HALMASHAURI YA MJI WA KAHAMA IKO MBIONI KUPOKEA TAKRIBANI MIL. 80 KWA AJILI YA KUKAMILISHA UJENZI WA ZAHANATI YA NYASUBI


Na Ndalike Sonda
KAHAMA.

Halmashauri ya Mji wa KAHAMA Mkoani SHINYANGA inatarajia kupokea takribani shilingi milioni 80 kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa zahanati ya NYASUBI ikiwa ni mikakati ya kupunguza msongamano wa wagonjwa katika hospitali ya halmashauri hiyo.

Akizungumza na KAHAMA FM, Kaimu Mganga Mkuu wa Halmashauri hiyo, Dk. LUCAS DAVID amesema fedha hizo zinatolewa na serikali katika mwaka huu wa fedha 2017/2018.

Amesema itakapokamilika zahanati hiyo itasaidia kuwapunguzia wagonjwa wanaotoka eneo hilo, umbali mrefu wa kufuata huduma za afya sanjari na mpango wa kuboresha sekta ya afya katika kata mbalimbali za Halmashauri hiyo.

Wakizungumzia hatua hiyo, wakazi wa mjini Kahama, SOLOMON JUMA na SEBASTIANI MASHINJI, wameshauri Halmashauri hiyo kujenga zahanati na vituo vya afya katika kila kata ili kupunguza msongamano wa wagonjwa kwenye hospitali ya mji wa Kahama.

Naye Mwenyekiti wa Halmashauri ya mji wa Kahama, ABEL SHIJA amewataka wananchi kuwa na subira kwani kwa sasa halmashauri hiyo inaendelea kuboresha ujenzi wa vituo vya afya katika kata zilizopo pembezoni mwa halmashauri hiyo.

Hospitali ya Halmashauri ya Mji wa Kahama, inakadiriwa kuhudumia wagonjwa wasiopungua 1000 kwa siku hali inayosababisha msongamano mkubwa wa wagonjwa katika hospitalii hiyo.
Share:

SERIKALI WILAYANI KAHAMA YAWATAKA WANANCHI WAISHIO PEMBEZONI MWA MAENEO YA MACHIMBO YA DHAHABU KURIPOTI MATUKIO YA UVUNJIFU WA AMANI


Na Ndalike Sonda
KAHAMA.

Serikali wilayani KAHAMA imewataka wananchi waishio katika maeneo ya machimbo madogo ya madini kutoa taarifa kwa vyombo vya ulinzi na usalama matukio yote yanayoashiria uvunjifu wa amani katika maeneo yao.

Akizungumza leo kwenye uzinduzi wa kampeni ya utunzaji wa mazingira na upandaji wa miti katika machimbo madogo ya dhahabu ya Kabela Ilindi, Mkuu wa Wilaya ya Kahama, FADHILI NKURLU amesema kila mchimbaji wa madini anawajibu wa kulinda usalama.

Amesema kutokana na wingi wa watu machimboni, ulinzi hauna budi kuimarishwa sanjari na utunzaji wa mazingira kwa ili kudumisha amani na kuzuia magonjwa ya mlipuko huku akiupongeza uongozi wa Machimbo hayo kwa utunzaji wa mazingira na usalama.

Akizungumza kwa niaba ya Wachimbaji wenzake, SHADRACK NYAMHOKYA amesema wavamimizi wa machimbo wamekuwa wakileta hofu kwa wachimbaji hao na kuiomba serikali kadhibiti hali hiyo ikiwa ni pamoja na kuboresha barabara ya kutoka Kahama kwenda katika machimbo hayo.

Katika zoezi hilo la utunzaji wa mazingira na upandaji wa miti jumla ya miche 500 imepandwa, huku akiahidi kupeleka miche mingine elfu 10 katika machimbo hayo ya dhahabu ya Kabela Ilindi.
Share:

AFIKISHWA MAHAKAMANI KWA TUHUMA YA UBAKAJI



Na Daniel Magwina
KAHAMA.

Mkazi wa Mtaa wa Majengo Wilayani KAHAMA Mkoani SHINYANGA, MORGAN SWEBE (32) amefikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya KAHAMA kwa tuhuma ya kumbaka mwanafunzi wa miaka 16 na kumsababishia ujauzito kinyume cha sheria.

Mbele ya Hakimu Mkazi wa Mahakama hiyo KENETH MUTEMBEI, mwendesha mashitaka wa Polisi MASAU MASATU amesema SWEBE kwa nyakati tofauti mwezi Agosti na Septemba 2017 katika mtaa wa Majengo Mjini KAHAMA, alimbaka mwanafunzi huyo na kumsababishia ujauzito.

MASATU amefafanua kuwa SWEBE ametenda kosa hilo kinyume na kifungu namba 130 na 131 cha kanuni ya adhabu sura ya 16 marejeo ya mwaka 2002, Na kifungu cha sheria ya Elimu namba 60 A sura ya 353 kama ilivofanyiwa marekebisho na sheria namba 2 ya mwaka 2016.

Katika shauri hilo la jinai namba 133/2018 SWEBE amekana kutenda tuhuma ya kwanza ya kubaka na kukiri tuhuma ya pili ya kumpa ujauzito mwanafunzi huyo.

Upelelezi wa shauri hilo haujakamilika na mshitakiwa amerudishwa rumande kwa kukosa dhamana na shauri hlo kutajwa tena April 6 mwaka huu.
Share:

ACACIA YAKABIDHI VIFAA VYA UJENZI KWA HALMASHAURI ZA KAHAMA MJI NA MSALALA

Na Amina Mbwambo
KAHAMA.

Kampuni ya ACACIA kupitia migodi yake ya dhahabu ya BULYANHULU na BUZWAGI Wilayani KAHAMA imekabidhi vifaa mbalimbali vya ujenzi kwa Halmashauri za KAHAMA Mji na MSALALA Wilayani KAHAMA, vyenye thamani ya shilingi milioni 150.

Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo, Meneja Mkuu wa migodi hiyo, BENEDICT BUSUNZU amesema wamefikia hatua hiyo baada ya kuguswa na tatizo la uhaba mkubwa wa vyumba vya madarasa katika Halmashauri hizo zinazoizunguka migodi.

BUSUNZU amesema leo wamekabidhi mifuko ya saruji 3200 yenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 80 na kwamba vifaa vingine vya ujenzi vitakabidhiwa kwa Halmashauri husika kwa nyakati tofauti kulingana na hatua za ujenzi wa madarasa ili kuinua kiwango cha elimu.

Akipokea msaada huo, mkuu wa wilaya ya KAHAMA, FADHILI NKURLU amesema Halmashauri hizo mbili kwa pamoja zina uhitaji wa vyumba vya madarasa zaidi ya 1500 hivyo msaada huo utasaidia kupunguza tatizo la uhaba huo.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Kahama Mji ANDERSON MSUMBA na Kaimu mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya Msalala, MARY NZUKI wameishukuru kampuni ya Acacia kwa msaada huo.

Kampuni ya Acacia kupitia migodi ya dhahabu ya Buzwagi na Bulyanhulu imedhamiria kujenga vyumba vya madarasa zaidi ya 1575 katika awamu hii, kwenye shule za msingi 84 na za sekondari 30 katika Halmashauri hizo za Msalala na Kahama Mji.
Share:

WAWILI WAFIKISHWA MAHAKANI KWA TUHUMA YA KUKUTWA NA DAWA ZA KULEVYA

Na Liluian Katabaro
KAHAMA.

Wakazi wawili wa mtaa wa Mwime Wilayani KAHAMA Mkoani SHINYANGA, GODFEY JACOB (23) na KAVULA JACOB (21) amefikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya KAHAMA kwa tuhuma ya kupatikana na dawa za kulevya aina ya bangi kinyume cha sheria.

Mbele ya Hakimu Mkazi wa Mahakama hiyo IMANI BATENZI, mwendesha mashitaka wa Polisi SAADA ADAM amesema watuhumiwa walikamatwa March 24 mwaka huu majira ya saa nane mchana huko mtaa wa Mwime wakiwa na bangi hiyo gram 35.

