Serikali
imepiga marufuku Watumishi wa Umma waliohamia Makao Makuu ya Nchi
Dodoma kwa gharama za Serikali kuomba uhamisho wa kurejea jijini Dar es
Salaam.
Hayo
yamesemwa jana na Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi
wa Umma, Dkt. Laurean Ndumbaro alipokuwa akifanya mahojiano maalum na
Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) kuhusiana na zoezi zima la uhamisho
wa watumishi wa umma kutoka Dar es Salaam kwenda Dodoma.
Dkt.
Ndumbaro amesema kuwa, Ofisi yake imekuwa ikipokea barua mbili au tatu
kwa siku za watumishi waliohamia Dodoma kuomba uhamisho wa kurejea Dar
es Salaam kutokana na sababu mbalimbali ikiwa ni pamoja na za kiafya
wakati hospitali ya Rufaa ya Benjamin Mkapa ina vifaa vya kisasa na
uwezo mkubwa wa kutoa huduma za matibabu kwa watumishi hao.
Dkt.
Ndumbaro amefafanua kwamba, kabla ya watumishi kuhamia Dodoma,
Serikali ilitoa maelekezo kwa waajiri kuwasilisha orodha ya watumishi
wenye matatizo ya kimsingi ili wabaki kwenye vituo vya kazi vilivyopo
Dar es Salaam wakiendelea kutekeleza majukumu yao.
Dkt.
Ndumbaro ameongeza kuwa, baadhi ya watumishi waliohamia Dodoma,
wamegeuza uhamisho huo kuwa mradi wa kuwaingizia kipato kwani mara
baada ya kuripoti Dodoma, ndani ya kipindi kifupi wanaomba uhamisho wa
kurejea Dar es Salaam.
Dkt.
Ndumbaro amesisitiza kuwa, kutokana na suala hilo, Serikali imetoa
Waraka wa Barua wenye Kumb. Na. CAC 228/257/01/A/53 wa tarehe 25
Septemba, 2018 kuhusu Uhamisho wa Watumishi Waliohamia Dodoma Kutekeleza
Uamuzi wa Serikali Kuhamishia Makao Makuu ya Nchi Dodoma ambao unazuia
mtumishi aliyehamishiwa Dodoma kwa gharama za Serikali kuomba uhamisho
wa kurejea Dar es Salaam mpaka atimize miaka mitatu katika kituo cha
Dodoma.
Watumishi
wa Umma kuhamia Dodoma ni utekelezaji wa agizo la Serikali lililotolewa
na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe
Magufuli tarehe 25 Julai, 2016 wakati wa maadhimisho ya Kumbukumbu ya
Siku ya Mashujaa.
No comments:
Post a Comment