Lugola Ampa Siku 7 Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Mkoa wa Kagera (RCO)


Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola, ametoa siku saba kwa Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Mkoa wa Kagera (RCO), Obassy Nguvillan, kupeleleza upya kesi ya mama aliyechomewa nyumba katika eneo la Kyakailabwa Kata ya Nyanga, Manispaa ya Bukoba.

Lugola alitoa agizo hilo jana kutokana na watuhumiwa kukamatwa kisha kuachiwa na baadaye jalada kufungwa na Mwanasheria wa Serikali.

Kabla ya agizo hilo, mama huyo, Sauda Amir, alilalamika kwa Waziri Lugola katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika uwanja wa Uhuru Manispaa ya Bukoba na baadaye RCO alikiri kuwa inawezekana Jeshi la Polisi lilipeleleza kesi hiyo kwa udhaifu.

Lugola alisema kuwa haiwezekani mwanamke huyo achomewe nyumba, watuhumiwa anawafahamu halafu kesi iishe katika mazingira ambayo yana utata na kulazimika kumwita RCO kujibu.

“RCO natoa muda wa wiki moja ufanye kazi hii wewe mwenyewe, uchunguze kesi hii upya na unipe majibu,” alisema.

Akizungumzia tukio hilo, Sauda anayedai alifiwa na mumewe, alisema kuwa nyumba yake ilichomwa moto Juni 11, mwaka jana na kuwa kutokana na tukio hilo, kwa sasa hana mahala pa kuishi.

“Mheshimiwa Waziri, naomba unisaidie suala langu lipatiwe ufumbuzi, nahangaika na watoto, sina pa kuishi, kwa sasa mimi na watoto wangu saba tumepewa hifadhi na mama mmoja katika eneo la Kyakailabwa,” Alisema mama huyo
Share:

1 comment:

IDADI YA WASOMAJI

TUSIKILIZE LIVE KUPITIA TUNEIN

UNGANA NASI FACEBOOK HAPA

10 ZILIZOSOMWA ZAIDI

Labels