SAADA amesema washitakiwa wametenda kosa hilo kinyume na kifungu namba 17 na kifungu namba 2 cha sheria ya kuzuia na kupambana na dawa za kulevya sura ya 5 marejeo ya mwaka 2015.

Katika shauri hilo la jinai namba 135/2018 washitakiwa wamekana kutenda kosa hilo na wamerudishwa rumande kwa kukosa dhamana hadi Aprili 11 mwaka huu shauri hilo litakapotajwa tena mahakamani hapo.
Share:

AFIKISHWA MAHAKAMANI KWA TUHUMA YA KUZINI



Na Daniel Magwina
KAHAMA.

Mkazi wa kijiji cha Sangilwa Wilayani KAHAMA Mkoani SHINYANGA, JUMANNE KUSINZA (35) amefikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya KAHAMA kwa tuhuma ya kuzini maharamu kinyume cha sheria.

Mbele ya Hakimu Mkazi wa Mahakama hiyo IMANI BATENZI, mwendesha mashitaka SAADA ADAM amesema KUSINZA kwa nyakati tofauti mwezi Agost na Septemba mwaka jana huko Sangilwa, alimbaka mtoto wake wa kumzaa mwenye umri wa miaka 8 mwanafunzi wa darasa la kwanza.

SAADA amefafanua kuwa KUSINZA ametenda kosa hilo kinyume na kifungu namba 158 cha kanuni ya adhabu sura ya 16 marejeo ya mwaka 2002.

Katika shauri hilo la jinai namba 131/2018, KUSINZA amekana kutenda kosa hilo na upelelezi wa shauri hilo haujakamilika na mshitakiwa amerudishwa rumande kwa kukosa dhamana hadi Aprili 5 mwaka huu shauri hilo litakapotajwa tena.
Share:

MADEREVA BAJAJI WAILALAMIKIA HALMASHAURI YA MJI WA KAHAMA KWA KUSHINDWA KUREKEBISHA BAADHI YA BARABARA AMBAZO NI MBOVU


Na Ndalike Sonda
KAHAMA.

Baadhi ya madereva wa magari na waendesha pikipiki za magurudumu matatu, (BAJAJI) Mjini KAHAMA wameilalamikia Halmashauri ya Mji wa KAHAMA kwa kushindwa kuyakarabati makaravati mbalimbali yaliyopo katika barabara licha ya kuwa yamevunjika muda mrefu.

Madereva hao, YUSUPH SAID, JOHN ROBERT na RAMADHAN NKANDI, wamesema wamekuwa wakipata usumbufu wakati wa kutumia barabara ambazo makaravati yake yamevunjika ikiwamo barabara ya kutoka lilipokwa soko la wakulima kwenda Standi ndogo ya mabasi iliyopo Majengo mjini humo.

Naye Katibu wa madereva wa magari madogo ya abiria yanayosafirisha abiria kati ya Kahama na Shinyanga, JUMANNE SONGORO amesema kutokana na ubovu wa makaravati mawili yaliyopo katika barabara ya kutoka Isaka kwenda Standi ndogo ya majengo ajali mbalimbali zimekuwa zikitokea.

Meneja wa wakala wa barabara za mjini na vijijni TARURA halmashauri ya Mji wa Kahama, Mhandisi JOB MUTAGWABA amekiri kuwepo kwa changamoto hiyo ambapo amesema katika bajeti ya mwaka 2017/2018 zaidi ya shilingi milioni 60 zimetengwa kuboresha makaravati yote ya mjini Kahama.
Share:

WATANO WAHUKUMIWA KWENDA JELA AU KULIPA FAINI KWA KOSA LA KUWEPO NCHINI KINYUME CHA SHERIA



Na Paulina Juma
KAHAMA.

Raia watatu wa nchini RWANDA wamehukumiwa kwenda jela miezi sita au kulipa faini ya shilingi laki tano kila mmoja kwa kosa la kuingia na kuwepo nchini kinyume cha sheria.

Akitoa Hukumu hiyo Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Wilaya ya KAHAMA, KENNETH MTEMBEI amesema ametoa hukumu hiyo baada ya watuhumiwa kukiri kutenda kosa hilo, hivyo watatumikia adhabu hiyo na baada ya hapo watarudishwa kwao Rwanda.

Waliohukumiwa ni pamoja na NIYONZIMA CLAUDE (25), NIYONZIMA TIERI (25) na ALEX CHOYITUNGE (24).

Awali muendesha mashitaka wa Idara ya Uhamiaji SALUM RASHID amesema wote kwa pamoja walikamatwa March 15, mwaka huu huko WENDELE wilayani Kahama wakiwa ndani ya basi la SELECT EXPRESS wakiwa wameingia nichini Tanzania bila vibali vyovyote vinavyowaruhusu.

Katika shauri hilo namba 119 la mwaka huu SALUM amesema wametenda kosa hilo kinyume na kifungu namba 45 cha sheria ya uhamiaji namba 7 ya mwaka 1995 marejeo ya mwaka 2016.

Wote kwa pamoja wameshindwa kulipa faini na wameanza kutumikia kifungo cha miezi sita jela wakimaliza watarejeshwa nchini kwao RWANDA.
Share:

KIASI CHA SHILINGI MILIONI 54 KIMEGAWIWA SHULE ZA MSINGI HALMASHAURI YA MJI WA KAHAMA


Na Ndalike  Sonda
KAHAMA.

Jumla ya shilingi milioni 54 zimegawiwa katika shule za msingi 36 kati ya 72 za Halmashauri ya Mji wa KAHAMA kwa lengo la kuziwezesha kuendesha miradi mbalimbali ya kujitegemea shuleni.

Akizungumza na KAHAMA FM, Kaimu Afisa Elimu wa Halmashauri ya Mji wa KAHAMA, PEREPETUA MAYIGE, amesema fedha hizo zimetolewa na Mpango wa kuboresha elimu Tanzania (EQUEP Tanzania) ambapo kila shule imepata shilingi milioni 1.5.

MAYIGE amesema lengo la mpango huo ni kuhakikisha kila shule ina kuwa na miradi ya kujitegenea ambayo itasaidia upatikanaji wa chakula cha wanafunzi shuleni na hivyo kuongeza kiwango cha ufaulu katika halmashauri hiyo.

MAYIGE amesema ukosefu wa chakula cha wanafunzi shuleni ni changamoto ambayo inasababisha baadhi ya wanafunzi kushindwa kumudu masomo na kwamba jamii inapaswa kushirikiana na shule ili kuatatua changamoto hiyo.

Halmashauri ya mji wa Kahama inajumla ya shule za msingi 72 za serikali zenye wanafunzi zaidi ya 68 elfu.
Share:

BEI YA NYANYA YAPANDA MASOKO YA HALMASHAURI YA MJI WA KAHAMA


Na Sebastian Mnakaya
KAHAMA.

Upatikanaji wa nyanya umekuwa mgumu katika Halmashauri ya Mji wa KAHAMA na kusababisha kupanda kwa bei ya biadhaa hiyo kutoka shilling Elfu kumi na tano hadi elfu ishirini na mbili kwa ndoo kubwa.

Kwa mujibu wa ufuatiliaji uliofanywa na KAHAMA FM katika masoko mbalimbali ya Halmashauri ya Mji wa KAHAMA, hali inawafanya Wafanyabiashara wa rejareja kupandisha bei kwa watumiaji wa bidhaa hiyo.

Wakizungumza na KAHAMA FM kwa nyakati tofauti wafanyabiashara wa soko kuu mjini Kahama wamesema kutokana na uhaba wa nyanya katika mikoa mingine nchini, wafanyabiashara wa nyanya wa mikoa hiyo wanakuja kununua bidhaa hiyo kwa wakulima wa Kahama.

