu wamepangiwa kazi kulingana na uhitaji pamoja na kuendelea kuwaajiri.

Vile vile Wadhibiti Ubora wa Elimu wamewezeshwa kwa kununuliwa magari na pikipiki ili kuzifikia shule kwa urahisi.

Prof. Ndalichako amewataka wadau hao kuutumia mkutano huo kujadili na kutoa mapendekezo ya namna ya kuimarisha ufundishaji wa masomo ya sayansi, kuunganisha elimu ya nadharia na vitendo, mafunzo ya walimu, elimu yenye usawa mijini na vijijini pamoja na mahudhurio shuleni.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia, Dkt. Leonard Akwilapo amesema mkutano huo umehusisha wadau mbalimbali wa elimu hapa nchini zikiwemo taasisi za utafiti, wadau wa maendeleo ya elimu, maafisa elimu pamoja na wanafunzi ambapo kwa pamoja watajadili mafanikio na changamoto katika sekta ya elimu na kutoa mapendekezo ya namna ya kukabiliana na changamoto hizo.
Share:

KCB Bank wachangia Mil 125 maafa ya ajali ya Mv Nyerere

Bodi ya Wakurugenzi, Menejimenti na Wafanyakazi wa KCB Bank Group, wameungana na waombolezaji wa msiba uliotokana na kuzama kwa kivuko cha MV Nyerere kwa kuchangia kiasi cha fedha taslim shilingi 125,000,000/=

Akikabidhi msaada huo wa fedha Mkurugenzi wa Bodi ya KCB, Zuhura Muro, alieleza kuwa wameguswa na maafa hayo na hivyo wanaahidi kuungana na serikali kadri wanavyoweza.

"Tunajua hatuwezi kumaliza shida au mahitaji ya waathirika hawa, hivyo tunapenda kuhamasisha taasisi nyingine zinazoguswa  kama sisi kutoa misaada yao ya hali na mali, huku tukiwaombea marehemu wapumzike  kwa amani na majeruhi majeruhi wapate kupona haraka," amesema.

Kutokana na kiasi hicho kilichotolewa na Bank KCB pamoja na michango ambayo  wananchi na tasisisi mbalimbali zilizoguswa na kuchangia rambirambi katika maafa hayo imefikia jumla ya shilingi milioni 557
Share:

Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Meja Jenerali Gaudence Milanzi astaafu utumishi wa umma


Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Meja Jenerali Gaudence Milanzi amewataka watumishi wa wizara hiyo kufanyakazi kwa weledi ili kuogeza tija kwa Taifa.

Katibu mkuu huyo ametoa rai hiyo leo, Septemba 25, 2018 alipokuwa akiwaaga watumishi wa wizara baada ya kustaafu jeshini na kwa mujibu wa sheria tangu Septemba 16.

Milanzi amesema kwa muda wote aliitumikia wizara hiyo alipata ushirikiano wa kutosha uliomuwezesha kuiongoza vyema wizara hiyo na kuchangia mafanikio yaliyojidhihirisha kwenye sekta za wanyamapori, utalii, misitu na nyuki na malikale.

Katika kipindi cha uongozi wake wizarani hapo, amesema wizara imepata mafanikio katika  vita dhidi ya ujangili.

“Tumekamilisha mambo mengi. Kila mmoja wenu alikuwa akinisaidia ili wizara isonge mbele. Hakuna aliyetaka kunikwamisha. Ninawashukuru sana,” amesema Milanzi.

Akizungumza kwenye hafla fupi ya kumuaga Milanzi iliyofanyika ukumbi wa mikutano wa Chuo Kikuu cha Dodoma, kaimu katibu mkuu wa wizara hiyo, Dk Aloyce Nzuki amempongeza kwa utumishi wake.

“Umeweka mifumo mizuri na kubuni mikakati na mbinu za kutatua changamoto zilizokuwa zinaikabili wizara na kuhakikisha watumishi wanapata utulivu wa akili kwa kujali maslahi yao. Uliwawezesha kufanya kazi wakiwa watulivu wa akili jambo liliongeza ufanisi kazini,” ameeleza Dk Nzuki.

Milanzi aliteuliwa kuwa katibu mkuu wa wizara hiyo Disemba 2015. 
“Nashukuru nimestaafu salama. Wizara hii ni muhimu sana kwa maendeleo ya nchi na inagusa masilahi ya wengi. Jukumu nililopewa lilikuwa kusimamia maslahi ya nchi, naamini kuna masilahi ya watu yalivurugwa hivyo mimi kuwa mwiba kwao,” amesema akiaga kamanda huyo wa Jeshi la Wananchi (JWTZ).
Share:

Kiswahili Kuwa Lugha Kuu Ya Mawasiliano Barani Afrika

 
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt. Harrison Mwakyembe amebainisha kuwa lugha ya Kiswahili inatarajiwa kuwa lugha kuu ya mawasiliano katika bara la Afrika ifikapo mwaka 2063.

Waziri Mwakyembe ameyasema hayo jana Jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maadhimisho ya Kampeni Ya Uzalendo na Utaifa kwa mwaka 2018 yanayotarajiwa kufanyika Desemba 8 Jijini Dodoma ambapo mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Rais John Pombe Magufuli.

Alisema kuwa kampeni hiyo kwa mwaka huu imejikita katika kuhamasisha matumizi ya lugha ya Kiswahili ambayo ni kielelezo kikubwa cha utashi na uhai wa taifa la Tanzania na inakua kwa kasi sana barani Afrika na duniani kote kwa ujumla.

“Sasa hivi Kiswahili ni lugha ya kumi kati ya lugha elfu 6 zinazoongelewa na watu wengi duniani na kwa mujibu wa Tafiti za Umoja wa Afrika zinaonesha kuwa ifikapo mwaka 2063 Kiswahili kitakuwa lugha kuu ya mawasiliano katika bara la Afrika na utambulisho wa mtu mweusi duniani,” alisema Mwakyembe.

Alieleza kuwa dunia yote inatambua kwamba Tanzania ndio chimbuko la lugha adhimu ya Kiswahili hivyo watanzania wanapaswa kujivunia lugha hiyo na kuitangaza kwa kuwa ni sehemu ya utamaduni wa taifa na msingi wa uzalendo na utaifa.

Waziri Mwakyembe alibainisha kuwa kampeni hiyo mwaka huu imejikita katika kuhamasisha matumizi ya lugha ya Kiswahili ili kuwasisitiza watanzania kuthamini lugha yao na utamaduni wao na kurejea kwenye misingi ya maadili ya taifa lao.

Alisema kuwa sasahivi kuna changamoto kubwa ya mmomonyoko wa maadili inayosababishwa na baadhi ya watu hasa vijana kuiga tamaduni za nje kutokana na utandawazi hivyo kupelekea kudharau utamaduni wao ikiwemo lugha ya Kiswahili jambo ambalo lisipochukuliwa hatua madhubuti litaleta athari kwa jamii.

Pia Waziri Mwakyembe alitoa pongezi kwa Rais John Pombe Magufuli kwa mchango wake mkubwa anaoonesha katika kutumia, kukuza na kuitangaza lugha ya Kiswahili ndani na nje ya nchi hivyo amekuwa ni mfano wa kuigwa.

