Ofisa
Uchunguzi Mwandamizi kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa
(Takukuru), Naza Alawi (43), amedai mahakamani kwamba aliyekuwa
Mhasibu Mkuu wa Takukuru, Godfrey Gugai, alifukuzwa kazi baada ya
kukutwa na hatia ya kukosa uaminifu.
Kipato cha mshtakiwa huyo cha mshahara na posho katika kipindi chote cha ajira kilikuwa Sh 334,175,332.05.
Shahidi huyo alidai hayo jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba.
Akingozwa
na Wakili wa Serikali Vitalis Peter, shahidi alidai majukumu yake
kusimamia dawati la mishahara, kuandaa malipo, kulipa kodi mbalimbali na
kutunza kumbukumbu ya daftari la watumishi waliokopa.
“Gugai alianza kazi Juni mwaka 2001 hadi Julai mwaka 2016 utumishi wake ulipokoma baada ya kufukuzwa kwa kukosa uaminifu.
“Alikutwa
na mali ambazo hakuzitolea tamko kwenye tamko la mali, nilipewa
maelekezo na mhasibu ya kuchambua mishahara ya Gugai kuanzia alipoanza
kazi hadi alipofukuzwa, “alidai.
Alawi
alidai mshahara wa Gugai alipoanza kazi Julai mwaka 2001 ulikuwa Sh
152,630, Februari mwaka 2004 ulipanda na kufikia Sh 191,822.15 ,hadi
anafukuzwa kazi mshahara wake ulikuwa Sh 4,417,838.
Anadai
posho za mazingira magumu Julai mwaka 2001, alikuwa analipwa Sh 45,000,
Machi mwaka 2008 alilipwa Sh 341,784 na mpaka anafukuzwa posho hiyo
alikuwa analipwa Sh 1,362,800.
Shahidi
alidai posho ya matibabu alilipwa Sh 150,000 kuanzia Agosti mwaka 2006
hadi Juni mwaka 2003 na posho ya nyumba ilikuwa Sh 92,858.40 Julai 2007
na Mei mwaka 2009 ilipanda na kuwa Sh 142,450.
“Kwa
kipindi chote cha ajira Gugai alilipwa mshahara wa Sh 218,916,859.65,
posho ya mazingira magumu Sh 99,944,099.50, posho ya matibabu Sh
12,450,000 na posho ya nyumba j Sh 2,864,372.90.
“Jumla ya kipato chote cha Gugai katika kipindi chake cha ajira ni Sh 334,175,332.05,”alidai Alawi.
Shahidi
huyo pia alichambua mshahara na posho za mke wa Gugai, Lina Francis,
aliandikia ripoti ambayo alitaka kuitoa mahakamani kama kielelezo.
Wakili wa utetezi, Alex Mgongolwa alipinga kuwasilishwa ripoti hiyo akidai kwamba muhusika hakuwapo mahakamani.
Baada
ya hoja hiyo mahakama iliahirisha kesi hadi leo kwa ajili ya kuendelea
na ushahidi baada ya kujiridhisha kuhusu sheria inasemaje katika
mazingira hayo.
Mbali na Gugai, washtakiwa wengine ni George Makaranga, Leonard Aloys na Yasin Katera.
Katika
kesi ya msingi, Gugai na mwenzake wanakabiliwa na makosa 43, kati ya
hayo 19 ni ya kughushi, 23 ni utakatishaji fedha na moja ni kumiliki
mali zilizozidi kipato halali.
Gugai
anakabiliwa na shitaka la kumiliki mali kinyume na kipato chake, ambako
alitenda kosa hilo kati ya January 2005 na Desemba 2015.
Inadaiwa
akiwa Dar es Salaam kama mwajiriwa wa Takukuru alikuwa akimiliki mali
za zaidi ya Sh bilioni 3.6 ambazo hazilingani na kipato chake cha awali
na cha sasa huku akishindwa kuzitolea maelezo.
No comments:
Post a Comment