WAZIRI
wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola amewataka wananchi wa Kakonko
wanaolima jirani na Kambi ya Wakimbizi ya Mtendeli, pamoja na kambi
zingine zote zilizopo mkoani Kigoma waendelee kulima bila kuomba kibali
chochote kama ilivyoagizwa awali.
Waziri
Lugola amefuta utaratibu huo wa utoaji wa vibali kwa ajili ya
kuruhusiwa kwenda kulima katika maeneo hayo, baada ya wananchi wilayani
humo kuulalamikia utaratibu huo ambao walisema unawafanya wasiwe huru na
unawachelewesha kuendeleza shughuli zao za kilimo kama ilivyokua awali.
Akizungumza
katika mkutano wa hadhara uliohudhuriwa na mamia ya wananchi mjini
Kakonko, Mkoani Kigoma, jana, Lugola alisema Serikali ya Awamu ya Tano
haitaki wananchi wake wanyanyaswe, wananchi wanapaswa kua huru katika
nchi yao.
“Naagizia
huu utaratibu ufutwe na wananchi wawe huru kwenda kulima katika maeneo
ambayo yapo jirani na hiyo kambi pamoja na kambi zinginezo, na pia
wasisumbuliwe na mtu yeyote, ” alisema Lugola.
Pia
Waziri Lugola alielekeza baadhi ya wananchi ambao hawajalipwa fidia
wakati mashamba yao yalipochukuliwa kwa ajili ya kuanzisha kambi hiyo
wafanyiwe uhakiki ili waweze kulipwa haki zao.
Hata
hivyo, Mratibu wa Idara ya Wakimbizi Kanda ya Kigoma, Tony Laiser
ambaye alikuwepo katika mkutano huo alipokea maagizo hiyo na kuahidi
kuyatekeleza.
Aidha,
kabla ya mkutano huo wa hadhara, Waziri Lugola alizungumza na
watendaji waliopo katika wizara yake mkoani humo na alisema Serikali
imepeleka mafunzoni vijana 1,500 kwaajili ya kujiunga na Jeshi la polisi
pamoja na kuagiza magari kwa ajili doria.
Pia
aliwataka watendaji hao kufanya kazi kwa bidii kwani serikali yao ipo
na inawajali na pia itahakikisha inatatua kero zao ambazo zinawakabili
ikiwemo ukosefu wa majengo, upungufu wa vitendea kazi na uhaba wa askari
katika sehemu mbalimbali nchini.
No comments:
Post a Comment