Wizara
ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki imeendelea kupokea
salamu za rambirambi kutoka kwa marais, mawaziri wakuu wa mataifa
mbalimbali duniani kwenda kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, kufuatia ajali ya kuzama kwa
kivuko cha MV Nyerere iliyotokea kwenye Ziwa Victoria, Mkoani Mwanza
tarehe 20 Septemba, 2018 na kusababisha vifo, majeruhi na upotevu wa
mali.
Baadhi
ya salamu zilizopokelewa ni pamoja na kutoka kwa Rais wa Kenya,
Mheshimiwa Uhuru Kenyatta, Rais wa Urusi, Mheshimiwa Vladmir Putin, Rais
wa China, Mheshimiwa Xi Jinping, Rais wa Ujerumani, Mheshimiwa
Frank-Walter Steinmeier, Rais wa Saharawi, Mheshimiwa Brahim Ghali,
Mtawala wa Kuwait, Mtukufu Sheikh Sabah Al-Ahmad al Jaber Al-Sabah, Baba
Mtakatifu, Papa Francis, Rais wa Italia, Mheshimiwa Sergio Mattarella,
Rais wa Uturuki, Mheshimiwa Recep Tayyip Erdogan, Rais wa Finland,
Mheshimiwa Sauli Niinistö, Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo,
Mheshimiwa Joseph Kabila Kabange na Rais wa Jamhuri ya Sudan, Mheshimiwa
Omar Hassan Ahmed Al-Bashir.
Viongozi wengine ni Waziri Mkuu wa Israel, Mheshimiwa Benjamin Netanyahu, na Waziri Mkuu wa Sweden, Mheshimiwa Stefan Löfven.
Viongozi
hao wameeleza kusikitishwa kwao na taarifa za vifo vilivyosababishwa
na ajali hiyo na kuwatakia majeruhi kupona haraka.
Sehemu
ya nukuu za salamu hizo zinasema “Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe
Magufuli, nilipokea kwa huzuni na masikitiko makubwa taarifa za ajali ya
kivuko cha MV Nyerere iliyosababisha vifo vya watu wengi, majeruhi na
wengine kutojulikana walipo. Kwa niaba ya Serikali na wananchi wa Kenya
naomba upokee na kufikisha salamu zetu za rambirambi kwa wafiwa na
wananchi wote wa Tanzania kufuatia ajali hiyo na tunawaombea majeruhi
wote wapone haraka” ni sehemu ya nukuu ya salamu kutoka kwa Mheshimiwa
Rais Kenyatta
“Mheshimiwa
Rais Dkt. John Pombe Magufuli, nilishtushwa na taarifa za ajali hiyo
mbaya iliyotokea Mkoani Mwanza. Kwa niaba ya Serikali ya China, wananchi
na mimi binafsi natoa pole kwa wafiwa wote na majeruhi” inasema sehemu
ya salamu kutoka kwa Rais wa China, Mheshimiwa Xi Jinping.
Naye
Rais wa Urusi, Mheshimiwa Putin amesema “Mheshimiwa Rais Dkt. John
Pombe Magufuli, tafadhali naomba upokee salamu zangu za rambirambi
kufuatia ajali iliyotokea. Naomba salamu hizi ziwafikie wafiwa wote na
ninawaombea majeruhi wapone haraka”
Aidha,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki imepokea
salamu za rambirambi kutoka kwa balozi mbalimbali zinazowakilisha nchi
zao hapa nchini pamoja na mashirika ya kimataifa yaliyopo nchini,
ikiwemo ubalozi wa Marekani, ubalozi wa Ufaransa, ubalozi wa Sudan
Kusini, Ubalozi wa Falme za Kiarabu (UAE), Serikali ya Brazil, Ubalozi
wa Cuba, ubalozi wa Nigeria na salamu kutoka kwa Mratibu Mkazi wa
Mashirika ya Kimataifa nchini.
Wakati
huohuo, Wizara imepokea salamu za rambirambi kutoka kwa mabalozi
wanaowakilisha Tanzania kwenye nchi mbalimbali. Salamu zilizopokelewa
zinatoka kwa mabalozi wote wa Tanzania katika nchi za Qatar, Ufaransa,
Uingereza, Uholanzi, Afrika Kusini, Sweden, Nigeria, Burundi, Uganda,
Kenya, Ubelgiji, Zambia, Msumbiji, China, Japan, Brazil, Comoro,
Algeria, Sudan, Canada,
Kadhalika
tumepokea salamu kutoka kwenye balozi zetu zilizoko Marekani, Uturuki,
Rwanda, Umoja wa Falme za Kiarabu, Misri, Kuwait, Saudi Arabia, Jamhuri
ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Zimbabwe, Malawi, Uswisi, India, Italia,
Jamhuri ya Korea, Urusi, Israel, Ethiopia, Ujerumani, Oman na Malaysia.