Aidha alitoa rai kwa watanzania wote na wadau mbalimbali kuunga mkono kampeni hiyo kwa hali na mali ili Tanzania iweze kufanikiwa kulinda misingi ya utamaduni na utaifa hususan lugha ya Kiswahili.

Kampeni ya Uzalendo na Utaifa ilianza rasmi mwaka jana 2017 na itakuwa ikiadhimishwa kila mwaka ambapo kwa mwaka huu kauli mbiu yake ni ‘Kiswahili Uhai Wetu, Utashi Wetu’. 
Share:

Waziri: “Sehemu Pekee Ya Vijana Kuimarisha Kipato Ni Kupitia Sekta Ya Kilimo”

Imeelezwa kuwa sehemu pekee ya kuimarisha kilimo cha mwananchi mmoja mmoja, wananchi katika makundi ya kijamii hususani vijana ni kupitia sekta ya kilimo kwani ndio sehemu pekee ya ukombozi wa mkulima katika jamii.

Imeelezwa kuwa kuna uwezekano wa kufanya biashara mbalimbali nchini ambazo zinaweza kuongeza kipato lakini sahemu sahihi isiyokuwa na jazba na dhoruba katika utendaji ni kufanya kilimo biashara ambacho kamwe hakiwezi kumtupa mkulima.

Dkt Charles Tizeba Waziri wa kilimo, ameyasema hayo leo tarehe 25 Septemba 2018 wakati akizungumza na vijana wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Mkoa wa Tanga ambao wapo katika kambi maalumu ya ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Muheza.

Vijana hao ambao wameamua kutumia nguvu zao pasina malipo wameamua kwa umoja wao kuunga mkono juhudi za Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Taifa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dkt John Pombe Magufuli kwa kauli yake inayohamasisha chachu na juhudi za kiutendaji kwa wananchi ya “Hapa Kazi Tu”.

Aidha, katika kuhamasisha juhudi za kiutendaji Waziri huyo mwenye dhamana ya kilimo ameunga mkono juhudi za vijana hao kwa kuchangia fedha ya chakula shilingi 1,100,000 sambamba na kushiriki ujenzi wa jengo maalumu la upasuaji.

Waziri wa kilimo Mhe Dkt Charles Tizeba alitembelea ujenzi huo wa Hospitali ya Wilaya ya Muheza akiwa safarini kutembelea mashamba ya mkonge ikiwa ni siku ya pili ya ziara ya kikazi Mkoani Tanga aliyoianza jana tarehe 25 Septemba 2018 ya kukutana na makundi mbalimbali ya wakulima wa zao la Mkonge ili kutafuta ufumbuzi wa changamoto zinazowakabili wakulima wa zao hilo.
Share:

TCU Yasitisha Udahili wa Wanafunzi Kwa Vyuo 7.....Viwili Vyafungiwa

Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU), imesitisha masomo na udahili wa wanafunzi wapya kwa ngazi zote za masomo na katika programu kwenye baadhi ya vyuo vikuu kutokana na kukosa vigezo.

Pia imefuta vituo viwili vya vyuo vikuu na kuamuru wanafunzi wanaoendelea na masomo wahamishwe.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo Jumanne Septemba 25, Katibu Mtendaji wa TCU, Profesa Charles Kihampa amevitaja vyuo hivyo kuwa ni pamoja na Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Kampala nchini (KIUT), Chuo cha Teofilo Kisanji (TEKU), Chuo Kikuu kishiriki cha Marian (MARUco) na Chuo Kikuu Kishiriki cha Kumbukumbu ya Kardinali Rugambwa  (CARUMUCo).

Vyuo vingine ni Chuo cha kumbukumbu ya Sebastian Kolowa (SEKOMU), Chuo kikuu cha Mt. Yohana cha Tanzania (SJUT-St. Marks Centers na Chuo kikuu cha Umoja wa Afrika Tanzania (UAUT).

Vyuo hivyo ni pamoja na Chuo kikuu Teofilo Kisanji, Kituo cha Tabora  na Chuo kikuu Mt. Yohana cha Tanzania, Msalato (SJUT -Msalato Center).

Aidha, amevitaja vyuo vilivyositishiwa utoaji mafunzo na kuamuru wanafunzi wote wanaoendelea na masomo wahamishwe kuwa ni Mlima Meru (MMU), Chuo Kikuu cha Bagamoyo (UoB), Chuo cha Eckernforde Tanga (ETU) cha Kilimo na Teknolojia cha Jomo Kenyatta Kituo cha Arusha na Chuo Kikuu Kishiriki cha Josiah kibira (JOKUCo).

“Asitokee mwanafunzi yeyote akasajiliwa katika vyuo hivyo na wanaotakiwa kuhama wawasiliane na vyuo vyao haraka,” amesema Profesa Kihampa.

Kwa upande wake mwakilishi kutoka Bodi ya Mikopo (HELSB), Deus Changala amesema waliokuwa na mikopo wasiwe na wasiwasi itapelekwa watakapokuwa.
Share:

Kila Mfiwa Ajali ya MV Nyerere Kulipwa Milioni 1 Badala ya Laki 5

Rais John Magufuli ameagiza wafiwa wote waliopoteza ndugu zao kwenye ajali ya kivuko cha Mv Nyerere kupata Sh 1 milioni baada ya awali kupewa Sh 500,000 kila mmoja.

Hata hivyo watu 41 walionusurika kwenye ajali hiyo nao watapewa Sh1 milioni kila mmoja.

Fedha hizo zinatokana na michango ya kampuni, watu na taasisi mbalimbali wanaoendelea kujitokeza kuchangia waathirika hao.

Awali, familia za waliopoteza maisha kwenye ajali hiyo iliyotokea Alhamisi iliyopita walipewa Sh500,000 kwa kila mtu aliyefariki, fedha ambazo zimepatikana kutokana na michango ya Watanzania, kampuni na taasisi mbalimbali.

Akizungumza na vyombo vya habari jana kisiwani Ukara wilayani Ukerewe, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Isaac Kamwelwe alisema leo wataanza kutoa fedha hizo kama walivyoagizwa na Rais Magufuli kwa familia za marehemu na wote walionusurika.

“Rais ameniagiza niwaambie kwamba fedha kwa waliopoteza ndugu zao na wale 41 walionusurika, sasa watapata Sh1 milioni kila mmoja. Kuanzia kesho (leo) tutaanza kutoa fedha hizo, wapeni taarifa,” alisema Kamwelwe.

Alisema kiwango cha fedha kilichokusanywa mpaka jana jioni ni Sh397 milioni ambazo zimetolewa na watu na taasisi mbalimbali. Alisema Rais Magufuli amesema fedha hizo ni za wananchi walioathirika na ajali hiyo.

Waziri huyo alisema mpaka kufikia jana jioni, miili miwili ya watoto ilipatikana wakati kazi ya kukiinua kivuko hicho ikiendelea na kufanya idadi ya waliopoteza maisha kwenye ajali hiyo kufikia 226.