Kwa upande wao wanunuzi na watumiaji wa nyanya waliozungumza na Kahama FM wamewaomba wafanyabiashara kupunguza kidogo bei hiyo ya nyanya kutokana na hali ilivyo ngumu.

Kutokana na upungufu huo wa nyanya, sado moja iliyokuwa ikiuzwa shilingi elfu tatu sasa inauzwa shilingi elfu nane wakati ndoo kubwa ambayo ilikuwa ikiuzwa shilingi elfu kumi na mbili sasa inauzwa shilingi elfu ishirini na mbili.

Aidha ufuatiliaji uliofanywa na Kahama FM umebaini kuwa bei ya sado moja la nyanya katika masoko mbalimbali nchini ni kati ya shilingi elfu saba hadi elfu kumi ikiwa ongezeko la takribani shilingi elfu tatu huku kasha kubwa la nyanya likiuzwa shilling elfu sabini hadi laki moja.
Share:

WANANCHI WA NYIHOGO KAHAMA WAANZA UJENZI WA SHULE YAO YA MSINGI


Na Ndalike Sonda
KAHAMA.

WANANCHI wa Mtaa wa Mayila Kata ya NYIHOGO katika Halmashauri ya Mji wa KAHAMA wameanza ujenzi wa shule yao ya msingi ili kuwaondolea watoto wao adha inayowakabili sasa ya kutembea umbali mrefu kwenda shule za msingi Kilima na Mhungula.

Wakazi wa Mtaa huo, AGNETHA JUVINUS na JOEL MWENDAPOLE wamesema kukamilika kwa shule hiyo kutapunguza ajali na vifo vya wanafunzi wakati wa kuvuka barabara kuu ya Isaka - Ushirombo ambapo vifo 17 vimeshatokea tangu kukamilika kwa barabara hiyo mwaka 2014.

Nao baadhi ya wanafunzi wanaoishi mtaa huo, pamoja na kufurahia ujenzi wa shule hiyo, wameiomba serikali kuharakisha ujenzi huo na pamoja na kuifungua kwaajili ya kusajili wanafunzi.

Kwa mujibu wa Diwani wa Kata ya Nyihogo, SHADRACK MGWAMI shule hiyo itakuwa imekamilika na kuanza kutumika ifikapo mwaka 2020 na amewataka Wananchi kuendelea kujitolea kwa hali na mali kukamilisha ujenzi huo.

Mwenyekiti wa Ujenzi huo, SOLOMON JUMA ukubwa wa ekari 8 limetengwa kwa ajili ya ujenzi wa shule hiyo ambapo wananchi wamekwisha kusomba mawe huku wadau mbalimbali wakiahidi kuchangia vifaa vya ujenzi.
Share:

AHUKUMIWA KWENDA JELA AU KULIPA FAINI KWA KOSA LA KUINGIA NCHINI KINYUME NA SHERIA



Na Paulina Juma
KAHAMA.

Raia wa Burundi, EDSON AJUAE (19) jana amehukumiwa kwenda jela mwaka 1 au kulipa faini ya shilingi 500,000 kwa kosa la kuwepo nchini kinyume na sheria ya Uhamiaji.

Akitoa hukumu hiyo leo, Hakimu Mkazi wa Mahakama ya wilaya ya Kahama, IMANI BATENZI amesema ametoa hukumu hiyo baada ya AJUAE kukiri kutenda kosa hilo mahakamani hapo.

Awali, Mwendesha Mashitaka wa Idara ya Uhamiaji, SALUMU RASHID amesema AJUAE alikamatwa March 13 mwaka huu majira ya saa 3 asubuhi maeneo ya Line Police mjini Kahama akiwa hana kibali chochote cha kuwepo nchini.

Katika shauri hilo la jinai namba 110/2018, AJUAE ametenda kosa kinyume na kifungu namba 45 cha sheria ya Uhamiaji namba 7 ya mwaka 1995 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2016.

AJUAE ameshindwa kulipa faini na ameanza kutumikia kifungo hicho leo na mara baada ya kumaliza kifungo hicho atarejeshwa nchini kwao BURUNDI.
Share:

WADAU WA ELIMU WILAYANI KAHAMA WATAKIWA KUUNGANA KUTOKOMEZA MIMBA ZA UTOTONI.


Na Salvatory Ntandu
KAHAMA.

Wadau mbalimbali wa sekta ya elimu Wilayani KAHAMA Mkoani SHINYANGA wametakiwa kuunganisha nguvu zao katika kupiga vita ndoa na mimba za utotoni kwa wanafunzi sanjari na kuwafichua watu wanaotekeleza vitendo hivyo kwenye jamii.

Kauli hiyo imetolewa Mjini KAHAMA jana na Mratibu wa Mradi wa uboreshaji wa lishe na afya ya uzazi kwa mama na mtoto (ENRICH) MWALLA MACHIBWA kutoka shirika la World Vision kwenye hafla ya kukabidhi msaada wa vifaa vya kutathimini hali ya lishe mkoani Shinyanga.

MACHIBYA amesema World Vision imeanzisha kampeni hiyo yenye lengo la kutomeza tatizo la mimba kwa wanafunzi na ndoa za utotoni kwa kutoa elimu kwa jamii kuhusu madhara yake.

Kwa upande wake, Mkuu wa wilaya ya Kahama FADHILI NKURLU ambaye alikuwa ni Mgeni Rasmi katika Makabidhiano ya vifaa hivyo vyenye thamani ya zaidii shilingi milioni 100 amesema hatua kali zitachukuliwa kwa watakaobainika kuwapa mimba wanafunzi.

Mkoa wa Shinyanga ni miongoni mwa mikoa inayoongoza kwa tatizo la ndoa na mimba miongoni mwa Wanafunzi hapa nchini.
Share:

SHIDEFA KUPIMA WATU LAKI MOJA WENYE UGONJWA WA KIFUA HALMASHAURI YA MJI WA KAHAMA PAMOJA NA MSALALA.


Na Salvatory Ntandu
KAHAMA.

Katika kuadhimisha Siku ya Kifua Kikuu Duniani Machi 24 mwaka huu, Shirika lisilo la kiserikali la SHIDEFA + linatarajia kupima watu laki moja katika Halmashauri za Mji KAHAMA na MSALALA ifikapo Septemba mwaka huu.

Hayo yamebainishwa leo na Mkurugenzi wa Shirika hilo, VENNANCE MZUKA wakati akizungumza na Waandishi wa Habari mjini Kahama kuhusi utekeleza wa zoezi hilo.

Amesema Utafiti uliofanywa na Shirika hilo umebaini kuwepo kwa dalili za awali za watu wenye viashiria vya ugonjwa huo hususani wanaofanya kazi kwenye migodi midogo na kwenye mikusanyiko ya watu.

Mbali na hilo MZUKA ametoa rai kwa wananchi kuacha dhana potofu kuwa mtu anapopata ugonjwa wa kifua kuku ni kuwa amerogwa jambo ambalo silo la kweli na badala yake waende hospitali kupata tiba.

Shirika la SHEDAFA + litaadhimisha siku hiyo katika mji mdogo wa Isaka, Halmashauri ya Msalala kwa kutoa elimu na huduma ya upimaji bure.
Share:

HALMASHAURI YA MJI WA KAHAMA YAANZA KUTOA HUDUMA YA UPIMAJI ARDHI SHIRIKISHI KWA WANANCHI.


Na Ndalike Sonda
KAHAMA.

Halmashauri ya Mji wa KAHAMA Mkoani SHINYANGA imeanza kutoa huduma ya upimaji wa ardhi shirikishi kwa wananchi, kwa lengo la kuondoa migogoro ya ardhi inayotokana na wananchi kuuza au kununua maeneo yenye migogoro.

Akizungumza baada ya kutatua mgogoro wa ardhi katika Mtaa wa Bukondamoyo, kutokana na mwananchi mmoja kujenga ndani ya hifadhi ya barabara, Afisa mipango wa halmashauri hiyo IRENE MARO amesema kwa sasa wanatoa elimu juu ya taratibu za ununuzi wa ardhi.

