TISA WAFIKISHWA MAHAKAMANI KWA KOSA LA UNYANG'ANYI WA KUTUMIA SILAHA NA KUNUNUA MALI YA WIZI



Na Lilian Katabbaro
KAHAMA

Watu tisa wamefikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya KAHAMA kwa makosa mawili tofauti ikiwemo unyang’anyi wa kutumia silaha na kununua mali ya wizi yenye thamani ya shilingi milioni 80 mali ya EMANUELI KALAMU.

Mbele ya Hakimu Mkazi wa Mahakama hiyo KENETH MUTEMBEI, mwendesha mashitaka wa Jeshi la Polisi, EVODIA BAIMO amedai washitakiwa hao wametenda kosa hilo March 8 mwaka huu majira ya saa 8 usiku huko katika kijiji cha Rwabakanga mkoani Geita.

Waliofikishwa Mahakamani leo ni SHIJA CHARLES(20) mkazi wa Kakola na SAIDI MANYAKENDA(18) Mkazi wa Busindi katika Halmashauri ya Msalala wilayani Kahama na YUSUPHU ELIDASU(36) na FIKIRI NGANGA(20) wote wakazi Rwabakanga mkoani Geita.

Wengine ni ALFONCE HASSAN (19), GERALD THOMAS (34), JOEL RAPHAEL (27) EZEKIELI MPIPI (19) na STAMILI SULI (18) Wote wakazi wa mkoani Geita.

BAIMO ameiambia Mahakama kuwa washitakiwa wote kwa pamoja walipatikana wakiwa na kg 300 za kemikali aina ya kaboni yenye thamani ya shilingi milioni 80 inayotumika katika uchenjuaji wa dhahabu, mali ya EMANUELI KALAMU huku wakijua kuwa ni mali ya wizi.

BAIMO amefafanua kuwa katika shitaka la kwanza watuhumiwa SAIDI SHIJA, CHARLES SAIDI, YUSUF ELIDASU na FIKIRI NGANGA wametenda kosa la unyang’anyi wa kutumia silaha kinyume na kifungu namba 287 A cha kanuni ya adhabu sura ya 16 marejeo ya mwaka 2002.

Aidha katika shitaka la pili, Washitakiwa ALPHONCE HASSAN, GERALD THOMAS, JOEL RAPHAEL, EZEKIEL MPIPI na STAMILI SULI wametenda kosa la kukaa na mali ya wizi kinyume cha kanuni ya adhabu sura ya 16 marejeo ya mwaka 2002.

Washitakiwa wote kwa pamoja wamekana mashitaka yanayowakabili huku washitakiwa wanne shitaka lao likiwa halina dhamana na washitakiwa watano wameshindwa kutimiza mashariti ya dhamana ambapo wote wamerudishwa rumande hadi March 28 mwaka huu shauri hilo litakapo sikilizwa tena.
Share:

No comments:

Post a Comment

IDADI YA WASOMAJI

TUSIKILIZE LIVE KUPITIA TUNEIN

UNGANA NASI FACEBOOK HAPA

10 ZILIZOSOMWA ZAIDI

Labels

Blog Archive