Kuhusu kurudisha hali ya usafiri katika kisiwa hicho, Kamwelwe alisema leo au kesho kitapelekwa kivuko kingine kinachoitwa Mv Temesa ambacho kiko Mwanza kwa ajili ya kutoa huduma wakati shughuli ya kukiinua kivuko cha Mv Nyerere ikiendelea.
Share:

Waziri Lugola Aibukia Kituo Cha Polisi Katoro, Awahoji Watuhumiwa Makosa Yao Wakiwa Wamepanga Foleni Mahabusu

WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola amefanya ziara ya kushtukiza katika Kituo cha Polisi Katoro mkoani Geita  na kuwahoji watuhumiwa wa makosa mbalimbali waliokuwepo katika mahabusu kituoni hapo.

Lugola ambaye alikua safarini kuelekea Mkoani Kigoma kwa ziara yake ya kikazi, ghafla aliibukia katika kituo hicho akitaka kujua utendaji kazi wa polisi pamoja na makosa mbalimbali wanayowakabili watuhumiwa waliopo katika mahabusu hiyo na pia kujua changamoto mbalimbali zinazowakabili askari wa kituo hicho.

Lugola aliowasili kituoni hapo jana mchana na akaelekea moja kwa moja mahabusu na akaomba kitabu cha taarifa ya makosa mbalimbali yaliyoripotiwa kituoni hapo, na akamuelekeza askari wa zamu awapange foleni watuhumiwa hao ili aweze kuwahoji makosa yao na pia Mkuu wa Kituo cha polisi hicho, aweze kufafanua makosa yao.

Baada ya watuhumiwa hao, Lugola licha ya kuwapongeza polisi wa kituo hicho kwa kufanya kazi vizuri, pia alimtaka Mkuu wa Kituo hicho, Steven Kimaro kua makini na utendaji wake na kuwafuatilia kwa umakini utendaji kazi wa askari wake kwasababu yeye ndio kiongozi wa kituo hicho.

“Sipendi wananchi waonewe, haki itendeke na si kila kosa lazima mtuhumiwa awekwe mahabusu, tumieni busara umakini ili tuweze kutenda haki na pia nataka jeshi hili liwe na picha nzuri zaidi kwa jamii,” alisema Lugola.

Pia alifafanua kua, hataki kusikia askari polisi anatuhumiwa kwa rushwa au kunyanyasa wananchi, na endapo taarifa hizo zitamfikia basi atahakikisha askari huyo anachukulia hatua za kisheria.

Aidha, Waziri Lugola alitaka polisi wa usalama barabarani kufuata sheria na pia si kila kosa lazima mwenye gari kuandikiwa risiti ya malipo, makosa mengine watoe elimu zaidi kwa madereva hao ili taifa liweze kusonga mbele.

Lugola Septemba 25 anatarajia kuanza ziara yake ya kutembelea mikoa yote nchini, ambapo ataanza ziara katika Wilaya ya Kakonko mkoani Kigoma ambapo atazungumza na askari na maafisa polisi, watumishi wa taasisi zilizopo katika wizara yake na baadaye atafanya mkutano wa hadhara kwa kuzungumza na wananchi pamoja na kusikiliza kero zao mjini humo.
Share:

CCM Yatoa Mil. 10 Kwa Ajili Ya Kusaidia Wahanga Wa Ajali Ya Mv Nyerere

CHAMA cha Mapinduzi (CCM) kimetoa kiasi cha Sh. 10 milioni kwa ajili ya kusaidia wahanga wa ajali ya MV Nyerere iliyotokea tarehe 20 Septemba 2018.

Fedha hizo zimekabidhiwa kwa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi, Isaack Kamwele na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole.

Makabidhiano hayo yalifanyika  katika kijiji cha Bwisya kisiwani Ukara, Septemba 24, 2018 na kushuhudiwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.
Share:

Taarifa Kwa Umma Kuhusu Salamu Za Rambirambi Kutoka Mataifa Mbalimbali Na Balozi Za Tanzania Nje Ya Nchi

Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki imeendelea kupokea salamu za rambirambi kutoka kwa marais, mawaziri wakuu wa mataifa mbalimbali duniani kwenda kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, kufuatia ajali ya kuzama kwa kivuko cha MV Nyerere iliyotokea kwenye Ziwa Victoria, Mkoani Mwanza tarehe 20 Septemba, 2018 na  kusababisha vifo, majeruhi na upotevu wa mali.

Baadhi ya salamu zilizopokelewa ni pamoja na kutoka kwa Rais wa Kenya, Mheshimiwa Uhuru Kenyatta, Rais wa Urusi, Mheshimiwa Vladmir Putin, Rais wa China, Mheshimiwa Xi Jinping, Rais wa Ujerumani, Mheshimiwa Frank-Walter Steinmeier, Rais wa Saharawi, Mheshimiwa Brahim Ghali, Mtawala wa Kuwait, Mtukufu Sheikh Sabah Al-Ahmad al Jaber Al-Sabah, Baba Mtakatifu, Papa Francis, Rais wa Italia, Mheshimiwa Sergio Mattarella, Rais wa Uturuki, Mheshimiwa Recep Tayyip Erdogan, Rais wa Finland, Mheshimiwa Sauli Niinistö, Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Mheshimiwa Joseph Kabila Kabange na Rais wa Jamhuri ya Sudan, Mheshimiwa Omar Hassan Ahmed Al-Bashir. 

Viongozi wengine ni Waziri Mkuu wa Israel, Mheshimiwa Benjamin Netanyahu, na Waziri Mkuu wa Sweden, Mheshimiwa Stefan Löfven.

Viongozi hao wameeleza kusikitishwa kwao na taarifa za vifo vilivyosababishwa na  ajali hiyo na kuwatakia majeruhi kupona haraka.

Sehemu ya nukuu za salamu hizo zinasema “Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli, nilipokea kwa huzuni na masikitiko makubwa taarifa za ajali ya kivuko cha MV Nyerere iliyosababisha vifo vya watu wengi, majeruhi na wengine kutojulikana walipo. Kwa niaba ya Serikali na wananchi wa Kenya naomba upokee na kufikisha salamu zetu za rambirambi kwa wafiwa na wananchi wote wa Tanzania kufuatia ajali hiyo na tunawaombea majeruhi wote wapone haraka” ni sehemu ya nukuu ya salamu kutoka kwa Mheshimiwa Rais Kenyatta

“Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli, nilishtushwa na taarifa za ajali hiyo mbaya iliyotokea Mkoani Mwanza. Kwa niaba ya Serikali ya China, wananchi na mimi binafsi natoa pole kwa wafiwa wote na majeruhi” inasema sehemu ya salamu kutoka kwa Rais wa China, Mheshimiwa Xi Jinping.

Naye Rais wa Urusi, Mheshimiwa Putin amesema “Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli, tafadhali naomba upokee salamu zangu za rambirambi kufuatia ajali iliyotokea. Naomba salamu hizi ziwafikie wafiwa wote na ninawaombea majeruhi wapone haraka”

Aidha, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki imepokea salamu za rambirambi kutoka kwa balozi mbalimbali zinazowakilisha nchi zao hapa nchini pamoja na mashirika ya kimataifa yaliyopo nchini, ikiwemo ubalozi wa Marekani, ubalozi wa Ufaransa, ubalozi wa Sudan Kusini, Ubalozi wa Falme za Kiarabu (UAE), Serikali ya Brazil, Ubalozi wa Cuba, ubalozi wa Nigeria na salamu kutoka kwa Mratibu Mkazi wa Mashirika ya Kimataifa nchini.

