MIUNDOMBINU ni muhimu katika maendeleo ya Taifa lolote ambalo linalohitaji kusonga mbele kiuchumi, kijamii kwa sababu husaidia Serikali katika kufanikisha malengo iliyojiwekea.
Miundombinu
hiyo ambayo inalenga kuboresha na kuimarisha uchumi inajumuisha ujenzi
wa miradi mbalimbali ya uchukuzi na usafirishaji kama reli, barabara,
viwanja vya ndege, bandari, ununuzi wa ndege na meli.
Kukosekana kwa miundombinu ya uhakika kunachangia kupanda kwa gharama za maisha kutokana na kuongezeka gharama za uchukuzi.
Katika
kutambua umuhimu wa miundombinu kwenye kukuza uchumi Serikali ya awamu
ya tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Magufuli imeamua kujikita katika
kuboresha miundombinu ikiwemo ujenzi wa reli ili kuhakikisha Taifa
linasonga mbele kiuchumi.
Mradi
huo wa ujenzi wa mfumo wa reli mpya ya kisasa (SGR) unaojengwa na
Serikali kupitia Shirika la Reli Tanzania (TRC), unatekelezwa kwa awamu,
ambapo awamu ya kwanza kati ya Dar es Salaam na Mwanza ina urefu wa km.
1,219.
Jumamosi,
Novemba 3 mwaka huu Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alifanya ziara ya
kutembelea ujenzi wa reli hiyo kuanzia eneo la Shaurimoyo (Dar es
Salaam) hadi Soga (Pwani) ambapo alisema ameridhishwa na kasi na viwango
vya ujenzi huo.
Alisema
kipande cha kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro chenye urefu wa km. 300
kinatarajiwa kukamilika Novemba 2019 na kipande wa cha kutoka Shaurimoyo
hadi eneo la Pugu chenye urefu wa km. 20 ambacho kilipangwa kukamilika
Julai 2019, lakini kwa kasi ya mkandarasi kitakamilika Machi 2019.
“Nimeridhishwa
na kasi ya ujenzi kwa sehemu ulivyofikia pamoja na ushiriki wa
Watanzania wengi katika mradi huu, tunataka muendelee kujenga kwa kasi
hii na kiwango hikihiki. Kazi mnayoifanya inavutia,” alieleza.
Waziri
Mkuu alisema Serikali inataka kuona malengo ya Rais Dkt. Magufuli ya
kutaka kuona SGR inakamilika kwa wakati na kuanza kutumika nchini
yanatimia kwani wananchi nao watakuwa wamerahisishiwa usafiri.
Alisema
kukamilika kwa ujenzi wa reli hiyo kutaimarisha biashara kati ya
Tanzania na nchi jirani hususani ambazo hazijapakana bahari pamoja na
kupunguza muda wa safari katika maeneo ambayo mradi huo unapita.
Pia
itasaidia katika kutunza barabara na kupunguza gharama za ukarabati wa
mara kwa mara kwa sababu mizigo mingi itakuwa inasafirishwa kwa njia ya
reli na maroli yatapungua barabarani, hivyo kuzifanya ziwe imara na
kudumu.
Waziri
Mkuu aliongeza kuwa SGR inakwenda kukuza sekta zingine za kiuchumi
nchini kwa sababu nazo zinategemea uimara wa miundombinu ya usafiri wa
uhakika.
Katika
sekta ya viwanda reli hiyo itasaidia kusafirisha bidhaa zinazozalishwa
kwenye viwanda mbalimbali na kuwafikia watumia kwa wakati na kwa gharama
nafuu.
Akizungumzia
kuhusu suala la ajira katika ujenzi wa mradi wa SGR, Waziri Mkuu
alisema amefarijika kusikia asilimia 96 ya watu walioajiriwa katika
mradi huo ni Watanzania, amewataka wawe mabalozi wazuri.
“Watanzania
mnaofanya kazi katika mradi huu, hakikisheni mnawajibika kwa
kufanyakazi kwa bidii, uadilifu na muwe mabalozi wazuri ili wananchi
wengine waweze kupata ajira kwenye miradi mbalimbali inayoendelea
kutekelezwa nchini ikiwemo ya ujenzi.”
Kwa
upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania (TRC), Masanja
Kadogosa alisema awamu ya kwanza ya mradi huo wa reli kutoka Dar es
Salaam hadi Makutupora unagharimu sh. trilioni 7.1.
Alisema
awamu hiyo ya mradi wa ujenzi wa reli hiyo yenye urefu wa km 1,219
kutoka Dar es Salaam hadi Mwanza umegawanyika katika vipande vitano,
kipande cha kwanza ni kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro chenye urefu km
300 na njia kuu 205 ambazo km 95 zitakuwa zinapisha kitagharimu sh.
trilioni 2.7.
