Vijana
saba wenye umri kati ya miaka 21 na 24 leo Jumanne Oktoba 2, 2018
wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na
shtaka la kuharibu noti za Sh70,000.
Wakili
wa Serikali, Mwanaamina Kombakono amewasomea mashtaka yao leo, akieleza
kuwa wanakabiliwa na kesi ya jinai namba 299 ya 2018 mbele ya Hakimu
Mkazi Mkuu, Hamza Wanjah.
Kombakono
amewataja washtakiwa hao kuwa ni Vicent Kaduma (24), Rogers Swale (23),
mwanafunzi Doreen Mwenisongole (22), Kelvin Mgeyekwa (23), Elia
Chengula (24), Said Sadiq (21) na Ramadhani Selemani (23) wote wakazi wa
Dar es Salaam maeneo ya Bahari Beach na Kunduchi.
Kombakono
amedai Septemba 16, 2018 jijini Dar es Salaam, bila ya kuwa na mamlaka
washtakiwa hao waliharibu kwa kuzikanyaga noti za Sh 70,000 za Benki Kuu
ya Tanzania (BoT).
Baada ya kusomewa shtaka hilo, washtakiwa wote walikana na upande wa mashtaka ulisema upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika.
Wakili
wa upande wa utetezi, Stoki Joackim anayewatetea washtakiwa wote
aliiomba mahakama iwapatie dhamana wateja wake kwa sababu shtaka
linalowakabili linadhaminika kwa mujibu wa sheria na kwamba dhamana ni
haki ya washtakiwa.
Baada
ya kusikiliza hoja hiyo, Hakimu Wanjah alitoa masharti ya dhamana kwa
washtakiwa kwa kumtaka kila mmoja kuwa na wadhamini wawili wenye barua
na nakala za kitambulisho na kwamba kila mdhamini asaini bondi ya Sh 2
milioni.
Washtakiwa wote walifanikiwa kukamilisha masharti hayo ya dhamana na kuachiwa huru.
Kesi hiyo imeahirishwa hadi Novemba 2, 2018 itakapotajwa tena.
No comments:
Post a Comment