Wakizungumzia mgogoro wa ardhi uliopo baina ya mwananchi na serikali ya mtaa wa Bukondamoyo, ODILIA KAJORO na JOHN MAGANGA wameishauri serikali kuwasimamia maafisa ardhi ili wajenge desturi ya kuwashirikisha wananchi kwenye masuala ya mipango miji.

Naye Mwenyekiti wa Mtaa wa Bukondamoyo, NASHON YOHANA amesema serikali ya mtaa huo, idara ya ardhi na muuzaji wa eneo lililo na mgogoro wanaangalia namna ya kumfidia mwananchi aliyeuziwa na kujenga kwenye eneo la umma.
Share:

WAFANYABIASHARA WA VYAKULA MJINI KAHAMA WATAKIWA KUHIFADHI VYAKULA HIVYO KATIKA MAZINGIRA SALAMA.


Na Sebastian Mnakaya
KAHAMA.

Wafanyabiashara wa vinywaji na vyakula vya kufungashwa Mjini KAHAMA wametakiwa kuhifadhi bidhaa hizo kwenye mazingira safi na yasiyo na jua ili visiharibike na kuwaletea madhara watumiaji.

Mratibu wa Mamlaka ya Chakula na Dawa(TFDA) wilayani KAHAMA, KARISTO KWIWEKO ameiambia KAHAMA FM kuwa tayari amewaandikia barua wafanyabishara hao ambao wamekuwa wakiweka bidhaa hizo nje ya maduka yao kinyume na taratibu za TFDA.

Amewataka Wafanyabiashara hao kufuata sheria, taratibu na kanuni zilizowekwa na mamalaka hiyo ili kuepuka madhara kwa walaji yanayotokana na kutumia bidhaa ambazo hazijahifadhiwa sehemu sahihi zikiwemo zilizokwisha muda wake.

KWIWEKO amesema kuwa kwa wafanyabiashara wanaojishughulisha na biashara ya vyakula, vipodozi na madawa wanapaswa kuwa na vibali kutoka TFDA.
Share:

SHIRIKA LA WORLD VISION LATOA MSAADA KWA VIFAA VYA KUPIMA HALI YA LISHE NA UDUMAVU VYENYE THAMANI YA ZAIDI YA SH. MIL 100.


Na Salvatory Ntandu
KAHAMA.

Serikali Mkoani SHINYANGA imepokea vifaa vya kupima hali ya lishe na udumavu vyenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 100 kutoka shirika lisilo la kiserikali la World Vision.

Vifaa hivyo vimekabidhiwa kwa Mkuu wa Wilaya ya KAHAMA, FADHILI NKURLU kwa niaba ya mkuu wa Mkoa wa SHINYANGA, katika Hafla iliyofanyika katika Zahanati ya Kilago katika halmashauri ya mji wa Kahama.

NKURLU amelishikuru Shirika la Word Vision kwa kuchangia maendeleo ya sekta ya Afya mkoani Shinyanga kupitia Mradi wake wa uboreshaji lishe na afya ya uzazi kwa mama na mtoto (ENRICH).

Kwa upande wake, Meneja Mradi wa (ENRICH) MWIVANO MALIBWI amesema wamelenga kuboresha hali ya lishe kwa Mama na mtoto kwa kuwajengea uwezo wa kutambua athari za lishe duni.

Naye Kaimu Mganga Mkuu wa mkoa wa Shinyanga, Dkt. JOHN MFUTAKAMBA amesema tatizo la udumavu bado ni kubwa, hivyo wazazi wanapaswa kuzingatia lishe bora kwa watoto wao..

Mradi wa ENRICH unatekelezwa katika mikoa mitatu hapa nchini ambayo ni Shinyanga, Tabora na Simiyu na utakamilika mwaka 2020.
Share:

AHUKUMIWA KWENDA JELA AU KULIPA FAINI KWA KOSA LA KUAJIRI RAIA WA KIGENI


Na Paulina Juma
KAHAMA.

Mkazi wa MALUNGA mjini Kahama HAMIDA JUMA amehukumiwa kwenda jela mwaka mmoja au kulipa faini ya Shilingi 500,000/= kwa kosa la kumuajiri raia wa BURUNDI asikuwa na kibali cha kuishi nchini.

Hukumu hiyo imetolewa jana na hakimu mkazi wa mahakama ya wilaya ya Kahama IMAN BATENZI baada ya HAMIDA kukiri kutenda kosa hilo mahakamani hapo.

Awali mwendesha mashitaka wa idara ya Uhamiaji SALUM RASHID amesema HAMIDA alikamatwa April 6 mwaka huu saa 4 asubuhi huko Malunga akiwa amemuajiri kufanya kazi za mamalishe raia huyo wa Burundi.

SALUM amesema HAMIDA amefanya kosa hilo kinyume na kifungu cha 45 na kifungu kidogo cha 2 cha sheria ya uhamiaji namba 7 ya 1995 iliyofanyiwa marekebisho 2016.

Katika shauri hilo la jinai namba 47/2018, HAMIDA ameshindwa kulipa faini na ameanza jana kutumikia kifungo hicho jela.
Share:

AFIKISHWA MAHAKAMANI KWA TUHUMA ZA MAUAJI


Na Lilian Katabaro
KAHAMA.
 
Mkazi wa kijiji cha Bubungu Wilayani KAHAMA Mkoani Shinyanga, NAOMI MABULA (21) jana amefikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Kahama kwa tuhuma za mauaji ya PASCHAL KASHINDYE.

Mbele ya Hakimu Mkazi wa Mahakama hiyo KENETH MUTEMBEI, mwendesha mashitaka wa Jeshi la Polisi MASAU MASATU amesema Machi 16 mwaka huu saa sita usiku katika kijiji cha Bubungu MABULA alimuua KASHINDYE kwa kutumia panga.

MASAU amesema NAOMI ametenda kosa hilo kinyume na kifungu namba 196 sura ya 16 kanuni ya adhabu marejeo ya mwaka 2002.

Katika shauri hilo la jinai namba 07/2018, NAOMI hakutakiwa kujibu chochote kwasababu Mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo ya mauaji.

NAOMI amerudishwa rumande na shauri hilo litatajwa tena Mahakamani hapo Machi 29 mwaka huu.
Share:

WANAWAKE ZAIDI YA ASILIMIA 70 WANAOTIBIWA HOSPITALI YA WILAYA KAHAMA HUSUMBULIWA NA MAGONJWA YA KINYWA


Na Sebastian Mnakaya
KAHAMA.

Zaidi ya asilimia 70 ya wanawake wanaotibiwa katika Hospitali ya Wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga, wanasumbuliwa na magongwa ya kinywa kutokana na ulaji wa vyakula vitamu mara kwa mara hali inayosababisha meno yao yatoboke.

Hayo yameelezwa na mganga wa meno kutoka katika Hospital ya halmashauri ya mji wa Kahama, DR ATHUMANI HUSSENI JUMA katika mahojiano na kahama FM kuhusiana na maadhimisho ya siku ya kinywa na meno duniani leo.

Kwa mujibu wa Dk. JUMA, watoto wa umri wa miaka 2 mpaka watu wazima walio na umri wa miaka 45 wako kwenye hatari zaidi ya kupata magonjwa ya kinywa na meno wasipozingatia afya ya kinywa.

Dk JUMA ametoawito kwa Wananchi kuwa na utaratibu wa kuangalia afya zao za kinywa na meno mara kwa mara na kupata matibabu mapema kuepuka kupata kansa ya kinywa.
Share:

JAMII WILAYANI KAHAMA YATAKIWA KUACHANA NA IMANI POTOFU YA KUWAKATA WATOTO NDIMI ZAO


Na Salvatory Ntandu
KAHAMA

Jamii wilayani KAHAMA Mkoani SHINYANGA imetakiwa kuondokana na imani potofu za kuwata watoto wachanga ndimi ili kuzuia kupata tatizo la kuzungumza(Ububu) jambo ambalo linaweza kusababisha vifo na kigugumizi wakati wa kuzungumza.

