Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi amekabidhi taarifa ya uchunguzi wa mgogoro wa kijiji cha Mabwegere na vijiji saba vya wilaya hiyo na mpango wa utekelezaji wake na kuagiza wote waliohusika kupotosha mipaka ya eneo hilo akiwemo Mkurugenzi Msaidizi wa Upimaji na Ramani wa Wizara ya Ardhi kuchukuliwa hatua za kisheria.
Lukuvi
alitoa agizo hilo jana mkoani Morogoro wakati akikabidhi taarifa ya
uchunguzi iliyofanywa na Jaji wa Mahakama Kuu ambaye sasa ni jaji wa
Mahakama ya Rufaa Jacob Mwambegele kwa Mkuu wa mkoa wa Morogoro Dkt
Kebwe Stephen Kebwe kuhusiana na mgogoro wa mipaka ya kijiji cha
Mabwegere na vijiji jirani vya Mambegwa, Mbigiri, Dumila, Matongolo
na Mfulu vilivyopo Wilaya ya Kilosa mkoa wa Morogoro.
"Wote
walioshiriki kwa namna moja ama nyingine katika process yote ambayo kwa
kiasi fulani imeigharimu serikali fedha nyingi na kuipa maumivu
serikali katika suala hilo ni lazima wachukuliwe hatua kali" alisema
Lukuvi.
Taarifa
ya uchunguzi ilibaini chanzo cha mgogoro ni kukosekana ushirikishwaji
wa vijiji jirani katika kuainisha na kuweka mipaka ya kijiji cha
Mabwegere jambo lililosababisha kijiji kiwe na eneo la ukubwa wa hekta
10, 234 kuliko hata kijiji mama cha Mfulu chenye hekta 1,717 jambo
lililothibitishwa na ukweli kwamba mipaka ya kijiji hicho imeingia ndani
ya mipaka ya kata tatu za Mbigiri, Msowero, na Kitete ingawa
kiutawala kijiji cha Mabwegere kinaratibiwa na kata ya Kitete.
Hata
hivyo, Waziri wa Ardhi alisema wizara haijakifuta kijiji cha Mabwegere
bali itaanza kutekeleza mapendekezo ya uchunguzi ya kufuta mipaka ya
kijiji hicho ambapo sasa TAMISEMI kwa kushirikiana na wilaya ya Kilosa
itatakiwa kuanza mchakato wa kuandaa upya mipaka ya vijiji hivyo kwa
njia shirikishi.
Katika
taarifa yake, Jaji Jacob Mwambegere alipendekeza kwa nia ya kuboresha
utendaji kazi, weledi, maadili na umakini na uwezo wa kulinda na
kutunza kumbukumbu katika idara ya Upimaji na Ramani na Ofisi ya
Kamishna wa Ardhi hatua za kinidhamu zichukuliwe ili kuzuia migogoro ya
ardhi.
Kwa
mujibu wa Lukuvi, Wizara ya Ardhi ilikosea katika zoezi la upimaji wa
kijiji cha Mabwegere lakini wilaya ya Kilosa itakuwa na jukumu la kuanza
mchakato upya wa uanzishaji wa kijiji hicho.
Alisema,
kwa kuwa serikali inaelekea katika uchaguzi wa serikali za mitaa
mwakani ni jukumu la Tamisemi kwa kushirikiana na wilaya ya Kilosa
kuhakikisha mipaka inaandaliwa upya kwa ajili ya kuanzishwa kijiji
upya.
Waziri
wa Ardhi alisisitiza kuwa shughuli za binadamu kama vile ufugaji na
kilimo hazihusiani na masuala ya mipaka, hivyo wilaya ya Kilosa pamoja
na kushughulikia suala la mipaka lazima iandae mpango wa matumizi bora
ya ardhi na kuanza kupendekeza maeneo ya ufugaji kwa vijiji vyote saba
na kusisitiza kuwa ni lazima busara itumike katika kushughulikia jambo
hilo.
Kwa
upande wake Naibu Waziri Tamisemi Joseph Kakunda alisema uanzishwaji
kijiji cha Mabwegere haukufuata sheria na kuwataka wataalamu kuacha kuwa
na nidhamu ya woga na kuzingatia kanuni na sheria katika kutekeleza
majukumu yao.
Aidha, amemuelekeza Katibu Mkuu TAMISEMI kuunda timu itakayochunguza mchakato mzima wa kuanzisha kijiji hicho, na kila atakaebainika kuhusika na uanzishaji wa kijiji hicho kinyume na sheria achukuliwe hatua.
Aidha, amemuelekeza Katibu Mkuu TAMISEMI kuunda timu itakayochunguza mchakato mzima wa kuanzisha kijiji hicho, na kila atakaebainika kuhusika na uanzishaji wa kijiji hicho kinyume na sheria achukuliwe hatua.
Naye
naibu Waziri wa Kilimo Merry Mwanjelwa alisisitiza hatua kuchukuliwa
kwa wote waliohusika na kusema katika serikali hii ya awamu ya tano ni
lazima kufufua makaburi kwa minajili ya kubaini wote waliohusika
kuidanganya serikali.
Taarifa
ya uchunguzi wa mgogoro wa mipaka kati ya kijiji cha Mabwegere chenye
jumla ya hekta 10,234 na mifugo takriban 24,146 na vijiji jirani katika
wilaya ya Kilosa àmbao mara kadhaa ulisababisha vifo vya watu tangu
mwaka 2008 lifanyika kwa muda wa siku sitini ambapo uchunguzi wake
ulizingatia uanzishwaji, upimaji, utolewaji hati miliki kwa kijiji cha
Mabwegere, maeneo yenye mgogoro na hatua zilizokwishachukuliwa juu ya
mgogoro huo, uwiano wa ardhi, mifugo na mahitaji mengine ya ardhi
pamoja na vyanzo vingine tofauti vya mgogoro.
Katika
hatua nyingine Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William
Lukuvi akiambatana na Manaibu waziri Tamisemi Joseph Kakunda na Kilimo
Merry Mwanjelwa amekutana na viongozi wa Halmashauri za vijiji hivyo
saba na kuwasomea taarifa ya uchunguzi wa mgogoro wa kijiji cha
Mabwegere na vijiji jirani.
Lukuvi
amewaeleza wananchi hao kuwa ameikubali taarifa nzima ya uchunguzi kwa
kuwa sheria inampa nafasi ya kuikubali au kuikataa taarifa hiyo, hivyo
kuikubali kwake ni mwanzo wa utekelezaji wa mapendekezo ya uchunguzi na
ndiyo maana aliamua kwenda kuwaeleza ukweli wa suala hilo.
Kwa
mujibu wa Waziri wa Ardhi viongozi wa wizara nne za Ardhi, Tamisemi,
Kilimo pamoja na wizara ya Uvuvi na Mifugo walikaa pamoja na na kupanga
mpango wa utekelezaji uchunguzi huo na namna ya kushughulikia mgogoro
baina ya kijiji cha Mabwegere na vijiji jirani.
No comments:
Post a Comment