Wizara
ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto inalaani na
kukemea vikali vitendo vya ukatili dhidi ya watoto vinavyoendelea
kujitokeza nchini. Vitendo hivi vinafanywa na kuhusisha ndugu na walezi
wa karibu wa wataoto hivyo kuzua hofu kubwa kwa watoto na jamii kwani
vinaathiri malezi na makuzi ya awali ya watoto kwa kutozingatia haki zao
za msingi.
Mapema
wiki hii, imeripotiwa mwalimu wa shule ya msingi jijini Dodoma (jina
limehifadhiwa) ambaye anatuhumiwa kumfungia mtoto mdogo ndani ya kabati
kwa kipindi kirefu na kusababisha afya ya mtoto huyo kudhohofika.
Mwalimu huyo anatuhumiwa pia kumfanyia vitendo vya ukatili mama mzazi wa
mtoto huyo kwa kumpiga na kumsababishia maumivu mwilini yaliyopelekea
binti huyo na mtoto wake kulazwa.
Kipekee,
Wizara inawapongeza wanajamii wote walioibua tukio hili na kuwezesha
Jeshi la Polisi kumkamata mtuhumiwa kwa ajili ya uchunguzi ili Sheria
iweze kuchukua mkondo wake. TunaaminiJeshi la Polisi watafanya upelelezi
wa tukio hili kwa weledi mkubwa ili hatua stahiki za kisheria ziweze
kuchukuliwa.
Matukio
ya ukatili wa watoto yanapotokea majumbani yanarudisha nyuma jitihada
za Serikali za kulinda na kuendeleza haki na ustawi wa watoto katika
ngazi ya familia ambayo ndio kitovu cha jamii wakiwemo na watoto.
Kufuatia
kitendo hicho kilichofanywa na mwalimu wa shule ya msingi ambaye ni
mlezi wa watoto, Wizara inawataka wazazi, walezi na jamii kuzingatia
wajibu wa ulinzi wa watoto ili kuwahakikishia usalama wao katika maeneo
ya majumbani, shuleni, mtaani, njiani na katika jamii kwa ajili ya
kutekeleza lengo la kupunguza matukio ya ukatili kwa asilimia 50 ifikapo
mwaka 2021/2022.
Aidha,
Wizara inatoa rai kwa jamii na wananchi wema kuwa makini na matumizi ya
mitandao ya kijamii ili kuepuka makosa ya kisheria yanayoweza kutokea
kwa kusambaza, kuchapisha na kupiga picha za watoto ambao ni wahanga wa
ukatili na kuziweka wazi kinyume na Sheria ya Mtoto Na. 21 ya Mwaka
2009.
Wizara
inatoa pole kwa wazazi, ndugu, marafiki na familia ya mtoto
aliyefanyiwa ukatili huo. Tunawaomba wanajamii kuendelea kutoa
ushirikiano katika kufichua vitendo vyote vya ukatili dhidi ya watoto
vinavyojitokeza katika maeneo yao. Aidha, katika kipindi hiki ambapo
uchunguzi unaendelea kufanyika tunaomba pawe na utulivu na uvumilivu ili
kutoa nafasi kwa vyombo vya dola kufanya uchunguzi kwa makini na Sheria
iweze kuchukua mkondo wake.
Imetolewa na
Kitengo cha Mawasiliano Serikalini
Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto
(Idara Kuu Maendeleo ya Jamii)
02/01/2019
No comments:
Post a Comment