Waziri
wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt. Harrison Mwakyembe
amebainisha kuwa lugha ya Kiswahili inatarajiwa kuwa lugha kuu ya
mawasiliano katika bara la Afrika ifikapo mwaka 2063.
Waziri
Mwakyembe ameyasema hayo jana Jijini Dar es Salaam wakati akizungumza
na waandishi wa habari kuhusu maadhimisho ya Kampeni Ya Uzalendo na
Utaifa kwa mwaka 2018 yanayotarajiwa kufanyika Desemba 8 Jijini Dodoma
ambapo mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Rais John Pombe Magufuli.
Alisema
kuwa kampeni hiyo kwa mwaka huu imejikita katika kuhamasisha matumizi
ya lugha ya Kiswahili ambayo ni kielelezo kikubwa cha utashi na uhai wa
taifa la Tanzania na inakua kwa kasi sana barani Afrika na duniani kote
kwa ujumla.
“Sasa
hivi Kiswahili ni lugha ya kumi kati ya lugha elfu 6 zinazoongelewa na
watu wengi duniani na kwa mujibu wa Tafiti za Umoja wa Afrika zinaonesha
kuwa ifikapo mwaka 2063 Kiswahili kitakuwa lugha kuu ya mawasiliano
katika bara la Afrika na utambulisho wa mtu mweusi duniani,” alisema
Mwakyembe.
Alieleza
kuwa dunia yote inatambua kwamba Tanzania ndio chimbuko la lugha adhimu
ya Kiswahili hivyo watanzania wanapaswa kujivunia lugha hiyo na
kuitangaza kwa kuwa ni sehemu ya utamaduni wa taifa na msingi wa
uzalendo na utaifa.
Waziri
Mwakyembe alibainisha kuwa kampeni hiyo mwaka huu imejikita katika
kuhamasisha matumizi ya lugha ya Kiswahili ili kuwasisitiza watanzania
kuthamini lugha yao na utamaduni wao na kurejea kwenye misingi ya
maadili ya taifa lao.
Alisema
kuwa sasahivi kuna changamoto kubwa ya mmomonyoko wa maadili
inayosababishwa na baadhi ya watu hasa vijana kuiga tamaduni za nje
kutokana na utandawazi hivyo kupelekea kudharau utamaduni wao ikiwemo
lugha ya Kiswahili jambo ambalo lisipochukuliwa hatua madhubuti litaleta
athari kwa jamii.
Pia
Waziri Mwakyembe alitoa pongezi kwa Rais John Pombe Magufuli kwa
mchango wake mkubwa anaoonesha katika kutumia, kukuza na kuitangaza
lugha ya Kiswahili ndani na nje ya nchi hivyo amekuwa ni mfano wa
kuigwa.
Aidha
alitoa rai kwa watanzania wote na wadau mbalimbali kuunga mkono kampeni
hiyo kwa hali na mali ili Tanzania iweze kufanikiwa kulinda misingi ya
utamaduni na utaifa hususan lugha ya Kiswahili.
Kampeni
ya Uzalendo na Utaifa ilianza rasmi mwaka jana 2017 na itakuwa
ikiadhimishwa kila mwaka ambapo kwa mwaka huu kauli mbiu yake ni
‘Kiswahili Uhai Wetu, Utashi Wetu’.
No comments:
Post a Comment