Mfanyabiashara Hafidhi Jonggradgorn ametiwa hatiani na madini yake yenye thamani ya Dola za Marekani 105,757.38 kutaifishwa na Serikali baada ya kukiri kosa la kukutwa na madini hayo bila leseni.
Mshtakiwa huyo alihukumiwa jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbard Mashauri.
Mahakama
hiyo ilimtia hatiani na kumhukumu kwenda jela miaka miwili au kulipa
faini Sh milioni mbili kwa kosa la kwanza na kosa la pili jela miaka
mitatu au faini Sh milioni tatu.
Kabla
ya hukumu hiyo, Wakili wa Serikali, Jackline Nyantori alimkumbusha
mshtakiwa mashtaka yanayomkabili ambapo alidai anadaiwa kutenda kosa
kati ya Januari 2017 na Juni 3, 2018.
Nyantori
alidai shtaka la kwanza mshtakiwa anadaiwa katika maeneo tofauti
Tanzania na Falme za Kiarabu na India, akiwa si mtumishi wa umma kwa
makusudi alifadhili biashara ya madini kwa lengo la kupata faida.
Nyantori
alidai katika shtaka la pili, mshtakiwa katika tarehe hizo maeneo ya
Mikocheni A, Mtaa wa Chwaku alikutwa na vito vya thamani aina ya
gamestones kilo 62.76 vyenye thamani ya Dola za Marekani 105,757.38.
Mshtakiwa
alikiri makosa hayo na kutiwa hatiani na upande wa mashtaka ulitaka
apewe adhabu kwa mujibu wa sheria kwa sababu mshtakiwa ameingilia
maliasili za taifa.
“Mheshimiwa
Hakimu tunaomba madini yataifishwe yakabidhiwe serikalini chini ya Tume
ya Madini, bastola arejeshewe mshtakiwa,” alisema Nyantori.
Akijitetea
mbele ya hakimu, mshtakiwa huyo aliomba apunguziwe adhabu kwani ana
familia na watoto wameshindwa kwenda shule kwa sababu ya kukosa ada, ni
mfanyabiashara anayeipa Serikali kipato.
Hakimu
Mashauri alisema mshtakiwa mbinu anayotumia inaikosesha Serikali
mapato, hivyo alimuhukumu kwa kosa la kwanza faini Sh milioni mbili au
kwenda jela miaka miwili.
Alisema kosa la pili faini Sh milioni tatu au jela miaka mitatu.
Hata hivyo mshtakiwa hajalipa faini hivyo amekwenda jela.
No comments:
Post a Comment