Aliyekuwa Akitapeli Watu Kwa Kutumia Majina Ya Jakaya Kikwete, Salma Kikwete, Ridhiwan Viccoba Afikishwa Mahakamani

 
Mfanyabiashara, Masse Uledi (41), amekiri kumiliki simu tisa na laini nane zilizotumika kujipatia pesa kwa udanganyifu Sh. milioni 3.6 kama dhamana ya mkopo kutoka Focus Vikoba-na kutumia majina ya Rais mstaafu Jakaya Kikwete, Salma Kikwete, Mwenyekiti wa IPP, Reginald Mengi na Mchungaji Getruda Rwakatare.

Uledi alikiri madai hayo jana aliposomewa maelezo ya awali katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam.Maelezo hayo yalisomwa mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba.

Wakili wa Serikali Mwandamizi, Patrick Mwita, alidai 2017, mshtakiwa alifungua kurasa katika mtandao wa kijamii wa Facebook kwa majina manne tofauti akidanganya yanatoa mkopo kupitia Focus Vikoba.

Ilidaiwa katika kurasa hizo mshtakiwa alitangaza wanaohitaji mkopo kupitia taasisi hiyo, wawasiliane kwa namba za simu, 0759142712, 0714230840 na 0657076983 ili kupata mkopo.

Ilidaiwa kuwa Joyce Chitumbi alipiga simu kuomba mkopo wa Sh. milioni 10, na Septemba 9, 2017, alitakiwa kutoa Sh. 840,000 kama dhamana ya mkopo huo.

Upande wa Jamhuri uliendelea kudai kuwa Daniel Dangi alitoa dhamana ya Sh. 600,000 na Sh. 200,000 kwa nyakati mbili tofauti kama dhamana ya mkopo wa Sh. milioni mbili.

Mwingine anayedaiwa kutapeliwa ni Lucas Kiula, ambaye alitoa ya Sh. 2,160,000 kama dhamana ya mkopo wa Sh. milioni 10, baada ya kudanganya taasisi hiyo iko chini ya Mchungaji Rwakatare wakati akijua si kweli.

Jamhuri ilidai mshtakiwa baada ya kujipatia fedha hizo alizima simu na namba nyingine alipopigiwa hakupokea.

Taarifa zilifikishwa Kituo Kikuu cha Polisi, Kanda Maalum ya Dar es Salaam na walifanya uchunguzi wa kimtandao na kubaini mshtakiwa anaishi Kitunda.

Ilidaiwa baada ya uchunguzi, Polisi walifanikiwa kufika nyumbani kwake na baada ya upekuzi walifanikiwa kumkamata na simu za mkononi nane na laini za simu tisa zilizotumika kwenye kurasa za facebook kwa majina ya Rais Kikwete, Mama Salma, Mengi na Mchungaji Rwakatare.

Mshtakiwa aliposomewa maelezo ya awali, alikiri majina na anuani yake, alikiri kumiliki simu na laini hizo kwamba ni mali ya marehemu mumewe.

Katika kesi ya msingi ilidaiwa kati ya Septemba 28 na Novemba, 2017 mshtakiwa alijipatia Sh. 3,600,000 kama dhamana ya kutoa mkopo wa jumla ya Sh. milioni 22 kutoka kwa watu tofauti huku akijua si kweli.

Awali, aliposomewa mashtaka hayo alikana na yuko nje kwa dhamana. Kesi itaendelea kwa kusikilizwa ushahidi wa Jamhuri Oktoba 11, mwaka huu.
Share:

No comments:

Post a Comment

IDADI YA WASOMAJI

TUSIKILIZE LIVE KUPITIA TUNEIN

UNGANA NASI FACEBOOK HAPA

10 ZILIZOSOMWA ZAIDI

Labels

Blog Archive