WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa amewatakabaadhi ya waagizaji wa taulo za kike ambao wanaziuza kwa bei ya juu licha ya kufutwa kwa kodi, waache mara moja na Serikali haitasita kuwafutia leseni zao za uagizaji mara watakapogundulika kutotekeleza maelekezo hayo.
Waziri
 Mkuu ametoa onyo hilo jana (Jumatano, Novemba 7, 2018) wakati akizindua
 mkakati wa Bunge wa masuala ya kijinsia, Bungeni jijini Dodoma. Amesema
 Serikali imeendelea kuchukua hatua mbalimbali kwa lengo la kuhakikisha 
kuwa wanawake wanawekewa mazingira mazuri yatakayowawezesha kupiga hatua
 zaidi.
Amesema
 hatua hizo ni pamoja na kuondoa kodi ya  taulio za kike ili kuwezesha 
wanafunzi wa kike ambao walikuwa wanaacha masomo kutokana na changamoto 
ya kununua taulo za kike kwa ajili ya kujisitiri wakati wa hedhi 
wazipate kwa gharama nafuu.
Waziri
 Mkuu amesema hatua nyingine ni mpango wa Serikali wa kujenga zahanati 
kila kijiji na kituo cha afya katika kila kata kwa lengo la kupunguza 
vifo vya wanawake na watoto vilivyokuwa vinasababishwa na uhaba wa 
huduma za afya ya mama na mtoto. 
Amesema
 mpango huo wa Serikali unatarajiwa kuongeza tija kwa wanawake hususan 
katika kuwapunguzia muda ambao wamekuwa wakiutumia katika kutafuta 
huduma hizo ambazo zilikuwa zinapatikana kutoka umbali mrefu.
“Imethibitika
 kupitia tafiti za kitaifa na kimataifa kwamba uzazi wa mpango huweza 
kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi kwa hadi asilimia 44 na vifo vya 
watoto kwa hadi asilimia 35.
 Pamoja
 na kulinda afya ya mama na mtoto, huduma hizi zinawasaidia wanawake na 
wasichana kupata nafasi za kujiendeleza zaidi pamoja na familia zao na 
kuongeza ushiriki wao katika shughuli za kiuchumi, kijamii, na 
kimaendeleo.”
Hata
 hivyo, Waziri Mkuu amesema Serikali imeendelea kuwahamasisha wanafunzi 
wa kike kusoma masomo ya sayansi sambamba na kuwawekea mazingira 
wezeshi. 
Amesema
 hatua nyingine ni mpango wa Serikali wa kuwasomesha wanawake katika 
ngazi ya uzamili ili waweze kushika nafasi nyingi zaidi za uongozi 
Serikalini na mahali pa kazi. Zoezi hilo linaratibiwa na Idara Kuu ya 
Utumishi.
Katika
 hatua nyingine,Waziri Mkuu amesema mifumo yetu, mila na historia 
vimewafanya wanawake na wasichana wabaki nyuma kwa kujiajiri kwenye 
sekta isiyo rasmi na isiyo na kipato cha uhakika wala maslahi na kubaki 
wakiwa wategemezi kiuchumi. 
Amesema
 hivi karibuni Serikali imeanza  kutekeleza kampeni ya Rais Dkt. John 
Magufuli ya kumtua mama ndoo kichwani. Kampeni hiyo inalenga kuwaondolea
 wananchi hususani wanawake tatizo la upatikanaji wa haraka wa huduma ya
 maji safi na salama. 
Kwa
 upande wake, Spika wa Bunge, Job Ndugai amesema Bunge linaendeshwa kwa 
kuzingatia uwiano wa kijinsia kwa kiwango cha kuridhisha. “Hata 
tunapoteua baadhi ya wabunge kwa ajili ya kutuwakilisha katika mikutano 
mbalimbali huwa tunazingatia uwiano wa kijinsia.
Amesema
 atahakikisha Bunge linaendeleza azma ya Serikali ya kujenga Taifa lenye
 usawa wa kijinsia inatimia, ambapo amewataka mawaziri wanapowasilish 
hotuba za makadirio ya mapato na matumizi ya wizara zao waeleze namna 
walivyotekeleza jambo hilo.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,






No comments:
Post a Comment