TAKUKURU
Mkoa wa Dodoma jana usiku iliweka mtego na kufanikiwa kumkamata Jacob
Paul Nyangusi ambaye ni Mhadhiri wa Kitivo cha Sayansi ya Jamii katika
Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) kwa kosa la kumtaka mwanafunzi wa mwaka wa
kwanza kingono ili amsaidie katika mitihani ya marudio aliyofanya hivi
karibuni.
Kosa hili ni kinyume na kifungu cha 25 cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na rushwa Na. 11/2007.
Mhadhiri
huyo alikamatwa saa tatu usiku katika eneo la nyumba mia tatu kata ya
Nzuguni jijini Dodoma akiwa chumbani na mwanafunzi huyo.
Awali
TAKUKURU ilipokea taarifa za Mhadhiri huyo kutaka rushwa ya ngono kwa
mwanafunzi wake ambaye jina limehifadhiwa ili amwezeshe kufanya mitihani
ya marudio baada ya kufeli na pia amsaidie wakati wa usahihishaji.
Baada ya kupokea taarifa hizo TAKUKURU ilifanya uchunguzi wa awali na kuandaa mtego uliofanikisha kukamatwa kwake.
TAKUKURU
inaendelea na uchunguzi na mtuhumiwa huyo atafikishwa mahakamani pindi
kibali cha Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) kikitolewa.
TAKUKURU
Mkoa wa Dodoma imekuwa inapokea taarifa za baadhi ya wahadhiri wasio
waadilifu kuwataka wanachuo hasa wa kike kingono ili wawasaidie katika
masomo yao.
Aidha, baadhi wanawafelisha wanafunzi kwa makusudi na baadaye kuwataka rushwa ili warekebishe matokeo yao.
TAKUKURU
inatoa wito kwa wanafunzi wa kike na wananchi wote kwa ujumla kutoa
taarifa za vitendo vya rushwa ya ngono wanapokutana navyo.
No comments:
Post a Comment