WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amesema uamuzi wa Serikali ya awamu ya tano wa
kujenga mradi wa kuzalisha umeme kwenye maporomoko ya mto Rufiji,
Stiegler’s Gorge utasaidia sana kudhibiti uharibifu wa mazingira nchini.
Akizungumza
baada ya kutembelea eneo utakapojengwa mradi huo, leo (Alhamisi, Oktoba
4, 2018), Waziri Mkuu amesema umeme utakaotokana na maji, utazalishwa
kwa gharama nafuu na utakuwa wa uhakika zaidi.
Amesema
kwa vile umeme utakaozalishwa katika mradi wa Stiegler’s Gorge utakuwa
wa bei nafuu na hivyo kuwa rafiki kwa wananchi wa kipato cha chini,
utatumika kama nishati mbadala kwa kuni na mkaa ambao umechangia sana
kwenye uharibifu wa mazingira hasa ukataji miti.
Waziri
Mkuu Majaliwa amewaomba viongozi wa Serikali na vyama vya siasa
wawaelimishe Watanzania kuwa mradi wa Stiegler’s Gorge una faida kubwa
kwa Taifa kiuchumi na hauna athari za mazingira na badala yake
utayaboresha.
Amewahakikishia
Watanzania kuwa mradi huo utajengwa na utakamilika katika muda
uliokusudiwa ambao ni miezi 36 kuanzia siku mkandarasi atakapokabidhiwa
kazi hiyo.
Akizungumzia
usalama katika eneo la mradi, Waziri Mkuu amesema viongozi wa mikoa ya
Morogoro na Pwani wahakikishe kwamba wanaweka ulinzi wa kutosha kuanzia
sasa na wakati ujenzi utakapoanza ili kuzuia hujuma na vitendo vya
wizi na udokozi vinavyoweza kuvuruga kasi ya ujenzi wa mradi.
Amesema
vifaa vitakavyoletwa na mkadarasi lazima vilindwe na wajenzi
watakaoshiriki katika ujenzi wa mradi wahakikishiwe usalama wao na mali
zao.
Amewataka
wananchi pia washiriki katika ulinzi kwa kutoa taarifa kwa vyombo vya
dola kuhusu watu wenye mienendo inayoweza kuzorotesha ujenzi wa mradi
huo kwani jukumu la ulinzi si la polisi peke yao.
Kuhusu
ajira kwa vijana wanaotoka katika maeneo yanayozunguka mradi, Waziri
Mkuu amesema utaratibu utawekwa ili vijana wenye sifa wapewe nafasi ya
kushiriki kwenye usaili na ikibidi watafanyiwa mchujo kwenye maeneo
yatakayofikiwa na wengi.
Aliwaasa
wote watakaobahatika kupata ajira ya kushiriki katika ujenzi wa mradi
huo wawe waadilifu na wachapakazi ili kulinda heshima ya vijana wa
Kitanzania na kuwashawishi wajenzi wa mradi kuajiri vijana wengine
zaidi.
Kuhusu
Wizara ambazo zinaguswa na maandalizi ya ujenzi wa miundombinu
inayohitajika katika ujenzi wa mradi wa Stiegler’s Gorge, Waziri Mkuu
ameagiza wizara hizo zishirikiane ili kuhakikisha kwamba kila Wizara
inatimiza majukumu iliyopangiwa kwa wakati.
Wizara
ambazo tayari zimeanza kuweka miundombinu wezeshi kwa mradi huo ni
pamoja na Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano inayosimamia ujenzi
wa barabara na tawi la reli itakayounganisha eneo la mradi na stesheni
ya Fuga katika reli ya TAZARA kazi ambayo imeanza na Waziri Mkuu
wenyewe aliikagua.
Wizara
ya maji nayo tayari imetimiza jukumu lake la kupeka maji katika eneo la
mradi wakati wizara ya nishati imepeleka umeme. Wizara ya Ardhi, Nyumba
na Maendeleo ya Makazi pamoja na Wizara ya Kilimo nazo zipo kwenye eneo
la mradi kutimiza majukumu yote yanayozigusa.
Awali,
Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani aliishukuru Serikali kwa
kukubali kutoa fedha ambazo zimesaidia sana katika ujenzi wa miundombinu
ya maandalizi ya ujenzi wa mradi.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
ALHAMISI, OKTOBA 04, 2018.
No comments:
Post a Comment