Wakati huohuo, Wizara imepokea salamu za rambirambi kutoka kwa mabalozi wanaowakilisha Tanzania kwenye nchi mbalimbali. Salamu zilizopokelewa zinatoka kwa mabalozi wote wa Tanzania  katika nchi za Qatar, Ufaransa, Uingereza, Uholanzi, Afrika Kusini, Sweden, Nigeria, Burundi, Uganda, Kenya, Ubelgiji, Zambia, Msumbiji, China, Japan, Brazil, Comoro, Algeria, Sudan,  Canada,

Kadhalika tumepokea salamu kutoka kwenye balozi zetu zilizoko Marekani, Uturuki, Rwanda, Umoja wa Falme za Kiarabu, Misri, Kuwait, Saudi Arabia, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Zimbabwe, Malawi, Uswisi, India, Italia, Jamhuri ya Korea, Urusi, Israel, Ethiopia, Ujerumani, Oman na Malaysia.

Baadhi ya nukuu ya salamu za rambirambi za mabalozi hao zinasomeka kama ifuatavyo “Inna Lillah Wainna Illah Rajiuon.  Kwa  niaba  ya  Ubalozi  Abuja  na  Watanzania  waliopo  katika  eneo  letu  la  uwakilishi,  tunatoa  pole  kwa  Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,  familia  na  Watanzania  kwa  ujumla  kwa  msiba  mkubwa  uliotufika.  Mwenyezi  Mungu  atupe  subira  na  faraja  katika  kipindi  hiki  cha  majonzi  na  aziweke  roho  za  marehemu  mahali  pema  na  majeruhi  wapone  haraka, Amin  Amin,”  ni kauli yake Mheshimiwa Muhidin Ally Mboweto, Balozi wa Tanzania nchini Nigeria.

Naye Balozi wa Tanzania nchini Sweden, Mheshimiwa Dkt. Wilbroad Slaa anasema “kwa niaba ya wenzangu katika kituo cha Stockholm tunatoa pole za dhati kwa Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ndugu na familia zote zilizoguswa na msiba huu mkubwa. Mwenyezi Mungu azilaze roho za marehemu mahali pema peponi na kuwatia nguvu na ujasiri ndugu wote walioguswa na msiba huu”.

Kwa upande wake Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa Mheshimiwa Balozi Modest Mero alisema haya; “Ubalozi wa New York tunatoa pole kwa ajali mbaya ya Meli ya MV Nyerere iliyopelekea wengi kupoteza maisha na wengi kuumia.  Tunawaombea marehemu pumziko la milele na wote waliojeruhiwa wapone haraka.”

Balozi wa Tanzania nchini China, Mheshimiwa Mbelwa Kairuki alieleza masikitiko yake kwa kusema kuwa “nasi huku Beijing tunaungana na wenzetu kutoa pole kwa Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Watanzania na wanafamilia walioguswa msiba huu mzito. Mwenyezi Mungu awape nguvu na awajalie moyo wa subira wakati wote mnaposhughulika na msiba huo.

“Japan na diaspora yetu tunatoa pole kwa Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Watanzania wote kwa msiba huu uliotokana na kuzama kwa kivuko. Mungu atupe nguvu wote tuliobaki na awape pumziko la amani wenzetu waliotutangulia. Kwa majeruhi tunawaombea wapone haraka na wavumilie mstuko huu mkubwa katika maisha yao. Marehemu wapumzike kwa amani”. Hizi ni salamu kutoka kwa Mheshimiwa Mathias Chikawe, balozi wa Tanzania nchini Japan.

Kwa upande wake, Balozi wa Tanzania nchini Abu Dhabi alisema haya; “Ubalozi wa Tanzania Abu Dhabi, tumepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za ajali ya MV Nyerere.Kwa niaba ya watumishi wote wa Ubalozi, tunatoa mkono wa pole kwa Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Joseph Magufuli na Watanzania wenzetu wote kwa msiba huu mkubwa. Mwenyezi Mungu awajaalie marehemu wapumzike mahali pema na awajaalie majeruhi kupona mapema. Amin”.

Naye Balozi wa Tanzania nchini Uingereza, Mheshimiwa Dkt. Asha-Rose Migiro akieleza kuguswa na ajali hiyo alitoa kauli hii “Ubalozi wa Tanzania London unajumuika na Watanzania wenzetu kutoa pole kwa Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, familia na ndugu wa wale wote waliopatwa na msiba kutokana na ajali hii. Tunawaombea majeruhi wapone haraka na warejee katika shughuli zao za kujikimu na kulijenga taifa letu”.

Kwa upande mwingine, Wizara imepokea salamu za rambirambi kutoka Baraza la Diaspora wa Tanzania ulimwenguni kote (TDC Global) ambao wameeleza masikitiko makubwa kufuatia ajali hiyo mbaya. Sehemu ya ujumbe wao unasomeka kama ifuatavyo; “TDC Global, kwa masikitiko makubwa, inatoa salamu za rambirambi kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli na Watanzania wote, ndugu, jamaa na marafiki kwa vifo vilivyotokana na ajali ya kuzama kwa kivuko cha MV. Nyerere kinachofanya safari zake kati ya visiwa vya Bugorora na Ukara katika Ziwa Victoria. Kama TDC Global, tunaungana na Watanzania wote katika kuomboleza msiba huu mzito kwa taifa letu. Pia tunatoa pole kwa majeruhi wote na kuwaombea wapone haraka”.
Share:

Mwanafunzi Atiwa Mbaroni Kwa Kutupa Mtoto Chooni....Mwingine Akamatwa kwa Kumuua Ndugu yake kisa Redio

 
JESHIi la Polisi Mkoa wa Mbeya linamshikilia mwanamke mmoja ambaye amefahamika kwa jina la INES MTUNDU [19] Mwanafunzi wa Kidato cha Nne katika Shule ya Sekondari Isengo kwa kosa la kumtupa chooni mtoto mchanga wa masaa kadhaa.

Tukio hilo limetokea mnamo tarehe 23.09.2018 majira ya saa 09:53 asubuhi huko maeneo ya Isengo – Airport ya zamani, Kata ya Iyela, Tarafa ya Iyunga, Jijini Mbeya. Inadaiwa kuwa mwanafunzi huyo alikuwa mjamzito na mara baada ya kujifungua chooni ndipo alimtupa mtoto huyo.

Mara baada ya taarifa kulifikia Jeshi la Polisi, jitihada za haraka zilifanyika kwa kushirikiana na Kikosi cha Zimamoto na Uokoaji na kufanikiwa kumuokoa mtoto huyo akiwa hai. Mama na mtoto huyo wote wapo Hospitali ya Wazazi – Meta wakipatiwa matibabu. Upelelezi unaendelea na mara baada ya kukamilika mtuhumiwa atafikishwa Mahakamani.

KUPATIKANA NA BHANGI – KYELA.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linamshikilia mtu mmoja ambaye amefahamika kwa jina la GOLIATH EMANUEL [43] Mkazi wa Kasumulu Wilaya ya Kyela akiwa na dawa za kulevya aina ya bhangi debe sita nyumbani kwake.

