Rais
John Magufuli ameagiza wafiwa wote waliopoteza ndugu zao kwenye ajali
ya kivuko cha Mv Nyerere kupata Sh 1 milioni baada ya awali kupewa Sh
500,000 kila mmoja.
Hata hivyo watu 41 walionusurika kwenye ajali hiyo nao watapewa Sh1 milioni kila mmoja.
Fedha hizo zinatokana na michango ya kampuni, watu na taasisi mbalimbali wanaoendelea kujitokeza kuchangia waathirika hao.
Awali,
familia za waliopoteza maisha kwenye ajali hiyo iliyotokea Alhamisi
iliyopita walipewa Sh500,000 kwa kila mtu aliyefariki, fedha ambazo
zimepatikana kutokana na michango ya Watanzania, kampuni na taasisi
mbalimbali.
Akizungumza
na vyombo vya habari jana kisiwani Ukara wilayani Ukerewe, Waziri wa
Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Isaac Kamwelwe alisema leo wataanza
kutoa fedha hizo kama walivyoagizwa na Rais Magufuli kwa familia za
marehemu na wote walionusurika.
“Rais
ameniagiza niwaambie kwamba fedha kwa waliopoteza ndugu zao na wale 41
walionusurika, sasa watapata Sh1 milioni kila mmoja. Kuanzia kesho (leo)
tutaanza kutoa fedha hizo, wapeni taarifa,” alisema Kamwelwe.
Alisema
kiwango cha fedha kilichokusanywa mpaka jana jioni ni Sh397 milioni
ambazo zimetolewa na watu na taasisi mbalimbali. Alisema Rais Magufuli
amesema fedha hizo ni za wananchi walioathirika na ajali hiyo.
Waziri
huyo alisema mpaka kufikia jana jioni, miili miwili ya watoto
ilipatikana wakati kazi ya kukiinua kivuko hicho ikiendelea na kufanya
idadi ya waliopoteza maisha kwenye ajali hiyo kufikia 226.
Kuhusu
kurudisha hali ya usafiri katika kisiwa hicho, Kamwelwe alisema leo au
kesho kitapelekwa kivuko kingine kinachoitwa Mv Temesa ambacho kiko
Mwanza kwa ajili ya kutoa huduma wakati shughuli ya kukiinua kivuko cha
Mv Nyerere ikiendelea.
No comments:
Post a Comment