Kauli hiyo imetolewa leo na Mkuu wa kitengo cha Meno katika Hospitali ya Halmashauri ya Mji wa KAHAMA DK ATHUMANI HUSEIN JUMA wakati akizungumza na KAHAMA FM kuhusiana na suala hilo.

Amesema ofisi yake imebaini kuwepo kwa Mama mmoja anayejifanya ni mtaalamu wa kukata watoto wachanga ndimi pindi wanapozaliwa jambo ambalo linasababisha madhara kwa watoto.

Amefafanua kuwa Tatizo la kuzungumza kwa mtoto (Ububu) linatokana mtu kuwa na tatizo kwenye ubongo hivyo wapaswa kutowapeleka watoto wao.

Hatua hiyo imekuja baada ya kuwepo kwa watoto wachanga ambao wamebainika kukatwa ndimi zao kwa kile kinachodawa kuwa ni kuzuia tatizo la Ububu.
Share:

AHUKUMIWA KWENDA JELA AU KULIPA FAINI KWA KOSA LA KUINGIA IFADHINI BILA KIBALI


Na Lilian Katabbaro
KAHAMA

Mkazi wa Wilaya ya Bukombe Mkoani Geita, JACOB MASUMBUKO (44) jana amehukumiwa kwenda jela mwaka mmoja au kulipa faini ya shilingi 350,000/= kwa kosa la kuingia ndani ya Pori la Akiba la Moyowosi-Kigosi bila kibali.

Akitoa Hukumu hiyo, Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Wilaya ya Kahama IMANI BATENZI amesema ametoa hukumu hiyo baada ya mshitakiwa MASUMBUKO kukiri kutenda kosa hilo Mahakamani hapo.

Awali mwendesha mashitaka wa Idara ya Wanyamapori CATHERINE ALOYCE amesema MASUMBUKO alikamatwa March 16 mwaka huu huko Bulumbaga ndani ya Pori hilo la Akiba la Moyowosi-Kigosi akiwa hana kibali kinachomruhusu kuwa katika eneo hilo.

ALOYCE amesema katika shauri hilo la jinai namba 120/2018, MASUMBUKO ametenda kosa hilo kinyume na kifungu namba 15 cha sheria ya wanyamapori namba 5 ya mwaka 2009.

MASUMBUKO ameshindwa kulipa faini na ameanza leo kutumikia kifungo chake jela.
Share:

MICHE YA MITI INAYOOTESHWA KWA AJILI YA UTUNZAJI WA MAZINGIRA YAARIBIWA NYASUBI SHULE YA MSINGI


Na Ndalike Sonda
KAHAMA

Miche ya miti inayooteshwa kwaajili ya utunzaji wa mazingira katika shule ya msingi Nyasubi Mjini KAHAMA imeelezwa kuharibiwa na mifugo kutokana na ukosefu wa uzio katika shule hiyo.

Hayo yamesemwa na Mwalimu wa Mazingira wa shule hiyo RACHEL IRUGA wakati akizungumza kuhusu utanzaji wa miti shuleni hapo, kwenye kipindi cha Raha ya leo kinachorushwa na KAHAMA FM.

Kutokana na changamoto hiyo, Mwalimu IRUGA ameiomba serikali kusaidia kujenga uzio katika eneo la shule hiyo ili kudhibiti uharibifu wa mazingira unaotokana na baadhi ya wananchi kuchungia mifungi yao katika eneo la shule pamoja na wapita njia.

Akizungumzia tatizo hilo, Mkazi wa Mtaa wa Nyakato ilipo shule hiyo, RASHID ATHUMAN ameiomba serikali itoe elimu shirikishi kwa wananchi ili wasaidie kulinda na kutunza maeneo ya shule.

Afisa Elimu shule za Msingi Halmashauri ya Mji wa Kahama, ALUKO LUKOLELA, amesema shule ni mali za wananachi hivyo ni jukumu lao kushirikiana kutunza mazingira na kwamba kutokana na kipaumbele cha vyumba vya madarasa hawawezi kujenga uzio huo kwa sasa.

Kukosekana kwa uzio katika shule nyingi za Serikali kumesababisha uharibifu wa mazingira, wizi na uvamizi wa maeneo ya shule.
Share:

WANANCHI ISAGEHE WAIOMBA HALMASHAURI KUMALIZIA BOMA LA OFISI YA SERIKALI YA KIJIJI


Na Ndalike Sonda
KAHAMA

Wananchi wa Kijiji cha MPERA kata ya ISAGEHE Halmashauri ya Mji wa KAHAMA wameiomba halmashauri hiyo kumalizia boma la ofisi ya serikali ya kijiji hicho baada ya kutelekezwa kwa zaidi ya miaka 13.

Wakizungumza jana na KAHAMA FM kwa niaba ya wananchi wengine, MANYANDA NDUBA na ALFERD HUNGWI wamesema wananchi walihamasishwa kuchangia ujenzi huo tangu mwaka 2005 ambapo walikamilisha boma hilo.

Mwenyekiti wa serikali ya Kijiji hicho, ALON MAKINGA amesema taarifa za ukamilishaji wa bomba hilo zipo kwenye ofisi ya halmashauri ya Mji wa Kahama na kwamba wananchi wamesaidia pia upatikanaji wa mbao za kenchi na bando mbili za mabati.

Afisa Uchumi wa Halmashauri ya Mji wa Kahama ANGERIA CLAVERY amesema jengo hilo halijakamilika kutokana kipaumbele cha ujenzi wa vyumba vya madarasa na katika mwaka wa fedha 2017/18 wametenga kiasi cha shilingi milioni 15 kwaajili ya ukamilishaji wa jingo hilo.
Share:

WANANCHI WANAOLIZUNGUKA BWAWA LA NYIHOGO KAHAMA WATAKIWA KUJIEPUSHA NA UHARIBIFU WA MAZINGIRA BWAWANI HAPO



Na William Bundala
KAHAMA

Wananchi wanaozunguka bwawa la NYIHOGO Mjini KAHAMA Mkoani SHINYANGA wametakwa kujiepusha na shughuli zozote zinazosababisha uharibifu wa mazingira katika bwawa hilo.

Akizungumza jana na KAHAMA FM, kuelekea wiki ya Maji duniani, Mwenyekiti wa bodi ya mamlaka ya maji na usafi wa mazingira KAHAMA, (KUWASA) Meja Mstaafu BAHATI MATALA amesema mamlaka hiyo imeanza kudhibiti uharibifu katika bwawa hilo

MATALA amesema wananchi wanapaswa kutambua kuwa eneo hilo kwa sasa linahifadhiwa na kulindwa kwa mujibu wa sheria baada ya kuwa limekabidhiwa rasmi kwa KUWASA na kwamba mikakati mbalimbali imeanza kufanyika ikiwamo upandajiwa wa miti.

KUWASA imejidhatiti kuliboresha bwawa hilo kwa lengo la kusaidia kupata huduma ya maji hasa katika taasisi mbalimbali mjini Kahama pindi inapotokea dharua ya ukosefu wa huduma ya maji kutoka mradi wa ziwa victoria.

Wiki ya maji duniani inaanza kesho ambapo KUWASA itatoa elimu mbalimbali kwa wateja wake na kauli mbiu ya mwaka huu ni “Hifadhi maji na mfumo wa kiikolojia kwa maendeleo ya jamii”
Share:

AHUKUMIWA KUNYONGWA HADI KUFA KWA KOSA LA KUMUUA MTOTO



Na Lily/Danny
KAHAMA

Mkazi wa kata ya Nyasubi mjini Kahama Mkoani Shinyanga, SAMSONI BWIRE (60) amehukumiwa kunyongwa hadi kufa baada ya kupatikana na hatia ya kumuua mtoto DEVOTA GERARD(4) kwa makusudi.

