Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano Ameitaka Mamlaka Ya Bandari Tanzania Kusitisha Mpango Wake Wa Kurasimisha Bandari Bubu

Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Atashasta Nditiye ameitaka Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) kusitisha mpango wake wa kurasimisha bandari bubu zilizopo mkoa wa Dar es Salaam

Hayo yameelezwa na Nditiye wakati wa ziara yake Wilayani Bagamoyo ya kukagua bandari bubu zilizopo ambapo amebaini uwepo wa bandari bubu zaidi ya kumi na tisa zinazosafirisha bidhaa  kwenye eneo la mwambao wa bahari lililopo wilayani Bagamoyo. 
Amesema kuwa uwepo wa bandari bubu hizo ni kipenyo cha baadhi ya wafanyabiashara kukwepa kulipa kodi kwa kutumia bandari rasmi na hivyo kupunguza mapato ya Serikali na kuihujumu nchi kwa kufifisha jitihada za Serikali za kufikia uchumi wa kati na azma yake ya ujenzi wa viwanda, utoaji wa huduma za afya, elimu, maji, umeme na ujenzi wa miudombinu ya sehemu mbali mbali nchini

Nditiye ameielekeza TPA iache mara moja mpango huo wa kurasimisha bandari bubu zilizopo Mbweni na Temeke kwa kuwa Dar es Salaam ipo bandari na itumike hiyo kwa shughuli za usafirishaji wa bidhaa na abiria. 
“TPA wafute mara moja mpango wao wa kurasimisha bandari bubu za Mbweni, Temeke kuwa bandari rasmi wakati kuna bandari ya Dar es Salaam,” amesema Nditiye. 
Pia, ameongeza kuwa fedha zilizotengwa na TPA kwa ajili ya mpango huo lipewe jeshi la bandari ili waweze kununua vifaa kwa ajili ya kufanya doria ya kuimarisha ulinzi kwenye mwambao wa bandari

Amefafanua kuwa yapo majahazi yanayofanya shughuli za usafirishaji ufukweni mwa bahari ya Hindi kwenye mwambao upatao kilomita 300 kwenye eneo la Bagamoyo ambapo majahazi yanashusha mizigo kinyemela. 
“Nimeshuhudia taratibu za nchi zikikiukwa na kamati ya ulinzi na usalama ya Wilaya ya Bagamoyo inapata changamoto ila inawadhibiti kwa namna moja au nyingine japo yapo majahazi yanayoshusha bidhaa na kuficha kwenye misitu iliyopo ndani ya bahari,” amesema Nditiye.

Pia ameielekeza Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Majini (TASAC) kufanya utaratibu wa kusajili majahazi yasiyozidi ishirini kwenye eneo la Bagamoyo ili yaweze kuwahudumia wananchi wa Bagamoyo na wengine wote watumie bandari Dar es Salaam. 
“Yapo baadhi ya majahazi yamesajiliwa ila mengine yanafanya shughuli zake kinyemela na yanaenda sehemu mbali mbali na baadhi yao wasio waaminifu wanatumia vibaya vibali vyao na wanashusha mizigo baina ya saa tano na saa tisa usiku,” amesema Nditiye. 
Amefafanua kuwa majahazi haya yanakiuka taratibu za nchi kwa kuwawezesha wafanyabiashara kukwepa kodi na hivyo kupunguza mapato ya Serikali na jitihada za Serikali za kufikia uchumi wa wakati

Naye Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo, Zainabu Kawawa amekiri uwepo wa bandari bubu zaidi ya 19 na amemweleza Nditiye kuwa wilaya hiyo inakabiliwa na changamoto za uwepo wa bandari bubu ambazo zinatumia usafiri wa majahazi kuvusha bidhaa mbali ili kukwepa ushuru wa mamlaka mbali mbali kwa mujibu wa sheria za taasisi husika ambapo wanavusha sukari, mafuta ya kula, matairi ya magari, maziwa ya unga, vitenge, khanga, vipodozi na wahamiaji haramu ambapo hadi sasa kuna wafungwa wapatao 203 waliopo gerezani kutokana na uwepo wa wahamiaji haramu.

Kawawa amefafanua kuwa majahazi hayo yanashusha mizigo nyakati za usiku wakiwa ndani ya bahari mara nyingine bila kufika ufukweni kwa kufaulisha na kupakia kwenye mitumbwi ijulikanayo kwa jina maarufu la ngwanda ili iweze kufikishwa nchi kavu kwa ajili ya kusambazwa kwenye maeneo mbali mbali ili kukwepa kodi. 
Amesema kuwa kamati ya ulinzi na usalama imekuwa ikifanya doria kwenye maeneo hayo ili kudhibiti jambo hilo japo wanakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa vifaa vya kufanya doria baharini na uwepo wa baadhi ya watumishi wa umma wachache wasio waaminifu ambao wanashirikiana na wafanyabiashara kuihujumu Serikali  kwa kutumia bandari bubu zinazotokana na uwepo wa bahari ya Hindi wilayani humo ambapo bandari bubu hizo ni pamoja na bandari bubu ya Mlingotini, Kasiki, Kaole, Magambani, Kilimani, Badeco, Msalabani, Nunge, Mtailindi, Jicho Kuu, Mto Ruvu, Razaba, Gama, Kayanjo – shamba la chumvi, Saadani, Kitongoji cha Gwaza, Changwahela na Duza
Share:

No comments:

Post a Comment

IDADI YA WASOMAJI

TUSIKILIZE LIVE KUPITIA TUNEIN

UNGANA NASI FACEBOOK HAPA

10 ZILIZOSOMWA ZAIDI

Labels

Blog Archive