Tanzania
ni ya pili kwa Urithi wa Maliasili baada ya Taifa la Brazil la Bara la
Amerika ya Kusini kwa kuwa na vivutio vingi vya Asili.
Hayo
yameelezwa leo wakati wa ufunguzi rasmi wa Tamasha la Urithi Wetu
(Urithi Festival) linalofanyika katika viunga vya Kijiji cha Makumbusho
Jijini Dar-es –Salaam na Mgeni rasmi Mwenyekiti wa Shirikisho la vyama
vya Wadau wa Utalii Tanzania, Bwana Abdukadir Luta Mohamed.
Amesema
kuna vivutio vingi vya urithi wa utamaduni, ukiweka pamoja vivutio vya
utalii wa asili na utamaduni, Tanzania inaweza kuongoza kwa kuwa na
vivutio vingi vya utalii duniani.
Bwana Mohamed amevitaja baadhi ya vivutio hivyo kuwa pamoja na tamaduni, makabila, mila, desturi, vyakula na Malikale.
Awali
akizungumza wakati wa kumkaribisha mgeni rasmi, Mwenyekiti wa Kamati ya
Maandalizi ya Tamasha la Urithi Kitaifa, Profesa Audax Mabula ameeleza
kuwa Tanzania inajivunia kuwa na lugha kuu nne zilizopo Barani Afrika.
Amezitaja
lugha hizo kuwa ni Wabantu ambao inawajumuisha makabila kama vile
Wasukuma, Wajita na Wanyamwezi, Wanailotiki inawajumuisha Wamaasai,
Wakushitiki-inayojumuisha Wairaq,Wambulu, Wakhoisan –inayowajumuisha
Wahadzabe na Wasandawe.
Profesa
Mabula ameeleza kuwa, Kabila la Wasandawe limeanza kupotea lakini ni
imani kuwa kabila hilo litaendelezwa kupitia tamasha la Urithi Wetu.
Mwenyekiti
huyo wa Kamati ya Maandalizi ya Tamasha la Urithi Kitaifa amesema
"Utalii wa Utamaduni utainuliwa kupitia Urithi festival.
Amewaomba
Watanzania kushiriki vema kwenye Tamasha hili na kuvaa mavazi ya
Kitanzania kama vitenge, ngozi, batiki, shuka na mavazi mengine ya asili
katika maadhimisho haya na ya kila Mwezi wa tamasha la Urithi.
"Urithi
festival inatoa fursa kwa watu wote. Tunapenda waje hapa waone ubunifu,
vitu muhimu na mambo ya ubunifu wa kila aina” Amesema Profesa Mabula.
Ameongeza kuwa, Watu tuheshimu Urithi wetu wa Utamaduni ili kuchochea Utalii wa ndani na nje ya Nchi.
Tamasha
hilo limepambwa na vikundi mbalimbali vya ngoma za kiasili, sarakasi,
nyimbo, Wajasiriamali, vyakula vya kiasili ikiwemo nyama choma za
porini kama swala na nyati zilnazouzwa kwa shilingi elfu Nane kwa kilo.
Naye
Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) Mkurugenzi Mkuu wa TAA, Bw.
Richard Mayongela katika kuunga mkono Tamasha la Urithi Wetu,
imekabidhi fulana 100 katika hafla hiyo.
Tamasha
hilo ambalo litakuwa likifanyika kila mwaka, linaandaliwa na Wizara ya
Maliasili na Utalii, na lilizinduliwa rasmi Septemba 15 mwaka huu jijini
Dodoma na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia
Suluhu Hassan likiwa na lengo la kuongeza idadi ya watalii nchini.
Imeelezwa
kuwa, baada ya Tamasha hilo kufungwa rasmi jijini Dar-es-Salaam
litaendelea kufanyika Jijini Arusha kwenye Uwanja wa Sheikh Amri
Abeida Karatu, ambako ni njia kuu ya kuingilia katika Hifadhi ya Bonde
la Ngorongoro na Serengeti kuanzia Oktoba 8 hadi 13.
No comments:
Post a Comment