Sakata
la vifo vya wananchi na polisi mkoani Kigoma vilivyosababishwa na
mgogoro wa ardhi hivi karibuni limeibukia bungeni, ikiwa ni siku chache
baada ya Mbunge wa Kigoma Mjini (ACT-Wazalendo), Zitto Kabwe kukamatwa
na kisha kushtakiwa.
Zitto
alikamatwa wiki iliyopita na kushtakiwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi
Kisutu jijini Dar es Salaam, baada ya mkutano wake na wanahabari
kuzungumzia suala hilo.
Wiki
chache zilizopita, polisi walikiri kutokea kwa mapigano yaliyosababisha
vifo vya watu wawili na askari wawili waliokwenda kwa ajili ya kulinda
amani huko Uvinza.
Jana,
mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Josephine Genzabuke ndiye aliyeliibua
bungeni akihoji ni kwa nini Wakala wa Misitu Tanzania (TFS) wamekuwa
wakiua na kuwatesa wananchi ambao Rais John Magufuli aliwataka kukaa
eneo la Kagerankanda bila ya kuongeza mipaka wakati Serikali
ikiwatafutia maeneo mengine.
Baada
ya majibu ya Serikali kutoka kwa Naibu Waziri wa Malisili na Utalii,
Japhet Hasunga, mbunge Genzabuke alisimama kwa kuuliza swali la nyongeza
lililoonekana kumkera Spika Job Ndugai. Genzabuke alihoji,
“Hawa TFS wanaua watu, wanawakata mikono na kuwatesa, kwa nini wanafanya hivyo wakati Rais aliagiza wasibuguziwe.”
Katika
swali lake la nyongeza, mbunge huyo alihoji kama TFS wanapingana na
agizo la Rais lililotaka wananchi wa maeneo ya Kagerankanda waendelee
kulima bila kuongeza maeneo.
Hata
hivyo, Spika Ndugai alimzuia kuendelea na swali hilo akisema mambo
anayozungumza ni mazito na kumtaka akae chini. Licha ya mbunge huyo
kutaka kuendelea kujenga swali lake, lakini aliitwa mbunge mwingine.
Baadaye
Ndugai alisimama na kutoa ufafanuzi kwa kukemea maswali aliyosema ni
mazito ambayo yalipaswa kupelekwa kwa Waziri Mkuu na si kuulizwa kama ya
nyongeza bungeni.
Baada
ya kipindi cha maswali na majibu, Mbunge wa Mbozi (Chadema), Pascal
Haonga aliomba mwongozo akitaka kuhoji ni kwa nini Spika alimzuia mbunge
huyo kuuliza swali la nyongeza.
Spika alimkatiza akisema jambo hilo alishaliondoa kwenye mjadala, hivyo halikuwa na ulazima tena wa kuulizwa mbele ya Bunge.
Awali,
katika majibu ya swali la msingi, Naibu Waziri Hasunga alikiri kuwa
Rais Magufuli aliagiza ofisi ya mkuu wa Mkoa wa Kigoma kuwapimia
wananchi eneo hilo.
Hasunga
alisema jumla ya hekta 10,012.61 zilitengwa kwa ajili ya kilimo kwa
wananchi wa maeneo hayo na kijiji cha Mvinza kilipewa hekta 2,174,
Kagerankanda 2,496 na eneo lingine la hekta 5,342.61 lilitengwa kwa
ajili ya wananchi wengine.
No comments:
Post a Comment