Hukumu hiyo imetolewa na Jaji wa Mahakama kuu kanda ya SHINYANGA, RICHARD KIBELLA baada ya kuridhika na ushahidi uliotolewa na mashahidi tisa wa upande wa jamhuri ambao wamethibitisha kosa hilo pasipo kuacha shaka yeyote.

KIBELLA amesema mashahidi hao wameithibitishia Mahakama hiyo kuwa BWIRE alimuua kwa makusudi DEVOTA GERARD kwa kutumia panga May 16/2013 katika kata ya Nyasubi Mjini Kahama huku akijua kuwa ni kosa kisheria.

Jaji KIBELA amesema mahakama hiyo imetoa adhabu hiyo ili iwefundisho kwake na kwa watu wengine kwenye jamii ambao wanajichukulia sheria mkononi na kuwadhuru watu wengine kwa maslahi yao binafsi.

Awali akisoma maelezo ya shauri hilo la mauaji namba 23/2013 wakili wa Selikali, UPENDO SHEMKOLE amesema BWIRE amekiuka kifungu cha sheria namba 196 na 197 cha kanuni ya adhabu sura ya 16 marejeo ya mwaka 2002 na kuiomba kutoa adhabu kali.

Nae wakili wa utetezi FESTO LEMA ameiomba mahakama kumpunguzia adhabu mteja wake kwani anafamilia inayomtegemea na ni kosa lake la kwanza hoja ambayo imetupiliwa mbali na Mahakama hiyo.

BWIRE ameanza jana kutumikia adhabu hiyo.
Share:

HALMASHAURI YA MJI WA KAHAMA YASEMA HAMASA YA USAFI WA MAZINGIRA IMEPUNGUA



Na Sebastian Mnakaya
KAHAMA

Halmashauri ya Mji wa KAHAMA Mkoani SHINYANGA imekiri kuwa mwaka huu hamasa ya wananchi wa halmashauri hiyo kufanya usafi wa mazingira katika siku zilizopangwa na Serikali imepungua ukilinganisha na mwaka jana.

Akizungumza na KAHAMA FM, Mkuu wa idara ya Usafi na mazingira halmashauri ya Mji wa Kahama, MARTINE MASELE amesema hali hiyo inatokana na mazoea ya wananchi kusubiri usimamizi wa maafisa kutoka serikalini.

Kutoka na hali hiyo, MASELE amesema wamekusudia kuanza kuchukua hatua za kisheria dhidi ya wanaoshindwa kutekeleza agizo hilo ambapo amewaomba wananchi kuendelea kutii agizo hilo bila shuruti.

Kwa mujibu wa MASELE, zaidi ya tani 121 za takataka zinazalishwa kila siku katika kata 12 zenye msongamano mkubwa wa watu katika mji wa Kahama huku ukusanyaji wake ukiwa ni wakuridhisha.

Zoezi la usafi wa mazingira kila jumamosi ya mwisho wa mwezi ni agizo la rais JOHN MAGUFULI alilolitoa Desemba 9 mwaka 2015 huku wilaya ya Kahama ikitekeleza agizo hilo pia Jumamosi ya katikati ya kila mwezi.
Share:

RAIA WAWILI WA BURUNDI WAHUKUMIWA KWENDA JELA MIAKA MIWILI


Na Daniel Magwina
KAHAMA

Raia wawili wa Burundi, STEVEN ELIAS (30) na IMINA NAJIRI(18) wamehukumiwa kwenda jela miaka 2 na miezi 6 au kulipa faini ya shilingi 500,000 kila mmoja kwa kosa la kuwepo nchini kinyume na sheria ya uhamiaji.

Akitoa hukumu hiyo hakimu mkazi wa mahakama ya wilaya ya KAHAMA IMANI BATENZI, amesema ametoa hukumu hiyo baada ya washitakiwa kukiri kutenda kosa hilo mahakamani hapo.

SALUMU RASHID amesema washitakiwa wote kwa pamoja walikamatwa Februar 27 mwaka huu majira ya saa 4 asubuhi katika mtaa wa Shunu mjini Kahama huku vibali vyao vya kuwepo nchini vikiwa vimekwisha muda wake.

Katika shauri hilo la jinai namba 86/2018, washitakiwa wanadaiwa kutenda kosa kinyume na kifungu namba 45 cha sheria ya Uhamiaji namba 7 ya mwaka 1995 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2016.

Hata hivyo washitakiwa wameshindwa kulipa faini na wameanza kutumikia vifungo vyao leo na mara baada ya kumaliza vifungo hivyo watarejeshwa nchini kwao Burundi.
Share:

TISA WAFIKISHWA MAHAKAMANI KWA KOSA LA UNYANG'ANYI WA KUTUMIA SILAHA NA KUNUNUA MALI YA WIZI



Na Lilian Katabbaro
KAHAMA

Watu tisa wamefikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya KAHAMA kwa makosa mawili tofauti ikiwemo unyang’anyi wa kutumia silaha na kununua mali ya wizi yenye thamani ya shilingi milioni 80 mali ya EMANUELI KALAMU.

Mbele ya Hakimu Mkazi wa Mahakama hiyo KENETH MUTEMBEI, mwendesha mashitaka wa Jeshi la Polisi, EVODIA BAIMO amedai washitakiwa hao wametenda kosa hilo March 8 mwaka huu majira ya saa 8 usiku huko katika kijiji cha Rwabakanga mkoani Geita.

Waliofikishwa Mahakamani leo ni SHIJA CHARLES(20) mkazi wa Kakola na SAIDI MANYAKENDA(18) Mkazi wa Busindi katika Halmashauri ya Msalala wilayani Kahama na YUSUPHU ELIDASU(36) na FIKIRI NGANGA(20) wote wakazi Rwabakanga mkoani Geita.

Wengine ni ALFONCE HASSAN (19), GERALD THOMAS (34), JOEL RAPHAEL (27) EZEKIELI MPIPI (19) na STAMILI SULI (18) Wote wakazi wa mkoani Geita.

BAIMO ameiambia Mahakama kuwa washitakiwa wote kwa pamoja walipatikana wakiwa na kg 300 za kemikali aina ya kaboni yenye thamani ya shilingi milioni 80 inayotumika katika uchenjuaji wa dhahabu, mali ya EMANUELI KALAMU huku wakijua kuwa ni mali ya wizi.

BAIMO amefafanua kuwa katika shitaka la kwanza watuhumiwa SAIDI SHIJA, CHARLES SAIDI, YUSUF ELIDASU na FIKIRI NGANGA wametenda kosa la unyang’anyi wa kutumia silaha kinyume na kifungu namba 287 A cha kanuni ya adhabu sura ya 16 marejeo ya mwaka 2002.

Aidha katika shitaka la pili, Washitakiwa ALPHONCE HASSAN, GERALD THOMAS, JOEL RAPHAEL, EZEKIEL MPIPI na STAMILI SULI wametenda kosa la kukaa na mali ya wizi kinyume cha kanuni ya adhabu sura ya 16 marejeo ya mwaka 2002.

Washitakiwa wote kwa pamoja wamekana mashitaka yanayowakabili huku washitakiwa wanne shitaka lao likiwa halina dhamana na washitakiwa watano wameshindwa kutimiza mashariti ya dhamana ambapo wote wamerudishwa rumande hadi March 28 mwaka huu shauri hilo litakapo sikilizwa tena.
Share:

MVUA ILIYONYESHA JUZI YASABABISHA KIFO KATIKA KIJIJI CHA TULOLE WILAYANI KAHAMA


Na Salvatory Ntandu
KAHAMA

MVUA kubwa zilizonyesha juzi usiku zimesababisha kifo cha Mtoto mmoja aliyefahamika kwa jina la MARITA MAZIKU (5) aliyeangukiwa na ukuta.

Akizungumza na KAHAMA FM leo Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Tulole katika Halmashauri ya Mji wa KAHAMA, SHABAN PASCAL MITUNDU pia amesema nyumba 30 zimebomolewa kufuatia mvua hiyo kubwa.