Mtuhumiwa alikamatwa mnamo tarehe 22.09.2018 majira ya saa 23:47 usiku huko Kasumulu, Kata ya Ngana, Tarafa ya Unyakyusa, Wilaya ya Kyela katika msako uliofanyika maeneo hayo. Mtuhumiwa alikuwa ameificha bhangi hiyo katika mifuko ya salfeti nyumbani kwake. Upelelezi unaendelea na mara baada ya kukamilika mtuhumiwa atafikishwa Mahakamani.

MAUAJI – CHUNYA.
Mnamo tarehe 22.09.2018 majira ya saa 15:00 alasiri huko katika kitongoji cha kasisi, kijiji cha nkwangu, kata ya upendo, tarafa ya kipembawe, wilaya ya chunya, mtu mmoja aitwaye LUTONJA LUKELESHA [33] Mkazi wa Kasisi alifariki dunia akiwa anajipatia matibabu kienyeji nyumbani kwake.

Inadaiwa kuwa marehemu alipigwa fimbo sehemu mbalimbali za mwili wake na kukanyagwa kwa miguu kifuani na tumboni siku ya tarehe 12.09.2018 majira ya saa 12:09 mchana huko kijiji cha Kasisi na kaka yake aitwaye MASANILA LUKELESHA [45] Mkazi wa Kasisi akiwa na wenzake wawili.

Chanzo cha tukio hili ni tuhuma za wizi wa radio ndogo yenye thamani ya Tshs 15,000/= ya mmalila mchoma mkaa ambaye jina lake halisi bado kufahamika. Mtuhumiwa mmoja MASANILA LUKELESHA amekamatwa na msako mkali wa kuwatafuta watuhumiwa wengine wawili waliokimbia unaendelea.

Katika kudhibiti ajali za barabarani, Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linaendelea na doria katika maeneo ya mlima nyoka [barabara kuu ya Mbeya-Njombe-Iringa], mlima iwambi [barabara kuu ya Mbeya – Tunduma], mlima Igawilo [barabara kuu ya Mbeya – Tukuyu] na Kawetele [barabara kuu ya Mbeya – Chunya]. Aidha katika operesheni ya kukamata bajaji zinazokiuka sheria za usalama barabarani ndani ya Jiji la Mbeya kuanzia mwezi Julai hadi Septemba 2018 jumla ya bajaji 170 zimekamatwa, madereva 31 wamefikishwa Mahakamani na bajaji 91 zimelipa tozo sawa na Tshs.2,730,000/= na bajaji 75 bado zipo kituoni kwa hatua zaidi za kisheria na watuhumiwa 14 wapo rumandewakiendelea na mashauri yao.

Imesainiwa na:
[ULRICH O. MATEI - SACP]
KAMANDA WA POLISI MKOA WA MBEYA.
Share:

Tume Iliyoteuliwa na Waziri Mkuu Kufanya Uchunguzi Ajali ya MV Nyerere....Itaongozwa na Jenerali mstaafu, George Waitara

 
 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ametangaza tume ya kuchunguza ajali ya Kivuko cha Mv Nyerere, kilichozama Septemba 20 mwaka huu, Ukerewe jijini Mwanza na kusababisha vifo vya watu 224.

Majaliwa ameitangaza tume hiyo ya wajumbe saba itakayoongozwa na Jenerali mstaafu, George Waitara leo Jumatatu Septemba 24, katika Kijiji cha Bwisya, wilayani Ukerewe alipokwenda kushuhudia shughuli ya kunasua miili iliyobaki katika kivuko hicho.

Amesema tume hiyo itaanza kazi mara moja na itafanya kazi kwa muda wa mwezi mmoja.

Aidha, Waziri Mkuu amewataja baadhi ya wajumbe watakaokuwa katika tume hiyo ambao ni Mbunge wa Ukerewe,  Joseph Mkundi, aliyekuwa Mtendaji Mkuu wa Temesa, Mhandisi Celina Magessa na Wakili Julius kalolo ambaye atasaidia mapitio ya sheria na mfumo mzima wa uendeshaji wa vivuko.

“Lakini yumo pia Katibu Mkuu wa UWT, Queen Mlozi kwa ajili ya kusimamia stahili na kina mama, aliyekuwa Kamanda wa Polisi, Mkoa wa Kinondoni, Camillius Wambura, Bashiru Hussein kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia maafa .Wajumbe hao wanaanza kazi mara moja, waje niwape hadidu za rejea,” amesema Waziri Mkuu.
Share:

Polisi yaua Watuhumiwa Watatu Wakijaribu Kutoroka


Polisi wilayani Nkasi, mkoani Rukwa, imewaua kwa kuwapiga risasi watu watatu wakati wakijaribu kutoroka wakiwa chini ya ulinzi.

Tukio hilo lilitokea Septemba 20, mwaka huu saa 5 usiku katika Barabara ya Nkundi kuelekea Kijiji cha Kate, wilayani humo, baada ya watu hao waliokuwa wakituhumiwa kufanya mauaji ya watu sita kwa kuwakata mapanga na mashoka baada ya kuruka katika gari la polisi na kutaka kukimbia.

Akitoa taarifa ya tukio hilo mwishoni mwa wiki, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Rukwa, George Kyando, aliwataja waliouawa kwa kupigwa risasi na polisi kuwa ni Nching’wa Njige (44), Dashina Ngeseyamawe (46) ambao ni wakazi wa Kijiji cha Ntalamila pamoja na Joseph Jiuke(34) mkazi wa Kijiji cha Chonga.

Alisema watu hao walikuwa wamepakiwa kwenye gari la polisi ili waende kuonesha watuhumiwa wenzao ambao walikuwa wakitafutwa kwa kushiriki kufanya mauaji ya watu sita kwa kuwakata mapanga na shoka kutokana na imani za kishirikina.

Kamanda Kyando alisema waliokuwa wanatafutwa ni Mabula Sokoni, Said Tongela pamoja na mganga wa jadi, John Luchwela ambaye aliwapa dawa ili wasikamatwe baada ya kufanya mauaji hayo.

Wakiwa wanaelekea wanakopatikana watuhumiwa hao wengine, ndipo waliporuka katika gari la polisi ili watoroke kitendo kilichosababisha polisi kuwafyatulia risasi.

Kabla ya kuuawa kwa watuhumiwa hao waliokamatwa kufuatia msako ulioanza Julai 1 na walipohojiwa na polisi walikiri kufanya mauaji ya watu sita kwa kuwakata mapanga na mashoka.

Waliwataja  waliowaua kuwa ni Naomi Ng’wanamayunga, mkazi wa Kijiji cha Ntuchi,  Samweli Seki, mkazi wa Kijiji cha Ntalamila, Jibuta Majebele, mkazi wa Kijiji cha Mkole, Odoviko Sumuni, Salome Kisinza, wakazi wa Kijiji chalachima na Said Matenga mkazi wa Kijiji cha Mwai kwa madai kuwa ni wachawi.

