Naibu
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Angeline Mabula,
amewaonya baadhi ya watu wanaomiliki nyumba na kuendelea kuwatoza
wapangaji wao kodi za miezi sita na mwaka mmoja, kinyume na maelekezo ya
serikali, kuheshimu maelekezo hayo.
Naibu
waziri huyo alitoa onyo hilo jana, alipokuwa akihojiwa na kituo kimoja
cha redio na kuwataka wenye nyumba hao kuwasaidia mwananchi wa kawaida.
"Lengo
na madhumuni ni kumsaidia Mtanzania wa kawaida ambaye hutegemea kipato
cha mshahara ama biashara, ili aweze kufanya bajeti yake kama kulipa
nyumba ama matumizi mengine. Unapomwambia alipe miezi sita ama mwaka
mmoja unamtaka atafute kipato cha ziada akuridhishe mwenye nyumba halafu
mpangaji abaki na madeni kitu ambacho hakimsaidii Mtanzania," alisema.
Alisema mkakati wa serikali ni kuweka vitu katika usawa ili kuwawezesha wapangaji.
Mabula
alisema sheria kuhusu suala hilo bado haijatungwa, lakini ni vizuri
wenye nyumba wakajiandaa mapema ili sheria itakapopitishwa wawe
wameshazoea.
"Kwa
sasa ipo katika mchakato haujapelekwa muswada wa kusomwa bungeni kwa
kuwa bado hatujachukua maoni ya wadau, lakini ndani ya mwaka wa fedha
unaokuja itakuwa tayari maana imeonekana ni hitaji kubwa," alisema.
Mwishoni
mwa mwaka juzi, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William
Lukuvi, aliagiza watu wanaomiliki nyumba za kuzipangisha, kuacha
kuwatoza wapangaji wao kodi za miezi sita hadi mwaka mmoja ili wasio na
uwezo waweze kumudu maisha.
Waziri
Lukuvi, wakati akitoa agizo hilo, alisema mpangaji anatakiwa kulipa
kodi kila mwezi labda atake mwenyewe kulipa kwa miezi zaidi ya mmoja.
No comments:
Post a Comment