Mkazi
wa Wilaya ya Nkasi mkoani Rukwa, Msema Msafiri maarufu kwa jina la
Giriki (35), ameliwa na mamba, alipokwenda katika mwambao wa Ziwa
Tanganyika kuogelea.
Imeelezwa
kuwa Msafiri, mkazi wa Kitongoji cha Lyela kilichopo mwambao wa Ziwa
Tanganyika katika Kijiji cha Izinga Kata ya Wampembe, alikwenda kuogelea
kutokana na joto kali alilokuwa akilihisi.
Alikumbwa na mkasa huo Ijumaa majira ya mchana, baada ya kuingia ziwani na kuanza kuogelea.
Akizungumzia
tukio hilo, Mwenyekiti wa Kijiji cha Izinga, George Fataki, alisema
kuwa kijana huyo alikuwa ni mgeni katika kitongoji hicho na alikuwa
ametokea mkoani Kigoma katika Kijiji cha Kalago na kwenda katika katika
kitongoji hicho ambacho ni makazi ya wavuvi mwezi mmoja uliopita, kwa
lengo la kufanya shughuli hizo.
Alisema
kwa kuwa mazingira aliyotoka yalikuwa na baridi, hivyo mazingira ya
ziwani yalikuwa yakimsumbua kutokana na joto kali, kitendo
kilichosababisha ajenge mazoea ya kwenda kuogelea ziwani.
Kwa
mujibu wa Fataki, siku ya tukio hilo majira ya saa 8 mchana aliwaaga
wavuvi wenzake kuwa anakwenda kuupoza mwili kwa kuogelea ziwani na
alipofika aliingia ndani ya maji na kuanza kuogelea, ghafla aliibuka
mamba na kumvutia katika kina kirefu cha maji na kuanza kumla kisha
kuondoka naye.
Mwenyekiti
wa kijiji hicho alisema kuwa baadhi ya wavuvi walikuwa wanashuhudia
tukio hilo kwa mbali, lakini walishindwa kutoa msaada, hivyo mamba huyo
kuondoka na Msafiri na mpaka sasa jitihada za kuutafuta mwili wake
zinaendelea.
Kamanda
wa Polisi mkoani Rukwa, George Kyando, alithibitisha kutokea kwa tukio
hilo na kuwatahadharisha wananchi wanaoishi maeneo ya mwambao mwa ziwa
na mito kuacha tabia ya kwenda kuogelea, kwa kuwa ni hatari kwa usalama
wao.
No comments:
Post a Comment