Serikali
imesema Shirika la Umeme nchini (Tanesco), liendelee kukata umeme kwa
wateja sugu wanaodaiwa malimbikizo ya Ankara zao za hata kama ni taasisi
nyeti za serikali.
Waziri
wa Nishati, Dk. Medard Kalemani ameyasema hayo kutokana na maombi
maalumu yaliyotolewa na Mkuu wa Gereza la Handeni Miraj Katumbili na
Meneja wa Mradi wa Maji wa HTM, Yohana Mgaza, waliotaka umeme usikatwe
katika ofisi zao na wizara wakati zikitafuta ufumbuzi wa kulipa
malimbikizo ya madeni yao.
Mrakibu
Mwandamizi wa jeshi la Magereza SSP Katumbili, alisema mara nyingi
umeme unapokatwa katika gereza hilo wanakuwa na wakati mgumu kutokana na
aina ya watu wanaofungwa kwa makosa mbalimbali, hivyo wangeomba
wasikatiwe.
Kwa
upande wake Mgaza, alisema mradi wao wa maji wa HTM licha ya kukabiliwa
na changamoto mbalimbali, wanakiri kwamba Tanesco wanawadai zaidi ya Sh
milioni 900 ambazo Wizara ya Maji imeanza kulipa lakini wamekuwa
wakikatiwa umeme mara kwa mara.
“Mheshimiwa
Waziri sisi ni wateja wakubwa wa Tanesco, tunawahudumia wananchi kwa
maana tunatoa huduma, ni kweli tunadaiwa zaidi ya Sh milioni 900, wizara
yetu imejitahidi kulipa kiasi cha Sh milioni 500 lakini bado tunakatiwa
umeme wananchi hawapati maji,” amesema Mgaza.
Naye
Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Godwin Gondwe, akichangia suala hilo alisema
anasikitishwa na Ofisi ya Tanesco Mkoa wa Tanga, namna wanavyoshindwa
kukaa pamoja kutafuta suluhisho la kudumu la kutatua tatizo hilo ambalo
kimsingi kwa vile wizara imeanza kulipa linazungumzika.
“Wizara
ilishaanza kuonesha jitihada za kumaliza deni lakini wanakata umeme na
wananchi wanakosa huduma hii muhimu, nimeongea na ofisi ya mkoa kumaliza
tatizo hili, nimelalamika kwenye kikao ch RCC nikitaka wakutane
walimalize, lakini hadi leo Tanesco hawataki kukaa pamoja,” amesema Mkuu
huyo wa Wilaya.
Akifafanua
hilo Dk. Kalemani aliwapongeza kwa kuonesha jitihada za kulipa lakini
akasisitiza madeni hayo lazima yalipwe kwa kuwa Shirika hilo na lenyewe
limekuwa na madeni mbalimbali ya zaidi ya Sh bilioni 700 huku lenyewe
likidai kwa wateja wake kiasi cha Sh bilioni 200.
“Ni
kweli tunajua wananchi wanaumia lakini mnapolipa Ankara hizi inasaidia
kuliwezesha shirika kuwasaidia wananchi kwa kuwasambazia nishati ya
umeme,” amesema Waziri na kumwagiza Meneja wa Tanesco Mkoa wa Tanga,
Julius Sabu, kuwafuata viongozi wa HTM kumaliza suala lao mapema
iwezekanavyo.
No comments:
Post a Comment