“Kipande
kingine ni kutoka Morogoro hadi Makutupora chenye urefu wa km. 422 na
njia kuu 336 ambazo km 86 zitakuwa zinapishana kitagharimu sh. trilioni
4.4, Makutupora hadi Tabora km. 376.5 chenye njia kuu 294 na km 73.5
zitakuwa zinapishana.
Kipande
kingine ni cha kutoka Tabora hadi Isaka km 162.5 chenye njia kuu 130 na
km 32.5 zitakuwa za kupishana na Isaka hadi Mwanza km. 311.25 njia kuu
249 huku km 62.5 zitakuwa za kupishana.”
Mkurugenzi
huyo alisema kukamilika kwa reli hiyo ya kisasa itachochea mipango ya
Serikali ya awamu ya tano katika kutekeleza sera ya Tanzania ya viwanda
na kulifikisha Taifa kwenye uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025.
Pia
Mkurugenzi huyo alisema reli hiyo itachochea mapinduzi ya kiuchumi kwa
kanda nzima ya Afrika Mashariki na Kati hususan kwa nchi zisizopakana na
bahari kwani watasafirisha mizigo yao kwa haraka na uhakika.
“Kuchangia
katika pato la Taifa na sera ya viwanda kwani mradi huo umeongeza
mahitaji ya saruji, kokoto, nondo pamoja na vifaa vingine vya ujenzi,
hivyo kuvifanya viwanda vyetu vya ndani kupata soko la bidhaa zake.”
Akizungumzia
mradi huo kwa ujumla, Mkurugenzi huyo alisema maendeleo ya mradi huo ni
asilimia 32 kwa kipande cha Dar es Salaam-Morogoro na asilimia 3. 31
kwa kipande cha Morogoro-Makutupora.
Alisema
jumla ya km. 722 za ujenzi wa mradi wa reli ya kisasa kwa sasa
zinatekelezwa katika vipande viwili, kipande cha Dar Es Salaam-Morogoro
km. 300 kinajengwa kwa ubia wa kampuni ya YAPI MERKEZI ya Uturuki na
MOTA-ENGIL ya Ureno na kipande wa Morogoro-Makutupora km. 422 kinajengwa
na kampuni ya YAPI MERKEZI.
Kadogosa
alisema katika mradi huo wa reli za kisasa mfumo wa uendeshaji wa treni
utatumia nishati ya umeme kutoka Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na
tayari taratibu za kumpata mkandarasi za kujenga njia za umeme upo
katika hatia za mwisho.
Kuhusu
ujenzi wa madaraja Kadogosa alisema kazi ya ujenzi wa madaraja na
makaravati unaendelea ambapo daraja refu katikati ya jiji la Dar es
Salaam ina jumla ya urefu wa km. 2.56 na ujenzi wake umefikia asilimia
46.
“Kuna
madaraja ya kati 26 na makaravati 243, madaraja ya treni kupita juu
yapo 17, madaraja ya treni kupita chini yapo 15 na madaraja reli juu ya
reli yapo matano, pia jumla ya stesheni sita zitajengwa kati ya Dar es
Salaam na Morogoro, kati ya hizo kubwa zitakuwa mbili na nne zitakuwa
ndogo.”
Alisema
usanifu wa stesheni hizo umezingatia mazingira na asili ya Tanzania
ambapo stesheni ya Dar es Salaam ina sura ya madini adimu ya Tanzanite
wakati stesheni za kati usanifu wake umezingatia utamaduni na nyumba za
asili na stesheni ya Morogoro itaonesha uhalisia wa milima ya Uruguru.
Kadhalika,
Mkurugenzi huyo alizungumzia kuhusu ajira katika mradi huo ambapo
alisema una jumla ya wafanyakazi 5,440, vibarua 4,743 ambapo jumla ya
asilimia 96 ni Watanzania na asilimia nne ni wageni, wataalamu 189 wa
Kitanzania na 258 wa kigeni kwa uwiano wa asilimia 42 Watanzania na
wageni asilimia 58.
Pia
jumla ya ajira 626 za Watanzania wasio na utaalamu na 19 za wenye
utaalamu zimepatikana kupitia kampuni za wazawa (sub-contractors)
wanaoshiriki moja kwa moja kwenye mradi huo.
Akizungumzia
kuhusu ardhi na mali nyingine, Kadogosa alisema mali za wananchi
wapatao 6,514 zenye thamani ya kiasi cha sh. bilioni 83.099 zitakiwa
kuhamishwa ili kupisha ujenzi wa reli kwa kipande wa Dar es
Salaam-Morogoro.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMANNE, NOVEMBA 6, 2018.
No comments:
Post a Comment