WAZIRI
Nishati Dk. Medard Kalemani amesema kukamilika kwa mradi wa ujenzi wa
mtambo wa kupoza umeme unaotarajiwa kujengwa Geita, kutawezesha serikali
kupeleka umeme wa gridi ya taifa katika Mgodi wa Dhahabu wa Geita
(Geita Gold Mine – GGM) na kuondoa sababu ya wao kutokulipa kodi stahiki
kwa serikali kwa kigezo cha kutumia mafuta katika uzalishaji.
Akikagua
eneo utakapojengwa mtambo huo, nje kidogo ya mji wa Geita, Desemba 31
mwaka huu, Waziri Kalemani alisema mtambo huo utafua umeme wa megawati
100 hivyo pamoja na kuwanufaisha wananchi wa Geita na maeneo jirani;
utatosheleza pia mahitaji ya mgodi husika ambayo ni takribani megawati
25.
“Ni
matumaini yangu, kufikia Desemba 2019, GGM watakuwa wameanza kutumia
umeme wa gridi ya taifa ili waanze kulipa kodi stahiki kwa serikali.
Waache kupata msamaha wa kodi wanaopata sasa kutokana na kuingiza mafuta
wanayotumia kuendeshea shughuli zao mgodini,” alisema Waziri.
Waziri
Kalemani aliongeza kwamba, kuwaunganisha GGM na umeme wa gridi,
kutakamilisha azma ya serikali kuwaunganishia umeme wachimbaji wa madini
wakubwa wote nchini kwani kwa sasa ni mgodi huo pekee uliobaki.
Alimtaka
Meneja wa TANESCO Mkoa wa Geita, Mhandisi Joackim Ruweta kuwapa taarifa
uongozi wa mgodi huo ili waanze kufanya maandalizi ya kuupokea umeme
kwenye miundombinu yao.
Akizungumzia
kuhusu mradi wenyewe, Waziri Kalemani alieleza kuwa serikali imetoa
takribani shilingi bilioni 23 kwa ajili ya kuujenga ili kuboresha hali
ya upatikanaji umeme kwa wananchi wa Geita na maeneo jirani.
Alisema mradi unahusisha kusafirisha umeme mkubwa kutoka Bulyanhulu, umbali wa kilomita 55 hadi Geita.
Aidha,
alisema kuwa taratibu zote za maandalizi zimekamilika hivyo akamtaka
mkandarasi atakayetekeleza mradi huo, ambayo ni kampuni ya CAMC
Engineering kutoka China kuanza mara moja shughuli za ujenzi, ambao kwa
mujibu wa mkataba utakamilika ndani ya kipindi cha miezi 17.
“Pamoja
na kuwa mkataba unabainisha muda wa kukamilisha ujenzi ni miezi 17
lakini tumekubaliana na mkandarasi ajitahidi kukamilisha ndani ya miezi
12,” alifafanua Waziri.
Akizungumzia
majukumu ya mkandarasi kwa mujibu wa mkataba, Waziri Kalemani alisema
yanajumuisha ujenzi wa mtambo wenyewe wa kupoza umeme katika eneo la
Mpomvu, nje kidogo ya mji wa Geita, ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme
kutoka Bulyanhulu hadi eneo la mtambo, umbali wa kilomita 55 pamoja na
kazi ya kusambaza umeme kwenye vijiji 11 vinavyopitiwa na mradi vikiwemo
vya Nyantororo na Buyagu.
Waziri
aliagiza mambo kadhaa yafanyike katika utekelezaji wa ujenzi wa mradi
huo ambayo ni pamoja na kujenga uzio kuzungushia eneo husika kwa sababu
za kiusalama pamoja na kuepusha watu kuvamia eneo husika na kujenga
makazi.
Pia,
aliagiza kuanza mara moja kwa kazi za kusafisha eneo husika pamoja na
kutoa elimu kwa wananchi ambako mradi unapita ili wajue namna ya
kujiandaa kuupokea mradi husika.
Waziri
Kalemani alikuwa katika ziara ya kazi kukagua utekelezaji wa miradi ya
umeme ambapo mbali na kukagua eneo utakapojengwa mtambo huo, aliwasha
umeme Katoro na Buseresere katika vijiji kadhaa pamoja na kuzungumza na
wananchi.
No comments:
Post a Comment