Kamishna
wa zamani wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Harry Kitilya na wenzake
wawili wanaokabiliwa na kesi ya kutakatisha fedha wanaendelea kusota
rumande kutokana na upelelezi wa kesi yao kutokamilika.
Mbali
na Kitilya ambaye pia Mwenyekiti wa Kampuni inayoshughulikia Uwekezaji
wa Mitaji na Dhamana (Egma), washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni
aliyekuwa Miss Tanzania (1996), Shose Sinare na Ofisa wa Benki ya
Stanbic, Sioi Solomon.
Kesi
hiyo imetajwa leo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu mbele ya
Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi ambapo upande wa Jamhuri ulidai
upelelezi haujakamilika huku Wakili wa Serikali Mwandamizi, Mutalemwa
Kishenyi akidai kesi hiyo ilipangwa kwa ajili ya kutajwa upelelezi wake
haujakamilika na kwamba wanaelekea ukingoni kukamilisha.
Akijibu Wakili wa utetezi Alex Mgongolwa alihoji ni ukingo gani huo ambao unazungumziwa na upande wa mashtaka.
Hakimu
Shaidi aliutaka upande wa mashtaka kufanya jitihada za kukamilisha
upelelezi wa kesi hiyo ili hatma ya washtakiwa hao ijulikane na
kuahirisha kesi hiyo hadi Novemba 30, mwaka huu na kuutaka upande wa
mashtaka kufanya jitihada kukamilisha upelelezi.
Washtakiwa
hao kwa pamoja wanakabiliwa na mashtaka ya kula njama, kujipatia fedha
kwa njia ya udanganyifu na kutakatisha fedha ambapo Machi 2013 jijini
Dar es Salaam walijipatia Dola za Marekani milioni sita, wakionyesha
kuwa fedha hizo zilikuwa ni malipo ya ada ya uwezeshaji upatikanaji wa
mkopo na zililipwa kupitia Kampuni ya Egma T Ltd.
No comments:
Post a Comment