MAHAKAMA
ya Hakimu Mkazi Kisutu imesema haiwezi kifuta kesi ya utakatishaji wa
fedha inayomkabili Rais wa Klabu ya Simba Evans Aveva na Makamu wake
Godfrey Nyange maarufu Kaburu sababu kesi hiyo imeishafikia hatua ya
usikilizwaji wa awali.
Badala
yake Mahakama kwa mara nyingine, imetoa amri na kuwapa siku 14 upande
wa mashtaka kutekeleza amri iliyoitoa ya kuwataka aidha wafute mashtaka
dhidi ya Zacharia Hanspoppe na mfanyabiashara, Franklin Lauwo au
wabadilishe hati ya mashtaka kwa kuwaondoa washtakiwa hao ili kesi
isikilizwe.
Uamuzi
huo umetolewa leo mahakamani hapo na Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba,
kutokana na ombi la mawakili wa washtakiwa hao wakiongozwa na Nehemia
Nkoko kuiomba mahakama ifute kesi hiyo kwa sababu upande wa mashtaka
wameshindwa kuiendesha.
Akisoma
uamuzi huo hakimu Simba amesema amepitia hoja za pande zote mbili na
ameona kuwa, huu si muda muafaka wa kufuta kesi hiyo kwa sababu tayari
ilikuwa katika hatua ya (PH) na pia ilishatoa amri ambayo bado
haijatekelezwa.Hakimu Simba amesema upande wa mashtaka wanatakiwa
watekeleze amri iliyotolewa Mei 12 mwaka ,2018, kwa hiyo haiwezi kufuta
kesi hiyo, kwa sababu itafuta hadi amri ambayo tayari ilishaitoa na
haijatekelezeka.
"Si
muda mwafaka wa kufuta kesi hii, natoa siku 14 kuanzia kesho kwa upande
wa mashtaka kufanya mabadiliko na kama hawatafanya hivyo, Mahakama
inaweza kuamua vingine itakavyoona inafaa, " amesema Hakimu Simba.Aidha
Hakimu Simba ametaka amri hiyo itekelezeke kwa sababu hawajulikani ni
lini Hansoppe na Lauwo watakamatwa wakati Aveva na Kaburu wapo
mahabusu.
Kesi
hiyo imeahirishwa hadi Oktoba 16 mwaka 2018 kwa ajili ya washtakiwa
kusomewa PH.Awali, Wakili wa utetezi, Nkoko aliomba Mahakama hiyo
iwafutie mashtaka, washtakiwa hao kwa sababu wameshindwa kuiendesha kesi
hiyo.Akijibu hoja hiyo, wakili wa Serikali Mwandamizi, Mutalemwa
Kishenyi akisaidia na Wakili kutoka Takukuru, Leonard Swai, aliiomba
mahakama kutupilia mbali maombi hayo kwa sababu bado wanaifanyia kazi
amri waliyopewa na mahakama ya kumtafuta Hanspope na Lauwo.
Amedai
Septemba 14 mwaka huu, Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Brigedia
Jenerali John Mbungo aliitisha mkutano na waandishi wa habari na kueleza
kuwa wanawatafuta Hanspope na Lauwo jambo ambalo ni moja ya utekelezaji
wa amri iliyotolewa na mahakama.
Katika
kesi hiyo washtakiwa wanakabiliwa na mashtaka 10 likiwemo la kula
njama, matumizi mabaya na kughushi nyaraka ikionyesha Klabu ya Simba
inalipa mkopo wa USD 300,000 kwa Aveva kitu ambacho sio kweli.
No comments:
Post a Comment