Sanjari na athari hizo, MITUNDU amesema Nyumba nyingi zimepata nyufa huku zingine zikianguka na kutoa rai kwa wakazi kuhama katika nyumba hizo ili kuepuka maafa zaidi.

Kwa upande wake MAZIKU KULWA ambaye mtoto wake amefariki dunia katika Tukio hilo amesema usiku akiwa amelala na familia yake ghafla alishangaa kuona wamefunikwa ukuta wa nyumba yao huku wakikosa masaada.

Amesema baada ya kupata Msaada kutoka kwa Majirani walipelekwa katika kituo cha Afya cha Igalilimi ambapo walipatiwa matibabu lakini kwa bahati mbaya mwanaye alifariki dunia wakati akipatiwa matibabu na mazishi yake yamefanyika jana kijijini hapo.

Hivi karibuni Mamlaka ya Hali ya Hewa nchini (TMA) imetangaza kuwepo kwa Mvua kubwa katika Mikoa 10 ikiwemo ya kanda ya pwani, kati na nyanda za juu kusini kutokana na ongezeko la mgandamizo wa hali ya hewa kwenye Bahari ya Hindi.

Share:

MADEREVA BAJAJI MTAA WA MHONGOLO WAFUNGA BARABARA KWA MASAA MAWILI



Na Ndalike Sonda
KAHAMA

Ubovu wa barabara ya muda inayotumika kusafirisha abiria kutoka Mjini KAHAMA kwenda Mtaa wa MHONGOLO umesababisha baadhi ya waendesha pikipiki za magurudumu matatu (Bajaji) kufunga barabara hiyo kwa zaidi ya saa mbili, kushinikiza serikali iifanyie ukabarabati.

Baadhi ya waendesha Bajaj wamesema wamelazimika kufunga barabara ili kufikisha kilio chao kwa serikali kwani wamekuwa wakipata usumbufu kutokana na ujenzi wa barabara hiyo ya Mhongolo.

Jeshi la Polisi wilayani Kahama kupitia mkuu wa kitengo cha Usalama barabarani, DESDERY KAIGWA limewaelekeza Madereva hao wa Bajaj kufuata taratibu kwa kupeleka malalamiko yao kwa viongozi wanaohusika kuliko kufunga barabara kwani kufanya hivyo ni kuvunja sjeria.

Kwa upande wake, Meneja wa Wakala wa barabara TANROADS mkoa wa Shinyanga, MIBARA NDIRIMBI amesema hali hiyo inatokana na kutokuwepo kwa mipango miji bora hali inayosababisha maji kuharibu miundombinu hiyo na kwamba amemuagiza mkandarasi kuboresha barabara ya muda.

Barabara hiyo ya muda inayotoka Mjini Kahama kwenda Mhongolo inatumika kutokana na kuwepo kwa ujenzi wa barabara yenye kiwango cha Lami kutoka Mjini Kahama hadi Mhongolo.
Share:

OFISI YA MKURUGENZI WA HALMASHAURI YA MSALALA WILAYANI KAHAMA YAOMBA RADHI KWA KUWASILISHA TAARIFA ISIYO RASMI KWENYE KIKAO



Na Amina Mbwambo
KAHAMA

Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya MSALALA wilayani KAHAMA Mkoani SHINYANGA imelazimika kuomba radhi katika kikao cha Kamati ya Ushauri cha wilaya ya KAHAMA (DCC) baada ya kuwasilisha mbele ya kamati hiyo taarifa isiyokidhi matakwa ya kikao hicho.

Akiomba radhi kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo SIMON BEREGE, Mwanasheria wa Halmashauri, MASHAKA MABULA amesema upungufu uliojitokeza umesababishwa na taarifa za ghafla za yeye kukaimu nafasi hiyo ya Mkurugenzi Mtendaji.

Akizungumzia hali hiyo, Mwenyekiti wa kikao hicho ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya na Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Kahama, FADHILI NKURLU ameitaka Halmashauri hiyo kuwa makini katika kushughulikia taarifa zake kwani tatizo hilo linaonekana kujirudiarudia.

Baadhi ya wajumbe wa kikao hicho cha Kamati ya Ushauri cha Wilaya ya Kahama akiwemo Diwani wa Kata ya Nyihogo, SHEDRACK MGWAMI na Diwani wa Kata ya ISAKA, GERALD MWANZIA wameeleza kusikitishwa kwao juu ya taarifa hiyo ya Halmashauri ya Msalala.

Katika kikao hicho cha siku moja, Wajumbe wa Kamati hiyo ya Ushauri ya Wilaya ya Kahama pamoja na mambo mengine wamesisitiza umuhimu wa Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (TARURA), kufanya mazungumzo na halmashauri zenye mitambo ya kutengeneza bara bara ili waweze kutumia mitambo hiyo.

Aidha wajumbe wamesisitiza mapendekezo ya bajeti ya halmashauri husika yapitishwe kwenye kamati ya ushauri ya wilaya kabla ya kujadiliwa na madiwani, na halmashauri ziwasilishe maombi serikali kuu ili kuwahishiwa fedha za ruzuku kwa ajili ya kutekeleza bajeti zao.
Share:

KUWASA KAHAMA YAAGIZWA KUFUFUA CHANZO CHA MAJI CHA NYIHOGO


Na Amina Mbwambo
KAHAMA

SERIKALI wilayani KAHAMA imeiagiza Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira mjini Kahama (KUWASA) kuhakikisha inakifufua na kukitunza chanzo cha maji cha Bwawa la Nyihogo ili kitumike wakati chanzo kikuu cha maji kutoka ziwa Victoria kinapopata hitilafu.

Agizo hilo limetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Kahama, FADHILI NKURLU wakati wa zoezi la upandaji miti katika Bwawa hilo la Nyohogo lililofanyika jana chini ya uratibu wa Wakala wa Misitu (TFS), wilayani humo.

Akizungumza wakati wa zoezi hilo, Mwenyekiti wa Bodi ya KUWASA, Meja Mstaafu BAHATI MATALA ameishukuru serikali kwa kulirudisha eneo hilo rasmi chini ya KUWASA na ameahidi kulisimamia na kuliendeleza.

Amesema Mamlaka yake tayari imepanda miti 6100 katika juhudi za kupambana na uharibifu mkubwa wa mazingira uliosababishwa na shughuli za kibinadamu katika Bwawa hilo la Nyihogo.

Jumla ya miche ya miti 500 ilipandwa katika chanzo hicho cha Nyihogo jana, huku kaimu meneja wa TFS wilaya ya Kahama, MOHAMED DOSSA akibainisha kuwa wanatarajia kupanda miti 34,000 katika eneo la mita za mraba 53,125 wilayani humo mwezi huu.

DOSSA ameibanisha kuwa nia ya Wakala wa Misitu ni kuhakikisha wilaya ya Kahama inakuwa na mandhari ya kijani wakati wote.

Takwimu zinaonesha kuwa Tanzania bara ina jumla ya hekta milioni 48.1 za misitu ambayo ni sawa na 55% ya eneo lote la Tanzania bara.
Share:

AFIKISHWA MAHAKAMANI KWA KUBAKA MWANAFUNZI.



Mkazi wa kijiji cha Ntobo Wilayani KAHAMA Mkoani SHINYANGA, BARAKA CHALESI (19) jana amefikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya KAHAMA kwa tuhuma za kumbaka mwanafunzi na kumsababishia ujauzito kinyume cha sheria.

Mbele ya Hakimu Mkazi wa Mahakama hiyo KENETH MUTEMBEI, mwendesha mashitaka wa Polisi EVODIA BAIMO amesema, CHALESI kwa nyakati tofauti mwezi Novemba 2017 huko kijiji cha Ntobo bila uhalali alimbaka mwanafunzi huyo na kumsababishia ujauzito.

