WAZIRI
wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola, amefanya ziara ya kushtukiza
kituo cha Polisi Tabata na Buguruni vya jijini Dar es Salaam ili kujua
kama maagizo yake aliyoyatoa katika vituo mbalimbali kama yameanza
kufanyiwa kazi.
Waziri Lugola alianza ziara yake saa 2:45 jana asubuhi kwa kuibukia katika kituo cha Tabata na moja kwa moja alianza kuulizia mahudhurio ya wafanyakazi wote wa kituo hicho na kujua nani yupo kazini na nani hayupo na kwanini hajafika ofisini hapo kwa muda huo wa asubuhi.
Wakati
alipokua kituoni hapo, pia Lugola alikichukua kitabu cha taarifa za
watuhumiwa wote waliopo mahabusu na baadaye kuelekea katika mahabusu
hiyo akiwahoji watuhumiwa kwa kuwaita kwa majina kujua makosa yao
yaliyoyafanya wawepo kituoni hapo.
Lugola
baada ya kumaliza katika kituo hicho, saa 5:27 alielekea kimyakimya
katika kituo cha Polisi cha Buguruni, na aliwahoji watuhumiwa waliopo
mahabusu katika kituo hicho na kujua makosa mbalimbali yanayowakabili
huku polisi wapepelezi wa tuhuma zao wakiwepo katika tukio hilo.
Akizungumza
mara baada ya kumaliza ziara yake, Lugola alisema, alitoa maagizo
mbalimbali katika ziara zake nchini, hivyo anafuatilia kujua maagizo
yake yameanza kufanyiwa kazi au bado baadhi ya vituo kama wameyapuuza.
“Lengo
la hii ziara yangu ni kuboresha utendaji kazi wa vituo vya polisi
nchini, sijaja kumuadhibu mtu mimi, hivyo msiwe na wasiwasi, bali
kilichonifanya hapa nije nikufuatilia maagizo mbalimbali ambayo
niliyatoa kama kweli mnayafanyia kazi,” alisema Lugola.
Maagizo
aliyoyatoa mwezi miwili iliyopita katika ziara zake mikoa mbalimbali
nchini ni kuhakikisha pikipiki zinaondolewa katika vituo vya polisi,
dhamana zitolewe saa 24 ikiwemo Jumamosi na Jumapili, pamoja na polisi
kutowabambikizia kesi wananchi.
Hata
hivyo, Lugola alivipongeza vituo hivyo vya polisi vilivyopo wilayani
Ilala na pia Kituo Kikuu cha Polisi Dodoma alichokitembelea wiki
iliyopita, kwa kuanza kuyafanyia kazi maagizo yake aliyoyatoa zikiwemo
baadhi ya bodaboda, zimeondolewa vituoni na zilizobaki zina kesi
mahakamani.
“Nilifanya
ziara ya kushtukiza pale Kituo cha Polisi cha Tabata, na pia nimekuja
hapa Buguruni, kwakweli wameaanza kuyafanyia kazi maagizo yangu,
pikipiki zote nilizozikuta zinasababu yakuwepo hapo, na si vinginevyo
kama walivyokua wanaziweka kiholela hapo awali,” alisema Lugola.
Pia
lugola aliwataka Makamanda wa polisi nchini kuwafuatilia askari wao kwa
umakini ili kujua utendaji kazi wao, na pia Waziri huyo alisema atakua
anafanya ziara kama hizo mara kwa mara hivyo vituo vya polisi nchini
viwe sawa muda wote.
“Hamjui
siku wala saa ambapo nitakuja, tufanye kazi, tuwahudumie wananchi,
tusiwaonee wananchi, tujitume kufanya kazi kwa weledi, sitamvumilia mtu
ambaye atavunja utaratibu,” alisema Lugola.
No comments:
Post a Comment