Mwanafunzi
wa kike (15) aliyekuwa kidato cha kwanza Shule ya Sekondari Nsemlwa,
Manispaa ya Mpanda, mkoani Katavi amenusurika kujiua kwa kujinyonga
baada ya baba yake Bushiri Joseph, kumuwahi akiwa tayari amepanda juu ya
kiti baada ya kulazimishwa kuendelea na masomo.
Mwanafunzi
huyo pamoja mwenzake wa kiume mwenye umri wa miaka 16, anayesoma kidato
cha pili katika shule hiyo, wanadaiwa kuwa watoro sugu na kutishia
kujiua kwa kujinyonga kwa kamba au kunywa sumu iwapo wazazi na walimu
wao wataendelea kuwalazimisha kuendelea na masomo.
Licha
ya kuhojiwa na wazazi na walimu wao, wanafunzi hao hawakuwa tayari
kueleza kinachowasababisha wakatae kuendelea na masomo na badala yake
wamekuwa wakitishia kujiua kama watalazimishwa kurejea shuleni.
Inadaiwa kuwa wazazi wa wanafunzi hao wameshawafikisha kituo cha polisi bila mafanikio, wakiwa na msimamo wao wa kujiua.
Mwalimu
Mkuu wa shule hiyo, Edgar Mwaisunga, aliwaambia waandishi wa habari
kuwa mwanafunzi huyo alifikishwa na baba yake mzazi shuleni hapo
kujiunga na kidato cha kwanza Januari, mwaka huu.
"Baba
yake alikuwa amemnunulia kila kitu alichohitaji binti yake, lakini
miezi miwili baadaye alianza utoro, tukimhoji alikuwa akidai kuwa hataki
kuendelea na masomo...tulidhani kuwa ni mjamzito, lakini alipopimwa
hakuwa na ujauzito,” alisema.
Alisema
walimu walijitahidi kumsihi, lakini msichana huyo alikataa kata kata
kuendelea na masomo...lakini alikuwa haelezi kwanini hataki kuendelea na
masomo, huku akitishia kujiua kama atalazimishwa kuendelea na masomo,"
alisema.
Kwa
mujibu wa Katibu wa Baraza la Kata ya Uwanja wa Ndege, Manispaa ya
Mpanda, Salum Msimani, wanafunzi hao wawili ni miongoni mwa 17 wa Shule
ya Sekondari Kasimba, Manispaa ya Mpanda, waliofikishwa katika Baraza la
Kata na kufunguliwa mashtaka ya utoro shuleni.
"Wanafunzi
hao msichana na mvulana waliokuwa wakisoma katika Shule ya Sekondari
Nsemlwa, wakiwa na wazazi na walezi wao walifikishwa wiki iliyopita
kwenye Baraza la Kata la Uwanja wa Ndege, Manispaa ya Mpanda na kusomewa
mashtaka yao baada ya mkuu wao wa shule na bodi ya shule hiyo
kuwasilisha malalamiko dhidi yao na wazazi wao kwenye baraza hilo,"
alieleza Msimani.
Msimami
alisema wanafunzi hao wakiwa kwenye baraza hilo waliendelea na msimamo
wao wa kukataa kuendelea na masomo, huku wakisisitiza kuwa kama
watalazimishwa kuendelea na masomo watajiua kwa kujinyonga kwa kamba au
kunywa sumu .
Alisema, walipotakiwa kueleza sababu zinazowafanya wakatae kuendelea na masomo hawakuwa tayari kuzieleza.
"Baraza
hili limeshindwa kutoa hukumu dhidi ya wanafunzi hawa wawili na hata
shuleni walikokuwa wanasoma walimu wameinua mikono, pia polisi
wamefikishwa na wazazi wao, lakini imeshindikana wameng'ang'ania msimamo
wao,” alisema na kuongeza:
“Kama
Katibu wa Baraza hili la Kata natarajia kuonana na Hakimu wa Mahakama
ya Wilaya ya Mpanda kwa ushauri wa kisheria," alisisitiza.
Aidha,
alieleza kuwa kamba aliyotaka kujinyongea mwanafunzi wa kike na kiti
alichokuwa amepanda, vipo katika ofisi za baraza hilo.
Baba
mzazi wa mwanafunzi huyo wa kike, Bashir Joseph, amedai kuwa hivi
karibuni alipomlazimisha binti yake kwenda shuleni aligoma na kuingia
chumbani kwake alikokuwa ametundika kamba ya kujinyongea na kumkuta
akiwa amepanda kwenye kiti tayari kwa kujinyonga.
Naye
baba mzazi wa mwanafunzi wa kiume, Sadok Isha, amedai kuwa pamoja
kuchukua hatua mbalimbali za kumfanya kijana wake huyo aendelee na
masomo, lakini imeshindikana baada ya kutishia kujinyonga.
Diwani
wa Kata ya Uwanja wa Ndege, Stephano Asalile, alisema kwa tukio la
wanafunzi hao wawili linaonyesha jinsi ambavyo baadhi ya wazazi wa
wanafunzi wamekuwa wakipewa adhabu kutokana na utoro wa watoto wao,
kumbe tatizo lipo kwa watoto wenyewe.
No comments:
Post a Comment