SERIKALI
inatekeleza Mpango wa Pili wa Maendeleo ya Taifa wa miaka mitano
(2016/17- 2020/21) unaolenga katika kuimarisha ustawi na maendeleo ya
jamii kwa kuongeza upatikanaji wa huduma bora za jamii ikiwemo elimu,
afya na maji.
Ili
kufanikisha malengo hayo, Serikali imeweka utaratibu wa kukusanya
taarifa muhimu za wananchi wake kupitia takwimu mbalimbali ili kuweza
kupanga mipango ya maendeleo.
Taarifa
hizo zinazotolewa katika mfumo wa takwimu ikiwemo hali ya vizazi na
vifo nchini zinalenga katika kuanisha mahitaji halisi ya wananchi ili
kurahisisha uandaaji wa sera na mipango ya maendeleo kulingana na
mahitaji na mazingira yaliyopo
Pamoja
na jitihada hizo inaelezwa kuwa mfumo wa usajili, utambuzi na uwekaji
wa kumbukumbu wa matukio muhimu ya binadamu ikiwemo vizazi, vifo, ndoa,
talaka na hati za uasili wa watoto umekabiliwa na changamoto mbalimbali
kutokana na mifumo ya sheria zilizopo.
Inaelezwa
kuwa matukio mengi yanatokea katika ngazi za vjiji, vitongoji, mitaa na
kata ambapo watendaji na viongozi wa mamlaka husika wanatambua uwepo
wake yameshindwa kuingizwa katika taarifa rasmi kutokana na Sheria za
Serikali za Mitaa kutowapa jukumu la kusajili na kutunza takwimu za
matukio hayo.
Wizara
ya Katiba na Sheria kupitia Wakala wa Usajili, Ufulisi na Udhamini
(RITA) inatekeleza Mkakati wa Taifa wa Usajili wa Matukio Muhimu ya
Binadamu na Takwimu (CRVS) ambao unalenga kuimarisha shughuli za usajili
wa matukio muhimu na upatikanaji wa takwimu muhimu kwa maendeleo ya
nchi.
Kupitia
Mkakati wa CRVS Wizara imedhamiria kukuza na kuendeleza matumizi ya
TEHAMA katika usajili wa vizazi na vifo ambapo tayari imezindua mfumo wa
kielektroniki wa usajili wa vizazi na vifo kwa kuzingatia mahitaji
ambao ulianza kufanya kazi rasmi mwezi Novemba, 2017.
Akiwasilisha
Hotuba ya Makadirio ya Bajeti ya Mapato na Matumizi kwa mwaka 2018/19,
Waziri wa Katiba na Sheria, Prof. Palamagamba Kabudi anasema katika
kipindi cha mwaka 2017/18, jumla ya vizazi 1,593,313, vifo 46,914, ndoa
15,866, talaka 91 na hati 44 za watoto wa kuasili zilisajiliwa nchini.
Anaongeza
kuwa Kupitia mradi huo wananchi wanapata huduma za usajili wa vizazi na
vifo kupitia ofisi za kata, vituo vya afya na hospitali, ambazo kwa
kawaida zipo karibu na wananchi walio wengi, na vyeti vya kuzaliwa na
kifo vinatolewa papo hapo.
“Hii
ni ongezeko la usajili wa vizazi 201,110, vifo 9,038, hati za watoto wa
kuasili 10 na talaka 69 ikilinganishwa na matukio yaliyosajiliwa katika
kipindi kama hicho kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 isipokuwa ndoa ambayo
ni pungufu ya ndoa 1,907” anasema Prof. Kabudi.
Kwa
mujibu wa Prof. Kabudi anasema jumla ya vizazi 929,938 vilisajiliwa na
kupatiwa vyeti vya kuzaliwa kupitia Mpango wa Usajili wa Watoto walio
Chini ya Miaka Mitano na kufanya kiwango hicho kwa Tanzania Bara
kuongezeka kutoka asilimia 13 mwaka 2012 hadi kufikia asilimia 28 mwaka
2017 sawa na ongezeko la vizazi 2,673,806.
Prof.
Kabudi anasema Ongezeko la usajili wa matukio ya vizazi na vifo ni
kielelezo kuwa RITA imejiimarisha katika kusajili matukio muhimu ya
binadamu na kuwataka wananchi kutoa taarifa za matukio hayo katika
mamlaka mbalimbali.
Akifafanua
zaidi Prof. Kabu vizazi 63,550 vimesajiliwa na kupatiwa vyeti vya
kuzaliwa kupitia Mpango wa usajili wa watoto walio shuleni katika Mkoa
wa Njombe.
Prof.
Kabudi anasema kupitia mfumo huo RITA itaweza kubadilishana taarifa na
mifumo mingine ya usajili kama Ofisi ya Taifa ya Takwimu, Mamlaka ya
Vitambulisho vya Taifa, Tume ya Taifa ya Uchaguzi na Idara ya Uhamiaji
kwa ajili ya kuziwezesha taasisi hizo kufanya maamuzi sahihi, kwa wakati
na kwa gharama nafuu.
Anasema
kuwa kufuatia taarifa ya utafiti ya mfumo wa Sheria ya Usajili wa
Matukio Muhimu ya Binadamu iliyoandaliwa na Tume ya Kurekebisha Sheria
Tanzania kwa kushirikiana na RITA, Wizara yake inatarajia kuwasilisha
Bungeni Muswada wa Sheria ya Usajili wa Matukio Muhimu ya Binadamu ili
kuwezesha matukio mengi zaidi kusajiliwa.
“Wizara,
kupitia Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA) pamoja na Tume ya
Kurekebisha Sheria Tanzania, imefanya maandalizi ya awali ya kufanyia
utafiti mfumo wa kisheria wa ufilisi nchini ili kuweka msingi wa
kutungwa upya kwa mfumo wa kisheria wa kuweka mazingira wezeshi ya
kufanya biashara na uwekezaji nchini” anasema Prof Kabudi.
Ili
mfumo wa CRVS uweze kuleta matokeo yaliyokusudiwa, ni wajibu wa taasisi
za umma kuimarisha na kuwa mfumo mmoja wa wa taarifa na mawasiliano
katika utambuzi wa matukio mbalimbali ili kuhakikisha kuwa matukio
yanaleta manufaa kwa wananchi na Taifa katika kupanga na kutekeleza
mipango mbalimbali ya maendeleo.
No comments:
Post a Comment