Baraza
la Usimamizi wa Mazingira nchini (NEMC), limekifungia kiwanda cha
kusindika nyama ya punda kilichopo kwenye Jiji la Dodoma, baada ya
ukaidi wa muda mrefu wa mmiliki kufuata taratibu sahihi za uhifadhi wa
mazingira.
Barua
iliyoandikwa na Kaimu Mkurugenzi wa NEMC, Dk. Vedast Makota, imeeleza
kwamba, kiwanda hicho ambacho kinashughulika na uchinjaji na
usafirishaji wa nyama ya punda nje ya nchi, kwa muda mrefu sasa
kimeonyesha kushindwa kuzingatia taratibu za uhifadhi wa mazingira,
licha ya onyo na ukumbusho kadhaa uliofanywa na baraza.
“Kufuatia
mlolongo huu wa uchafuzi wa mazingira, ambao umekuwa ni kero kwa
majirani na ambao unaleta mashaka kwenye ubora wa bidhaa, Baraza
limefikia hatua ambayo linakosa cha kushauri zaidi ya kufunga kiwanda,”
imeeleza barua hiyo.
Kwenye
maelezo ya ufungaji wa kiwanda hicho, Dk. Makota alisema: “Kwa mamlaka
yaliyokabidhiwa kwa Baraza chini ya Kifungu cha 196(2) cha Sheria ya
Usimamizi wa Mazingira ya mwaka 2004, unaamuriwa kusimamisha shughuli
zote za uzalishaji kuanzia siku ya agizo hili mpaka utakapochukua hatua
kikamilifu za kutekeleza maagizo yote uliyopewa hapo awali,” ilieleza
barua hiyo
Kiwanda
hicho ambacho kinamilikiwa na kampuni inayofahamika kama Huwachen
Company Limited, kimekuwa kwenye mvutano wa muda mrefu na Baraza pamoja
na Wizara inayohusika na uhifadhi wa mazingira tangu Mei, mwaka huu,
ambapo aliyekuwa Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na
Mazingira), Kangi Lugola, alitembelea na kueleza kutoridhishwa kwake na
hali ya uhifadhi wa mazingira.
Ziara
hiyo ya Naibu Waziri ilitokana na ukaguzi wa NEMC uliofanywa Agosti,
mwaka huu kwa lengo la kutathmini hali ya uhifadhi wa mazingira kwenye
kiwanda hicho kutokana na shughuli zake. Katika tathmini hiyo, suala la
uchafuzi wa mazingira liliendelea kuonekana kuwepo.
Mambo
yaliyoonekana kuwa ni tatizo ni pamoja na mabaki ya damu kwenye eneo
hilo ambayo yalipelekea uwepo wa nzi wengi, kuziba kwa mitaro ya
kupitisha maji machafu, kukosekana kwa utaratibu madhubuti wa kuhifadhi
mbolea, kiwango duni cha shimo la kuhifadhia uchafu, harufu mbaya na
ukosekanaji wa mpango endelevu.
Mapungufu
hayo kwa mujibu wa taarifa hiyo ya Mkurugenzi wa NEMC yanakiuka vifungu
kadhaa vya sheria ya mazingira ya mwaka 2004, hii ni pamoja na kifungu
cha 106 (1) (2) na (6) pamoja na kifungu cha 187 (1) (b) na (C).
No comments:
Post a Comment