BAIMO amefafanua kuwa CHALESI ametenda kosa hilo kinyume na kifungu namba 130 na 131 cha kanuni ya adhabu sura ya 16 marejeo ya mwaka 2002, na kifungu cha Sheria ya Elimu namba 60 A sura ya 353 kama ilivyofanyiwa marekebisho na sheria namba 2 ya mwaka 2016.

Katika shauri hilo la jinai namba 107/2018 CHALESI amekana kutenda kosa hilo na upelelezi wa shauri hilo haujakamilika na mshitakiwa amerudishwa rumande kwa kukosa dhamana hadi shauri hilo litakakapotajwa tena March 23 mwaka huu.
Share:

RAIA WAWILI WA BURUNDI WAFIKISHWA MAHAKAMANI BAADA YA KUINGIA NCHINI KINYUME CHA SHERIA

Raia wawili wa Burundi jana wamefikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya KAHAMA kwa tuhuma za kuingia nchini bila kuwa na vibali maalum kinyume cha sheria.

Mbele ya Hakimu Mkazi wa Mahakama hiyo KENETH MUTEMBEI, mwendesha mashitaka wa Jeshi la Polisi SHABANI MATESO amewataja washitakiwa hao kuwa ni FROLENCE NDAHIZEHE (27) na JANETH MTONELE (22) wote wawili wakiwa ni raia wa BURUNDI.

MATESO amefafanua washitakiwa hao walikamatwa March 6 mwaka huu majira ya saa 7 usiku huko mtaa wa Mwime Wilayani KAHAMA wakiwa hawana kibali kinachowaruhusu kuwemo nchini.

Katika shauri hilo la jinai namba 93/2018, washitakiwa wametenda kosa kinyume na kifungu namba 45 cha sheria ya uhamiaji namba 7 ya mwaka 1995 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2016.

Washitakiwa wote kwa pamoja wamekiri kutenda kosa hilo na wamerudishwa rumande baada ya kukosa dhamana hadi March 14 mwaka huu shauri lao litakapotajwa tena.

Share:

WANANCHI WA PUGU BUKONDAMOYO MJINI KAHAMA WAMEKUBALI KUCHANGIA FEDHA KWA AJILI YA MAENDELEO YA KIJAMII.



Na Ndalike Sonda
KAHAMA.


Wananchi wa Kitongoji cha Pugu mtaa wa Bukondamoyo mjini Kahama wamekubaliana kuchangia fedha na nguvu kazi ili kufanikisha uwekaji wa changarawe na mawe kwenye daraja lililopo katika kitongoji hicho, ili kuwezesha barabara hiyo kuanza kutumika.

Wakizungumza leo kwenye kipindi cha Raha ya leo kinachorushwa na Kahama FM baadhi ya wananchi wamesema kutokana na kero ya barabara inayowakabili kwa muda mrefu, serikali ya mataa iliitisha mkutano na wananchi, na kupitisha maazimio hayo.

Mwenyekiti wa Mtaa wa Bukondamoyo NASHONI YOHANA amesema daraja hilo limejengwa tangu mwaka jana na hakuna mwendelezo wowote na kwamba wanakusudia kukamilisha baada ya wiki moja ili barabara hiyo ianze kutumika.

Diwani wa kata ya Mhungula IGNAS SHABAN amewapongeza wananchi hao, na kuahidi kushirikiana nao katika shughuli mbalimbali za maendeleo, ikiwamo ukamilishaji huo wa daraja katika barabara ya kitongoji cha Pugu.

Mkuu wa kitengo cha Uhandisi kutoka wakala wa barabara za mjini na vijijini (TARURA) halmashauri ya mji wa Kahama Mhandisi, YUSUPH SHABAN amesema wananchi wanaruhusiwa kufanya marekebisho hayo lakini wawashirikishe wataalam wanaohusika kutoka TARURA.

Hata hivyo Mhandisi SHABAN amesema TARURA inaendelea kukabarabati barabara mbalimbali zilizopo mjini Kahama kulingana na bajeti ya mwaka wa fedha 2017/2018.
Share:

SERIKALI WILAYANI KAHAMA KUENDESHA MSAKO WA WAFANYABIASHARA WA MBAO, ALMINIUM NA WACHOMELEAJI.





Na Salvatory Ntandu
KAHAMA


Serikali wilayani KAHAMA imesema itaendesha msako wa wafanyabiashara wa mbao, alminium na wachomeleaji vyuma ambao wamekaidi kuhamia katika eneo jipya walilotengewa la Dodoma baada ya kukamilisha uwekaji wa miundo mbinu muhimu ukiwemo umeme katika eneo hilo.

Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa Wilaya ya KAHAMA, FADHILI NKURLU wakati akizungumza na Waandishi wa habari Mjini humo ambapo amesema wapo baadhi ya wafanyabiashara ambao hawataki kuhamia katika eneo hilo.


NKURLU amesema ofisi yake imepokea taarifa za baadhi ya wamiliki wa nyumba mjini Kahama kuwapangisha kwa siri watu wanaochomelea vyuma katika Nyumba zao licha ya kutambua madhara yatokanayo na moto.

Kwa upande wao baadhi ya mafundi wanaochomelea katika eneo la Lumambo, RASHID OMAR na ISSA JUMA wamesema wao hawapingani na agizo la serikali ila wanachoomba ni kuboreshewa mazingira ya kazi katika eneo hilo la Dodoma.

Mwaka jana Halmashauri ya mji wa Kahama iligawa viwanja zaidi ya 400 katika eneo la Dodoma kwa wafanyabiashara wa mbao, aluminum na wachomeleaji vyuma baada ya eneo lao la awali la Majengo kuteketezwa kwa moto.
Share:

SHULE YA MSINGI ISAGEHE YAKABILIWA NA UHABA WA MATUNDU YA VYOO.





Na Ndalike Sonda
KAHAMA


Jumla ya wavulana 339 wanaosoma katika Shule ya Msingi Isagehe Halmashauri ya Mji wa KAHAMA wanakabiliwa na ukosefu wa matundu ya choo hali ambayo imesababisha watumie matundu yaliyokuwa yakitumiwa na wanafunzi wasichana wa shule hiyo. 

Hayo yamebainishwa na Mwalimu mkuu wa shule hiyo, NAMSEMBA MRISHA wakati akipokea msaada wa vifaa vya ujenzi kutoka kwa baadhi ya wanafunzi waliowahi kusoma katika shule hiyo.
 
Akizungumza wakati wa kukabidhi msaada huo, Mwenyekiti wa wanafunzi waliosoma katika shule hiyo, ZABRON FEGA amesema wametoa mifuko ya saruji 30, Nondo 50 na malori 10 ya mawe vyote vikiwa na thamani ya zaidi ya shilingi Milioni 2.
 
Mwenyekiti wa Kijiji cha Isagehe, ALEXANDER JOHN na mwenyekiti wa kamati ya shule hiyo, MABALA NKANDI wamesema wameahidi kikamilifu matumizi ya vifaa hivyo ili vitumike kwa malengo yaliyokusudiwa.

Nao baadhi ya wananchi wa Kijiji cha Isagehe wamepongeza jitihada zilizofanywa na wanafunzi hao wa zamani wa shule ya Msingi Isagehe na kwamba msaada wao umeleta mwamko kwa wazazi katika kuchangia sekta mbalimbali za maendeleo.

Kwa upande wake, Afisa elimu shule za msingi Halmashauri ya Mji wa Kahama, ALUKO LUKOLELA amesema Halmashauri yake itaendelea kushirikiana na wadau wa sekta ya elimu na kwamba wananchi wanapaswa kutambua kuwa serikali inaruhusu michango ya hiari.
 
Shule ya Msingi Isagehe ilianzishwa mwaka 1939 ambapo kwa sasa inawanafunzi 774 huku ukosefu wa matundu ya choo kwa wavulana ukidumu tangu mwaka 2015.
Share:

IDADI YA WASOMAJI

TUSIKILIZE LIVE KUPITIA TUNEIN

UNGANA NASI FACEBOOK HAPA

10 ZILIZOSOMWA ZAIDI

Labels

Blog Archive