WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ametoa siku mbili kwa Kaimu Afisa Elimu (Msingi) wa wilaya ya Muleba, mkoani Kagera Bw. Bukuru Malembo awe amepeleka walimu wawili katika shule ya msingi iliyoko kwenye kitongoji cha Rwenzige kwa kuwa haina mwalimu hata mmoja.
Shule
hiyo yenye madarasa wawili na ofisi moja ya mwalimu ina jumla wanafunzi
216 wa darasa la awali hadi la nne, ilijengwa na wananchi ambapo
wanafunzi wake wanafundishwa na mwananchi mmoja aliyemua kujitolea ili
kuwapunguzia watoto kutembea umbali wa kilomita 16 kwenda kusoma katika
shule ya kijiji cha Kiteme.
Waziri
Mkuu alitoa agizo hilo jana (Jumatatu, Oktoba 8, 2018) baada ya
wanafunzi wa shule hiyo kuwasilisha malalamiko yao kwa njia ya bango
wakati akizungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika
kwenye kiwanja cha kituo cha afya Kimeya, baada ya kukagua majengo ya
kituo hicho.
“Haiwezekani
watoto wadogo wenye umri wa kuanzia miaka mitano wakatembea umbali wa
kilomita 16 kwenda shule wakati katika kitongoji chao kuna shule yenye
madarasa mawili na chumba kimoja cha ofisi ya mwalimu na Afisa Elimu
hadi sasa hajapeleka walimu na kumuachia mwalimu Benson (kijana ambaye
si mwalimu ila anajitolea kufundisha) akifundisha wanafunzi hao peke
yake.”
Waziri
Mkuu alimuagiza Afisa Elimu huyo ahakikishe ifikapo Jumatano (Oktoba
10, 2018) saa nne asubuhi awe ameshawapeleka walimu hao katika shule
hiyo ya msingi ili waweze kuwafundisha wanafunzi hao na kisha Mkuu wa
wilaya hiyo, Mhandisi Richard Ruyango awasilishe taarifa ya utekelezaji
wa agizo hilo ofisini kwake. “Walimu wengi mmewaacha katika shule za
barabarani huku za vijijini zikiwa hazina walimu.”
Kwa
upande wake, Bw. Benson Bukerebe (29) maarufu mwalimu Benson alisema
yeye kitaaluma si mwalimu bali ni mhitimu wa kidato cha nne, alimua
kuanzisha darasa kwa ajili ya kuwafundisha wanafunzi hao kwani alikuwa
akiwahurumia kwa sababu baadhi yao hawakuwa na uwezo wa kutembea umbali
wa kilomita 16 hadi iliko shule ya msingi ya Kiteme.
Kijana
huyo alisema kwa muda wote huo ameweza kumudu kuwafundisha wanafunzi
hao kwa kutumia vitabu vya kuazima kutoka shule mbalimbali za msingi,
lengo ni kuhakikisha watoto wenye umri wa kuanza shule katika kitongoji
chao wanapata fursa ya elimu ambayo ni haki yao ya msingi.
Katika
hatua nyingine,Waziri Mkuualisema Serikali imeweka sheria kali ili
kuwalinda watoto wa kike na wanatakiwa kuheshimiwa katika jamii kwa
kuachwa waendelee na masomo yao bila ya usumbufu wa aina yoyote na
atakayebainika kukatisha masomo yao atachukulia hatua kali za kisheria.
Alisema
Serikali itatoa adhabu kali ya kifungo cha miaka 30 jela kwa mtu
atakayekatisha elimu ya mtoto wa kike iwe kwa kumuoa, kumpa ujauzo na
hata ukikutwa naye nyumbani kwako na katika nyumba ya wageni.
“Tukikukuta
na binti wa shule katika kona isiyoeleweka tunakukamata na kukuchukulia
hatua za kisheria. Ole wenuvijana, mkibainika mmewapa mimba mabinti
wanaosoma, adhabu yake ni miaka 30 jela.”
Waziri
Mkuu alisema kwa wazazi au walezi watakaowaozesha watoto kike ambao
bado ni wanafunzi na kwa upande wa wazazi watakaomsindikiza mtoto wao wa
kiume kwenda kuoa mwanafunzi wote watachukuliwa hatua za kisheria.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMANNE, OKTOBA 9, 2018.
No comments:
Post a Comment