Kesi inayomkabili, aliyekuwa Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Jamal Malinzi na wenzake wanne imekwama kusikilizwa kwa sababu kiongozi wa jopo la mawakili wa utetezi, Richard Rweyongeza anaumwa.
Kesi hiyo imekwama kuendelea leo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbard Mashauri.
Wakili
 wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Leonard Swai 
amedai kesi hiyo ilipangwa kwa ajili ya kusikilizwa, wamejiandaa na 
shahidi yupo mahakamani.
Wakili
 wa utetezi, Abraham Senguji aliieleza mahakama kuwa kiongozi wa jopo la
 mawakili wa utetezi, Wakili Rweyongeza bado anaumwa.
Wakili
 Rweyongeza yeye ndiye aliyemsikiliza shahidi wa nane anayeendelea kutoa
 ushahidi katika kesi hiyo upande wa mashtaka kwa kirefu, aliomba wapewe
 ahirisho fupi ili aweze kuwepo.
Hakimu Mashauri baada ya kusikiliza pande hizo mbili aliiahirisha kesi hiyo hadi Novemba 15, 2018 kwa ajili ya kutajwa.
Mahakama ilipanga  Novemba 21 na 22, mwaka huu kesi hiyo itasikilizwa kwa ushahidi wa mashahidi wa upande wa mashtaka.
Shahidi
 huyo wa nane wa upande wa mashtaka ni Katibu Mkuu wa Shirikisho la 
Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Kidao Mzigama Wilfred (41).
Washtakiwa
 katika kesi hiyo mbali na aliyekuwa rais TFF, Jamal Emil Malinzi(57) 
wengine ni Katibu Mkuu wa TFF, Mwesigwa Joas Selestine(46) na Mhasibu wa
 TFF,  Nsiande Isawayo Mwanga(27).
Meneja
 wa  Ofisi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Miriam 
Zayumba na Karani wa TFF, Flora Rauya ambao kwa pamoja wanakabiliwa na 
mashtaka 30 katika kesi ya jinai namba 213 ya mwaka 2017 yakiwamo ya 
kula njama, kughushi, kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu na 
utakatishaji wa fedha wa Dola za Marekani 173,335 na Sh 43,100,000.
Malinzi,
 Mwesigwa na Nsiande wapo rumande kwa kukabiliwa na mashtaka ya 
utakatishaji wa fedha kuwa miongoni mwa mashtaka  ambayo kwa mujibu wa 
sheria hayana dhamana huku wenzao Zayumba na Frola wapo nje kwa dhamana.






No comments:
Post a Comment