Serikali imezitaka Benki zote zinazotoa mikopo ya kilimo Tanzania Bara na Zanzibar kuhakikisha zinatoa mikopo kwa kuzingatia vigezo vya ukopeshaji vikiwemo kuangalia historia ya mkopaji ili kuondoa mikopo Chechefu (NPL).
Hayo yameelezwa Bungeni jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji, alipokuwa akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Bububu Mhe. Mwantakaje Haji Juma, aliyetaka kujua utaratibu unaotumika kutoa mikopo kwa wakulima wa Zanzibar kupitia Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB).
Dkt. Kijaji alieleza kuwa kabla ya kutoa mkopo ni lazima Benki ijiridhishe na aina ya mradi wa mkopaji ikiwa utaleta faida itakayomuwezesha mkopaji kurejesha mkopo huo kwa wakati ili kuzuia ukuaji wa Mikopo Chechefu.
Akijibu swali la msingi la Mbunge huyo aliyetaka kujua ni wananchi wangapi wanaonufaika na mikopo ya Kilimo kwa upande wa Zanzibar, Dkt. Kijaji alisema kuwa jumla ya wananchi 3,000 wamenufaika na mikopo ya Benki ya TADB hadi kufikia Julai 31, 2018.
“Kati ya wanufaika hao 3000, idadi ya wanaume walionufaika ni 1800, wanawake 900 na vijana wa kike na kiume ni 300”, alieleza Dkt. Kijaji.
Alisema kuwa jumla ya mikopo ya shillingi bilioni 6.50, imetolewa kwa wananchi hao wa Zanzibar hadi kufikia Julai 31, 2018.
Imetolewa na;
Kitengo cha Mawasiliano Serikalini
Wizara ya Fedha na Mipango.
No comments:
Post a Comment