Vijana
wanane wa jamii ya wafugaji ya Kimasai (morani) kutoka Kitongoji cha
Oldonyo Lengai, Kijiji cha Loondolwo, Longido mkoani Arusha,
wamenusurika kifo baada ya kujeruhiwa na simba.
Kwa
mujibu wa vijana hao, walikutwa na simba majira ya saa nane alasiri
juzi kisha kushambuliwa wakati wakichimba kisima kutafuta maji ya
kunyweshea mifugo.
"Tulijaribu
kupiga kelele, simba akaanza kutushambulia. Kuona hivyo, wengine wakawa
wanapiga simu kuomba msaada na kila aliyekuwa anakuja kutoa msaada
alishambuliwa," alisema Mibaku Mundesyo (35) mmoja wa manusura hao.
Alisema
walishambuliwa maeneo mbalimbali ya mwili hali iliyosababisha moja wao
kuwahishwa Hospitali ya Rufani ya Seliani ya jijini hapa kwa matibabu
zaidi.
Wengine
walionusurika ni Melubo Sung'are (24) Milya Lemayaka (28), Loning'o
Sung'are (20), Sakaya Osikarari (20), Ng'ahari ole Bainu (30),
Leng'arwua Loda (20) na Laari Olchuda (21).
Kwa mujibu wa jamii ya wafugaji ya Kimaasai, morani wana umri wa miaka kuanzia 18 hadi 40.
Mtaalamu
wa wanyamapori na uwindaji anayemiliki kampuni ya uwindaji ya
Mantheakis Safaris Ltd, Michel Mantheakis, alisema alimfuatilia simba
huyo kuchunguza tukio la kujeruhiwa kwa vijana hao, akabaini kwamba
simba ndiye aliyewashambulia vijana hao.
"Ni kweli simba aliwavamia vijana hao lakini jambo la kushangaza hakuweza kuua mtu zaidi ya kuwajeruhi kwa kucha.
"Nilipomfuatilia
huyo simba, hakuonekana kuwa na jeraha kwani hata tembea yake haikuwa
na shida na kama alirushiwa mkuki haukumpata vyema.
"Nimeshangazwa na tukio hili kwani haijawahi kutokea watu wanane kujeruhiwa na simba bila kuwa kwenye uwindaji,” alisema.
Hata hivyo, aliitaka jamii hiyo wakimwona simba wamwache ili sheria zifuatwe.
Mkuu
wa Wilaya ya Longido, Frank Mwaisumbe, aliyefika katika kitongoji hicho
na kukutana na wananchi, aliwasihi kuacha kuwinda wanyama kinyume cha
sheria.
Alisema wanyamapori huingiza fedha nyingi kijiji hapo kutoka kwa kampuni za uwindaji.
Pia
aliwataka kuwa walinzi wa wanyamapori na akalaani vitendo vya baadhi
yao kuharibu mitego na kamera zilizowekwa na wawekezaji walioingia nao
mikataba.
No comments:
Post a Comment