Awali kabla ya kuuawa kwa kupigwa risasi na polisi, watu hao katika mahojiano walikiri pia kuwaua watu zaidi ya 15 kwa nyakati tofauti katika mikoa ya Rukwa, Katavi na Simiyu.
Share:

Rais Magufuli Apokea Taarifa Ya Utekelezaji Wa Mradi Wa Kufua Umeme Wa Stiegler”s Gorge Ikulu Jijini Dar Es Salaam

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli na viongozi waandamizi wa serikali wanaosimamia utekelezaji wa mradi wa kufua umeme katika Mto Rufiji wa Stiegler’s Gorge wakisimama kwa dakika kadhaa kuwakumbuka marehemu waliopoteza masiha kwenye ajali ya kivuko cha MV Nyerere huko Ukara wilayani Ukerewe mkoa wa Mwanza majuzi. 

Hii ilikuwa ni kabla ya kuanza kwa kikao kazi ambapo alipokea taarifa ya maendeleo ya utekelezaji wa mradi huo Ikulu jijini Dar es salaam leo Septemba 24, 2018.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiongea na viongozi waandamizi wa serikali wanaosimamia utekelezaji wa mradi wa kufua umeme katika Mto Rufiji wa Stiegler’s Gorge pamoja na wataalamu wakati wa  kikao kazi ambapo alipokea taarifa ya maendeleo ya utekelezaji wa mradi huo Ikulu jijini Dar es salaam leo Septemba 24, 2018.
Share:

Updates: Idadi ya Waliofariki Dunia Baada ya Kivuko cha MV Nyerere Yafika 86

Zoezi  la ukoaji wa miili ya watu waliopoteza maisha katika Kivuko cha MV Nyerere limeanza rasmi baada ya kusimama jana usiku, ambapo Vikosi Maalum vya uokoaji vya Jeshi la Polisi na Jeshi la Wananchi wa Watanzania (JWTZ) na Jeshi la Zimamoto na uokoaji vinaendesha zoezi hilo.

Hadi sasa idadi ya miili ya watu waliopoteza maisha katika ajali hiyo iliyotokea jana tarehe 20 Septemba 2018 imeongezeka kutoka watu 44 hadi 86.

Kivuko cha MV Nyerere kilizama katika Ziwa Victori kikitokea Bugorora kisiwani Ukerewe kuelekea Kisiwa cha Ukara.

Inahofiwa kuwa, mamia ya watu waliokuwamo katika kivuko hicho wamepoteza maisha, ambapo watu 37 walifanikiwa kuokolewa wakiwa hai hapo jana.
Mkuu wa Wilaya ya Ukerewe Cornel Maghembe amesema kuwa sababu ya kuzama kwa kivuko hicho inasadikika kuwa ilibeba watu zaidi ya 400 ambapo kilizidisha uwezo wake ambao ni watu 101.

Maghembe amesema kuwa imezama mita chache kabla ya kuwasili eneo la Ukara ambapo dereva alipunguza mwendo kuashiria amekaribia kutia nanga ndipo abiria wengi walihamia upande wa lango la kutokea wakiwahi kusogea ili washuke ndipo uzito ulizidi na kupinduka.

“Abiria walipoona mwendo umepunguzwa walikimbilia kuwahi mbele ya lango ili kujiandaa kushuka, ndipo uzito ukaegemea upande mmoja”, amesema Maghembe
Share:

wanaotembeza chakula stendi ndogo kahama wapigwa stop


Halmashauri ya Mji wa Kahama imeshauriwa kuwadhibiti watu wanaotembeza chakula katika kituo kidogo cha mabasi Majengo ili kutoa fursa ya kupata wateja, kwa Mamalishe wanaouza chakula ndani ya jengo jipya la Mamalishe lililofunguliwa hivi karibuni katika kituo hicho.

Wakizungumza kwenye kipindi cha Raha ya Leo cha KAHAMA FM, Baadhi ya Mamalishe, wamesema ni vyema serikali ikawadhibiti watu hao ili kuongeza mapato ya ndani yanayotokana na mradi wa jengo hilo.

Mamalishe hao, VICTORIA MWETA, CHRISTINA KIDUBO, na DIANA VICENTY wamesema mbali na kudhibiti wauzaji hao, wameiomba halmashauri hiyo kuziondoa baadhi ya nyumba zilizopo mbele ya jengo hilo ili wateja waweze kuliona kwa urahisi.

Naye Mwenyekiti wa Mamalishe katika jengo hilo, RAHAMA JOHN amesema tayari wamewapa taarifa viongozi wa halmashauri ili kuboresha mradi huo huku akiwataka Mamalishe kuendelea kujituma katika kazi zao kwa lengo la kujiimarisha kiuchumi.

Kwa upande wake Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya Mji wa Kahama ANDERSON MSUMBA amesema halmashauri hiyo itaendelea kuwapa mazingira bora na rafiki mama lishe wa eneo hilo ili kufanya biashara zao kwa ufanisi.

Jengo la mama lishe Majengo mjini Kahama limefunguliwa rasmi mwishoni mwa mwezi uliopita kwenye mbio za mwenge wa uhuru kitaifa likiwa na vyumba 12 vinavyotumiwa na mama lishe 24 na kwmaba limegharimu kiasi cha shilingi milioni 183.
Share:

Anthony Mavunde: Kilimo cha umwagiliaji kiwe kipaumbele kwa wakulima Halmashauri ya Mji Kahama


Halmashauri ya mji wa kahama mkoani Shinyanga imetakiwa kuwatengenezea miundombinu ya kilimo cha umwagiliaji wakulima wake badala ya kuwapatia fedha katika vikundi ili kutengeneza kilimo chenye tija.

Ushauri huo umetolewa na Naibu waziri wa kazi, vijana, ajira na ulemavu ATHONY MAVUNDE alipokuwa akizungumza na wananchi wa kata ya mwendakulima, Katika Halmashauri hiyo wakati akikagua Mradi wa kilimo cha kisasa (GREEN HOUSE) Mradi ambao umetengwa kwa ajili kilimo cha mboga mboga.

Nao baadhi ya wakulima kutoka kata ya mwendakulima wamesema wanaukosefu wa mitaji, pembejeo, masoko, maeneo na ushirikishwajiki katika sekta mbalimbali za kiuchumi hali inayosabisha kushindwa kuendelea kumudu gharama za uendeshaji wa kilimo hicho.

Naye mkurugenzi mtendaji wa Halmashuri ya mji wa Kahama, ANDERSON MSUMBA amesema wanatoa mikopo kwa vijana na wanawake kwa kila kata kwa kufuata utaratibu na kanuni ili uweze kuwanufaisha walengwa wote.

Naibu waziri MAVUNDE amendelea na ziara ya siku moja katika Halmashauri ya Ushetu ikiwa na lengo la kukagua Mradi wa kilimo hicho cha kisasa cha (GREEN HOUSE)
Share:

Serikali yapiga MARUFUKU matangazo ya uzazi wa mpango


Serikali  imesitisha matangazo yanayohamasisha uzazi wa mpango yanayorushwa kwenye runinga na redio mbalimbali nchini mpaka itakapotangazwa tena.

Sitisho hilo limetolewa katika taarifa iliyotolewa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Mpoki Ulisubisya kwenda kwa Shirika la Msaada la Marekani (USAID).

