Mahakama
ya Wilaya ya Mpanda mkoani Katavi, imemhukumu Ramadhani Shaban (24),
Mkazi wa Mtaa wa Majengo B, kifungo cha miaka 30 jela, baada ya kumtia
hatiani kwa kosa la kumbaka mtoto mwenye umri wa miaka 15, bubu ambaye
pia ana upungufu wa akili.
Hukumu hiyo ilitolewa jana na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa mahakama hiyo, Gosper Luoga, baada ya mshtakiwa kukiri kosa.
Awali,
Mwendesha Mashtaka wa Serikali wa Mkoa wa Katavi, Flaviana Shio, alidai
mahakamani hapo kuwa mshtakiwa alitenda kosa hilo Septemba 9, mwaka huu
majira ya saa 12 jioni katika Mtaa wa Majengo B.
Alidai
kuwa siku ya tukio mshtakiwa alikwenda maeneo ya Mtaa wa Mjimwema
alikokuwa akiishi mtoto huyo na mjomba wake, Ernest Chambala na kumpakia
kwenye baiskeli yake.
Alisema alikwenda naye hadi kwenye chumba chake alichokuwa amepanga na kumbaka.
Aliendelea
kuiambia mahakama kuwa baada ya tukio hilo mtoto huyo alitoka nje na
kuanza kuwaonyesha watu kwa ishara kuwa amebakwa.
Mjomba
wa mtoto huyo alianza jitihada za kumsaka mbakaji huyo kwa kumchukua
mpwa wake huyo ambaye alimwongoza hadi kwenye nyumba alikofanyiwa unyama
huo.
Alieleza
kuwa majirani wa nyumba hiyo walipoulizwa kama walimuona mtoto huyo
akiingizwa kwenye chumba cha mshtakiwa walikiri kumuona.
Baada
ya kukamatwa alichukuliwa na kupelekwa kituo cha polisi na katika
maelezo yake alikiri kutenda kosa hilo na taarifa za daktari
zilithibitisha kuwa mtoto huyo alikuwa ameingiliwa na mwanaume kwa kuwa
sehemu zake za siri zilikuwa na mbegu za kiume.
Mshtakiwa alikiri kutenda kosa hilo kwa kile alichodai amekuwa akifanya naye mapenzi mara kwa mara kwa sababu ni mpenzi wake.
Katika
utetezi wake, mshtakiwa aliiomba mahakama impunguzie adhabu kwa kuwa
mama yake mzazi anamtegemea na baba yake alishafariki.
Hakimu
Luoga baada ya kusikiliza utetezi huo aliiambia mahakama kuwa mshtakiwa
amepatikana na hatia imemhukumu kwenda kutumikia jela miaka 30.
Alisema katika hukumu hiyo mahakama pia imezingatia ongezeko la matukio ya ubakaji wilayani humo.
No comments:
Post a Comment