Aliyekuwa
mwanafunzi wa Shule ya Msingi Kisangura wilayani Serengeti, Mkoa wa
Mara, Emmanuel Nyakitare, (15), amefariki baada ya kukatwa mguu kwa
panga na mwanafunzi mwenzake wakiwa wanachunga ng’ombe.
Emmanuel
alifariki wakati akisubiri matokeo ya mtihani wa darasa la saba,
yaliyotangazwa hivi karibuni. Chanzo cha tukio ni kugombania eneo la
kulisha mifugo baada ya mtuhumiwa, Charles Kaheke (13), mwanafunzi wa
darasa la sita katika Shule ya Msingi Kisangura kumkata kwa panga
marehemu kwa kumtuhumu kulisha mifugo eneo lisilo lake.
Ofisa
Tarafa ya Rogoro, Gasper Richard, alisema tukio hilo lilitokea Oktoba
29, mwaka huu, baada ya wanafunzi hao kugombana na baada ya kutenda kosa
hilo mtuhumiwa alikwenda shuleni bila mfuko wa madaftari kama ilivyo
kawaida, mwalimu wake alipomuuliza kwa nini hakuwa na daftari akamjibu
mwalimu kwamba amnunulie ampe.
“Siku
ya tukio marehemu alikwenda kuchunga mifugo yao eneo hilo jirani na
nyumbani kwa akina Kaheke, (mtuhumiwa) ambaye alipotoka shule kuja
kupata chakula cha mchana alimkuta marehemu eneo hilo, katika kuzozana
ndipo mmoja alimkata mwenzake kwa panga na kuvuja damu nyingi,” alisema.
Akielezea
tukio hilo, Mkuu wa Wilaya ya Serengeti, Nurdin Babu, alisema lilitokea
Oktoba 29, mwaka huu, kati ya saa 6 na saa 7 mchana, wakati wanafunzi
hao wakichunga mifugo, ndipo ulipozuka ugomvi kugombania eneo la
malisho, ndipo mtuhumiwa alikasirika na kumkata mguu mwenzake kwa panga,
hivyo kuvuja damu nyingi na kusababisha kifo chake.
“Hata
hivyo, baada ya kuona amesababisha kifo cha mwenzake alitokomea na
kukimbia kwenda kusikojulikana na mpaka sasa haijulikani alipo na
marehemu Nyakitare alikuwa akisubiri matokeo ya darasa la saba mwaka
huu, baada ya kufanya mtihani,” alisema Babu.
Babu,
ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya
Serengeti, alisema baadaye wazazi wa mtuhumiwa walikwenda kwa familia ya
marehemu na kuomba msamaha na kuahidiana mambo ambayo hayakuwekwa wazi,
hivyo kulimaliza suala hilo bila kufika Ofisi ya Mkuu wa Wilaya kwa
hatua zaidi.
No comments:
Post a Comment