January Makamba: Nilitamani Kujiuzulu Ubunge Ili Kulinda Maslahi Mapana ya Wananchi


Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Mazingira, January Makamba amesema kuwa mgogoro wa kiwanda cha Chai cha Mponde ulitaka kumfanya achukuwe uamuzi wa  kujiuzulu nafasi zake zote za uongozi kisiasa na kiserikali.

Hatua hiyo ilitokana na namna ambavyo viongozi wenzake walivyokuwa wamegawanyika katika namna ambavyo usuluhisho wa mgogoro huo ulivyokuwa ukionekana kutaka kuwanyima haki wananchi.

Waziri huyo alizungumza hayo jana Novemba 1 kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika kata ya Mponde wilayani Bumbuli wakati wa ziara ya Waziri Mkuu Majaliwa Kassim Majaliwa hapo juzi.

Alisema alishadhamiria kuachana na nyadhifa zake baada ya kuona viongozi wenzake walitofautiana katika swala hilo wakidhani anamaslai nalo.

“Niliona ni wajibu wangu kusimamia haki za wananchi na maslahi yao hata kama ningetengwa na kunyanyaswa kwani naamini siku zote yule anayesimamia haki Mwenyezi Mungu hawezi kumtupa” alisema Waziri Makamba.

Amesema mgogoro huo ulileta mpasuko kwa viongozi wa ngazi ya mkoa hadi shina lakini imani yake kwa sasa ni kwamba wameelewa alichokuwa akikitetea na sasa wapo pamoja.

“Wananchi na Wakulima wa chai wameumua wamenyanyasika sana, wamedhulimiwa lakini siasa ninaimani kwa mikakati ya serikali sasa uchumi utaimarika” alisema Waziri huyo.

Hata hivyo aliiomba serikali kuwasaidia wakulima kufufua zao hilo kwa kuwapatia miche bora, pembejeo za kilimo ili kufufua zao hilo.

Katika hatua nyingine Waziri Mkuu Majaliwa Kassim Majaliwa alisema kuwa serikali imekichukuwa kiwanda hicho na sasa wapo kwenye maandalizi ya kukifufua upya.

Alisema kwa sasa wanafanya uhakiki wa madeni yote pamoja na ukaguzi wa mashine na mitambo katika kiwanda hicho ili kujiridhisha kabla hakijaanza kufanyakazi tena.

Alisema tayari deni la kiwanda ni sh Bil 4.4 na kwa sasa anataka afahamu madeni yote mpaka ya wafanyakazi wa kiwanda hicho ili baada ya hapo wajipange kwa ajili ya ulipaji wa  madeni hayo ili kiwanda kianze upya.

Katika hatua hiyo Waziri Mkuu amemuagiza meneja wa kiwanda hicho, Stephen Wahome kuhakiki idadi ya wafanyakazi waliokuwepo awali kiwandani hapo kujua madai yao ya pamoja na idadi ya vifaa vilivyokuwepo kiwandani hapo.

“Watu wote waliokuwa wakidai kiwanda hiki serikali italipa madeni yao wakati tukiendelea na jitihada za kukifufua kiwanda hiki kiweze kurudi katika hali yake ya uzalishani na wananchi waweze kunufaika” alisema Waziri huyo.

Waziri Majaliwa alisema kuwa mgogoro wa kiwanda hicho ulianza Mara baada ya wakulima kuanzisha Umoja wa wakulima wa chai UTEGA na kuusajili kama Shirika la kijamii NGOs badala ya chama cha ushirika.

Alisema kuwa chama hicho kiliwabagua wakulima na kutoa upendeleo kwa baadhi ya wakulima hali iliyosababisha mgogoro huo.

Alisema kuwa mgogoro ulikuwa zaidi baada ya viongozi wa UTEGA nao kugeukana na kuuza kiwanda kwa mwekezaji bila ya kutoa taarifa kwa wakulima wala wanachama wao.

Hivyo kutokana na kasoro hizo huku maslahi ya mkulima yakiwa madogo ndipo serikali ilipoamua kuchukuwa kiwanda chake ili iweze kukiendesha mwenyewe kwa maslahi ya wakulima na wananchi.
Share:

No comments:

Post a Comment

IDADI YA WASOMAJI

TUSIKILIZE LIVE KUPITIA TUNEIN

UNGANA NASI FACEBOOK HAPA

10 ZILIZOSOMWA ZAIDI

Labels

Blog Archive