Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imewahukumu kifungo cha miaka 28 jela kila mmoja wafanyakazi wawili wa Benki ya NMB.
Wafanyakazi
hao, Mtoro Midole na Daudi Kindamba wamehukumiwa jana Jumatatu Oktoba
Mosi, 2018 baada ya kupatikana na hatia katika mashtaka ya wizi,
utakatishaji wa fedha na kuisababishia benki hiyo hasara ya Sh1.03
bilioni.
Hukumu hiyo iliandaliwa na hakimu mkazi mwandamizi, Godfrey Mwambapa na kusomwa na hakimu Mkuu, Wanjah Hamza.
Akisoma
hukumu hiyo, Wanjah chini ya sheria ya kanuni ya adhabu aliamuru
washtakiwa hao mbali na adhabu ya vifungo hivyo pia walipe kiasi cha
hicho cha fedha.
John
Kikoka aliyekuwa miongoni mwa washtakiwa hao, aliachiwa huru baada ya
mashahidi 21 wa upande wa mashtaka katika kesi hiyo ya jinai namba 118
ya 2014, kushindwa kuthibitisha mashtaka dhidi yake.
Hakimu
Wanjah akiisoma hukumu hiyo, alisema washtakiwa Midole na Kindamba
wamekutwa na hatia katika shtaka la wizi ambapo aliwahukumu kifungo cha
miaka mitano jela kila mmoja.
Katika
shtaka la kutengeneza miamala ya uongo, ambalo linamkabili mshtakiwa
Midole pekee, Hakimu Wanjah alisema atatumikia kifungo cha miaka 10
jela.
Katika
mashtaka ya utakatishaji wa fedha, Hakimu Wanjah alisema mshtakiwa
Midole na Kindamba wamekutwa na hatia katika shtaka moja moja, kati ya
mawili mawili yanayowakabili hivyo kila mshtakiwa atalipa faini katika
kosa moja Sh500 milioni hivyo katika mashtaka mawili kila mshtakiwa
anapaswa kulipa Sh1 bilioni ama kutumikia kifungo cha miaka mitano jela.
Hakimu
Wanjah katika shtaka la kusababisha hasara ya Sh1.03 bilioni kwa benki
ya NMB, aliamuru kila mshtakiwa kulipa faini ya Sh5 milioni ama
kutumikia kifungo cha miaka mitano jela.
Awali,
kabla ya Hakimu Wanjah kusoma hukumu hiyo, wakili wa Serikali
mwandamizi Kishenyi Mutalemwa aliieleza mahakama hiyo kuwa hana
kumbukumbu za makosa ya nyuma ya washtakiwa hao.
Wakili
Kishenyi aliiomba mahakama hiyo kutoa adhabu ya kiwango cha juu kwa
washtakiwa hao, katika kila kosa walilotiwa hatiani kama Matakwa ya
sheria yanavyotaka.
Alibainisha
lengo la kuomba adhabu hiyo ni mshtakiwa wa kwanza ambaye ni
mfanyakazi wa benki ya NMB na amekasimiwa na kuaminika kutunza fedha za
wananchi na kwamba kosa la wizi na utakatishaji wa fedha imekuwa ni
tishio kwa uchumi nchini hasa ukizingatia kiwango kikubwa cha fedha
kilichohusika katika kesi hiyo.
Pia, aliiomba mahakama itoe amri kwa washtakiwa hao kurudisha fedha walizoisababishia hasara benki ya NMB.
Hakimu
Wanjah alipowataka washtakiwa hao waongee chochote kabla ya kupewa
adhabu hizo, Midole aliiomba Mahakama iwafikirie kwani wamekaa mahabusu
kwa miaka minne kwa sababu mashtaka yaliyokuwa yakiwakabili ni miongoni
mwa mashtaka yasiyo na dhamana kwa mujibu wa sheria.
Pia, aliiomba mahakama impatie nakala ya mwenendo wa shauri hilo na nakala ya hukumu kwa sababu anakusudia kukata rufaa.
Kindamba
aliomba mahakama iangalie muda waliokaa mahabusu huku akiomba kupatiwa
mwenendo wa shauri hilo na nakala ya hukumu kwa kuwa anakusudia kukata
rufaa.
No comments:
Post a Comment