Shirika hilo ndilo linalofadhili mradi wa Tulonge Afya unaotoa matangazo hayo ya kuhamasisha uzazi wa mpango kwenye vyombo vya habari.

Barua hiyo iliyosambaa mitandaoni, inaeleza kuwa serikali inatambua mchango na juhudi za shirika hilo katika kuboresha uzazi wa mpango.

Inaeleza kuwa wizara inakusudia kufanya marejeo ya maudhui yote ya matangazo kwenye runinga na redio kwa ajili ya uzazi wa mpango.

“Hivyo unaombwa kusimamisha mara moja kutangaza na kuchapisha maudhui yoyote yale ya uzazi wa mpango kwenye vyombo vya habari mpaka itakavyoamuliwa vinginevyo,” inaeleza taarifa hiyo.

Akiwahutubia mamia ya watu Septemba 9, mjini Meatu Mkoani Simiyu, wiki mbili zilizopita, Rais John Magufuli alisema Watanzania waendelee kuzaa, lakini wachape kazi ili kukidhi mahitaji ya watoto wanaowazaa.

Alisema anafahamu Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu angependa kuongelea mambo ya uzazi wa mpango, lakini mengine yeye (Magufuli) hakubaliani nayo.

“Najua Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu, angependa kuongelea mambo ya uzazi wa mpango hapa, lakini mimi mengine huwa sikubaliani nayo sana, utapangiwaje kuzaa...kwa hiyo katika kushauriwa mengine tukubali na mengine tukatae tutumie msemo wa mzee Jakaya Kikwete ‘Ukiambiwa changanya na za kwako’ kuzaa ni muhimu,” alisema.

Katika mkutano huo Rais Magufuli aliwaeleza wananchi kuwa katika mataifa ya kigeni aliyowahi kuishi hakuwahi kusikia wimbo wa uzazi wa mpango.

“Mimi Ulaya nimekaa, nafahamu madhara ya kutokuzaa, nchi gani sijakwenda, Japan nimekaa, Uingereza nimekaa mwaka mzima, Ujerumani nimekaa, Canada nimekaa na nikachaguliwa kuwa Mwenyekiti Mwenza wa Mawaziri Ardhi Duniani, nimekaa Denmark, Norway, China nimefika sasa utanidanganya wapi,” alisema.
Share:

Waziri Mkuu: Lishe Duni Na Ulaji Usiofaa Ni Adui Wa Maendeleo Nchini

MAGONJWA yasiyoambukiza yanachangia  kwa kiasi kikubwa katika kupunguza kasi ya maendeleo yetu kwani gharama za matibabu yake ni kubwa mno, si kwa kaya zinazoathirika tu bali kwa Taifa zima.

Lishe duni pamoja na ulaji usiofaa na mitindo ya maisha vinachangia kwa kiasi kikubwa katika ongezeko la magonjwa yasiyo ya kuambukiza hususan kwa vijana na watu wazima; ambao ndiyo nguvu kazi kwa Taifa letu.

Kauli hiyo ilitolewa hivi karibuni na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa  wakati akifungua mkutano wa tano wa wadau wa masuala ya lishe,  jijini Dodoma. Alisema ni muhimu wadau hao kuweka mikakati kupunguza kasi ya ongezeko la magonjwa sugu yasiyo ya kuambukiza.

Waziri Mkuu alisema magonjwa hayo yanapaswa kudhibitiwa kwa kuzingatia ulaji unaofaa na mtindo bora wa maisha. Ni jambo lisilopingika kuwa hatua za kukabiliana na magonjwa ya kusendeka (mfano matatizo ya moyo, saratani, kisukari na shinikizo kubwa la damu), zinapaswa kuchukuliwa.

Alisisitiza dhamira ya Serikali ya Awamu ya Tano, inayoongozwa na Rais Dkt. John Magufuli ni kujenga uchumi wa viwanda ambao utatuwezesha kufikia uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025, hivyo ni muhimu suala la lishe bora likapewa kipaumbele. 

Alisema kauli mbiu ya mkutano huo “Kuelekea Uchumi wa Viwanda: Lishe Bora ni Msingi wa Kuendeleza Nguvu Kazi yenye Tija” inatoa hisia chanya ya kufikia azma hiyo kwa kuwa maendeleo ya Taifa yanategemea sana uwepo wa nguvu kazi ya kutosha na madhubuti. 

Alifafanua kuwa miongoni mwa matatizo ya lishe duni ni pamoja na upungufu mkubwa wa vitamini na madini kwa watoto walio chini ya umri wa miaka mitano (5), wanawake walio katika umri wa kuzaa na wajawazito, vijana balehe pamoja na wakina baba.

Waziri Mkuu alisema kuwa ni dhahiri kuwa tunahitaji kuanzisha viwanda vitakavyozalisha vyakula vilivyoongezwa virutubishi muhimu ili kurahisisha upatikanaji wa vyakula hivyo katika jamii zetu. 

“Nitoe wito kwa wadau wote hususan sekta binafsi kutumia fursa zilizopo na kuwekeza katika viwanda vya usindikaji wa vyakula vinavyozingatia viwango vya ubora. Niwahakikishie kuwa Serikali imeandaa mazingira mazuri ya uwekezaji, kwa hiyo, tumieni kikamilifu nafasi hiyo.” alisema Waziri Mkuu, Majaliwa

Alisema kwa pamoja, wanaweza kuimarisha mikakati yao ya kuivusha nchi na watu wake kutoka katika lindi la umaskini na kujenga nguvu kazi imara itakayoweza kuhimili changamoto za maendeleo ya viwanda. 

Waziri Mkuu anatumia fursa hiyo kutoa rai kwa wadau wote, waendelee kuiunga mkono Serikali kwa kuwekeza katika utekelezaji wa sera na mikakati mbalimbali ambayo inalenga kuboresha hali ya chakula na lishe miongoni mwa jamii, hususan kwa watoto, wanawake walio katika umri wa kuzaa, vijana balehe na watu wenye mahitaji maalum kilishe.

“Kwa msingi huo, Serikali imejumuisha masuala ya lishe katika Mpango wake Jumuishi wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano (2016/2017 – 2020/2021), kama eneo la kipaumbele katika kuboresha na kuendeleza nguvu kazi ya Taifa.”

Waziri Mkuu aliongeza kuwa “dhamira ya Serikali ni kutokomeza aina zote za utapiamlo kwa kuwekeza na kuweka mazingira wezeshi kwa wadau wote kushiriki katika kuchangia utekelezaji wa afua za lishe nchini ambazo zina matokeo ya haraka miongoni mwa makundi yote yanayoathirika.”

Alisema jitihada hizo zinalenga kutimiza azma ya Baraza la Umoja wa Mataifa la “Muongo wa Kuchukua Hatua katika Masuala ya Lishe – Decade of Action on Nutrition” ya mwaka 2016 hadi 2025 na pia kuwezesha kufikiwa kwa Malengo yote 17 ya Umoja wa Mataifa ya Maendeleo Endelevu (United Nations Sustainable Development Goals). 

Alibainisha kuwa Serikali inaendelea kutilia mkazo suala la uhamasishaji miongoni mwa watunga sera na viongozi katika ngazi mbalimbali kuhusu masuala yote yanayohusiana na lishe kwa lengo la kuwa na uelewa wa pamoja kuhusu masuala hayo. 

Alisema juhudi hizo zinaenda sambamba na utoaji wa elimu sahihi ya lishe kwa umma kwani tunaamini kuwa Watanzania wakielimishwa vizuri kuhusu masuala haya itachangia kuleta mabadiliko chanya katika jamii pamoja na taasisi zetu kwa ujumla. 

Alisema Serikali imeendelea kuongeza rasilimali kila mwaka kwa ajili ya kutekeleza masuala ya lishe hususan katika ngazi za mikoa na halmashauri, ambapo takwimu zinaonesha kuwepo kwa ongezeko kutoka wastani wa sh. milioni 65 mwaka 2011/2012 hadi kufikia sh. milioni 219 mwaka 2016/2017. 

Kwa mwaka 2017/2018 Serikali ilikadiria kutumia jumla ya sh. billioni 11 katika utekelezaji wa masuala ya lishe katika ngazi ya halmashauri, hivyo hadi kufikia robo ya tatu ya mwaka 2017/2018, kiasi cha sh. bilioni mbili zilitolewa na kutumika. 

Kadhalika, Waziri Mkuu aliendelea kuhimiza kuhusu suala la kutenga kiasi cha shilingi 1,000 kwa idadi ya watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano katika Halmashauri zetu kupitia mapato ya ndani ili ziweze kutumika katika kutekeleza Afua hizo kwenye Halmashauri husika. 

Aliwahakikishia wadau hao kuwa, Serikali itaendelea kutenga fedha kwa ajili ya kugharamia utekelezaji wa Afua za Lishe kama zilivyoainishwa katika Mpango wa Taifa wa Utekelezaji wa Masuala ya Lishe 2016/2017 – 2020/2021; kwa kadiri hali itakavyoruhusu.

“Nitoe rai kwa Watendaji Wakuu wote katika Wizara husika, Idara, Wakala na Taasisi za Serikali, wadau wa maendeleo, asasi za kijamii; kila mmoja kwa nafasi yake au mamlaka yake, kuendelea kutenga fedha kwa ajili ya utekelezaji wa Mpango wa Taifa wa Utekelezaji wa Masuala ya Lishe.” 

Alisema mikoa na halmashauri zihakikishe kuwa afua zilizoainishwa katika mpango huo zinajumuishwa katika mipango na bajeti zao za kila mwaka, sambamba na kutoa fedha zilizopangwa kwa ajili ya utekelezaji. 

Waziri Mkuu alisisitiza tena kuwa kila mdau anayeshiriki katika utekelezaji wa shughuli za lishe nchini aoneshe bayana mchango wake katika kukabiliana na utapiamlo nchini ili Taifa liweze kufikia malengo tuliyojiwekea.

Alisema ili wahakikishe hatua tunazochokua katika mapambano dhidi ya utapiamlo zinaleta matokeo kama walivyopanga na zinawanufaisha au zinawafikia walengwa, aliwaagiza  viongozi wa Serikali katika ngazi mbalimbali kutambua wajibu wao na kushiriki kikamilifu katika kudhibiti na kukabiliana na athari za utapiamlo katika maeneo yao.

Pia, Waziri Mkuu aliwataka viongozi hao wa Serikali katika ngazi za mbalimbali wafanye tathmini ya ufanisi wa hatua wanazochukua na watoe taarifa za ufanisi au changamoto mara kwa mara. 

Kwa upande wake,Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu, Jenista Mhagama  alisema ushirikishwaji wa wadau kwenye masuala ya lishe umeongezeka na wanashuhudia wadau wengi wa maendeleo wakionesha nia na wengine kuwekeza katika masuala ya lishe nchini.

 Aidha, Waziri Jenista alisema wameweza kuratibu wa uanzishwaji wa mabaraza mbalimbali yanayojadili masuala ya lishe likiwemo baraza la sekta binafsi ambao wana mchango mkubwa katika kuhakikisha azma ya Serikali ya kutokomeza utapiamlo inafikiwa. 

Alisema hatua hizo kwa kiasi kikubwa zimechangia kupunguza viwango vya utapiamlo pamoja na idadi ya vifo kwa watoto wenye umri chini ya miaka mitano. “Mfano mzuri ni pale tulipopunguza udumavu kutoka asilimia 42 mwaka 2010 hadi asilimia 34.4 mwaka 2016.”

Alisema Taifa linahitaji nguvu kazi imara itakayohimili ushindani katika soko la ajira na kuendeleza Tanzania ya Viwanda. Nguvu kazi hiyo inaanza kujengwa kwa kuimarisha lishe bora hususan kuanzia pale mama anapokuwa mjamzito hadi mtoto anapofika miaka miwili. 

Awali,Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, alisema viwango vya matatizo ya lishe vimepungua kwa baadhi ya viashiria ingawa si kwa kiasi cha kuridhisha.

Alitaja moja ya viashiria vya kupungua kwa matatizo ya lishe ni kushuka kwa tatizo la udumavu, ambapo kwa sasa kuna wastani wa watoto watatu wenye udumavu kati ya watoto 10 walio katika umri chini ya miaka mitano.

Waziri Ummy alisema kuwa udumavu huathiri ukuaji wa mtoto kimwili na kiakili, hivyo kupunguza uwezo wa kufanya vizuri shuleni na kupunguza ufanisi wake katika maisha yake ya utu uzima.

Alitaja mikoa ambayo imeathiriwa zaidi na tatizo hilo la lishe ni pamoja na Rukwa, Njombe, Ruvuma, Iringa, Kagera, Mwanza na Geita, ambayo ina wastani wa zaidi ya asilimia 40. Mikoa hiyo ni kati ya mikoa yenye uzalishaji mkubwa wa chakula nchini.

“Ni dhahiri kuwa, utatuzi wa suala hili unahitaji mbinu na hatua za haraka pamoja na ushirikiano wa kila mmoja wetu. Kulingana na takwimu za kidemografia na afya ya mwaka 2015/2016, watoto 106,000 wana utapiamlo mkali ukilinganisha na watoto 340,000 wenye utapiamlo wa kadiri.”

Alisema idadi hiyo inaashiria kuwa watoto hao wenye utapiamlo mkali wapo kwenye hatari kubwa ya kupoteza maisha, ambapo hadi sasa changamoto kubwa waliyonayo ipo katika utambuzi wa tatizo, utoaji wa rufaa, upatikanaji wa chakula dawa na utoaji wa matibabu sahihi kwa watoto wenye tatizo hilo.

Kadhalika, Waziri Ummy alisema bado kuna hospitali chache zenye uwezo wa kutoa huduma ya matibabu ya utapiamlo mkali. Juhudi zinaendelea kuhakikisha hospitali zote nchini zinajengewa uwezo wa kutoa huduma hizo muhimu ili kuokoa maisha ya watoto walioathirika na utapiamlo mkali.

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU
Share:

IDADI YA WASOMAJI

TUSIKILIZE LIVE KUPITIA TUNEIN

UNGANA NASI FACEBOOK HAPA

10 ZILIZOSOMWA ZAIDI

Labels

Blog Archive