Baadhi
ya nukuu ya salamu za rambirambi za mabalozi hao zinasomeka kama
ifuatavyo “Inna Lillah Wainna Illah Rajiuon. Kwa niaba ya Ubalozi
Abuja na Watanzania waliopo katika eneo letu la uwakilishi,
tunatoa pole kwa Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, familia na Watanzania kwa ujumla
kwa msiba mkubwa uliotufika. Mwenyezi Mungu atupe subira na
faraja katika kipindi hiki cha majonzi na aziweke roho za
marehemu mahali pema na majeruhi wapone haraka, Amin Amin,” ni
kauli yake Mheshimiwa Muhidin Ally Mboweto, Balozi wa Tanzania nchini
Nigeria.
Naye
Balozi wa Tanzania nchini Sweden, Mheshimiwa Dkt. Wilbroad Slaa anasema
“kwa niaba ya wenzangu katika kituo cha Stockholm tunatoa pole za dhati
kwa Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, ndugu na familia zote zilizoguswa na msiba huu
mkubwa. Mwenyezi Mungu azilaze roho za marehemu mahali pema peponi na
kuwatia nguvu na ujasiri ndugu wote walioguswa na msiba huu”.
Kwa
upande wake Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa
Mheshimiwa Balozi Modest Mero alisema haya; “Ubalozi wa New York tunatoa
pole kwa ajali mbaya ya Meli ya MV Nyerere iliyopelekea wengi kupoteza
maisha na wengi kuumia. Tunawaombea marehemu pumziko la milele na wote
waliojeruhiwa wapone haraka.”
Balozi
wa Tanzania nchini China, Mheshimiwa Mbelwa Kairuki alieleza masikitiko
yake kwa kusema kuwa “nasi huku Beijing tunaungana na wenzetu kutoa
pole kwa Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Watanzania na
wanafamilia walioguswa msiba huu mzito. Mwenyezi Mungu awape nguvu na
awajalie moyo wa subira wakati wote mnaposhughulika na msiba huo.
“Japan
na diaspora yetu tunatoa pole kwa Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph
Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Watanzania wote kwa
msiba huu uliotokana na kuzama kwa kivuko. Mungu atupe nguvu wote
tuliobaki na awape pumziko la amani wenzetu waliotutangulia. Kwa
majeruhi tunawaombea wapone haraka na wavumilie mstuko huu mkubwa katika
maisha yao. Marehemu wapumzike kwa amani”. Hizi ni salamu kutoka kwa
Mheshimiwa Mathias Chikawe, balozi wa Tanzania nchini Japan.
Kwa
upande wake, Balozi wa Tanzania nchini Abu Dhabi alisema haya; “Ubalozi
wa Tanzania Abu Dhabi, tumepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za
ajali ya MV Nyerere.Kwa niaba ya watumishi wote wa Ubalozi, tunatoa
mkono wa pole kwa Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Joseph Magufuli na
Watanzania wenzetu wote kwa msiba huu mkubwa. Mwenyezi Mungu awajaalie
marehemu wapumzike mahali pema na awajaalie majeruhi kupona mapema.
Amin”.
Naye
Balozi wa Tanzania nchini Uingereza, Mheshimiwa Dkt. Asha-Rose Migiro
akieleza kuguswa na ajali hiyo alitoa kauli hii “Ubalozi wa Tanzania
London unajumuika na Watanzania wenzetu kutoa pole kwa Mheshimiwa Rais
Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, familia na ndugu wa wale wote
waliopatwa na msiba kutokana na ajali hii. Tunawaombea majeruhi wapone
haraka na warejee katika shughuli zao za kujikimu na kulijenga taifa
letu”.
Kwa
upande mwingine, Wizara imepokea salamu za rambirambi kutoka Baraza la
Diaspora wa Tanzania ulimwenguni kote (TDC Global) ambao wameeleza
masikitiko makubwa kufuatia ajali hiyo mbaya. Sehemu ya ujumbe wao
unasomeka kama ifuatavyo; “TDC Global, kwa masikitiko makubwa, inatoa
salamu za rambirambi kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli na Watanzania wote, ndugu,
jamaa na marafiki kwa vifo vilivyotokana na ajali ya kuzama kwa kivuko
cha MV. Nyerere kinachofanya safari zake kati ya visiwa vya Bugorora na
Ukara katika Ziwa Victoria. Kama TDC Global, tunaungana na Watanzania
wote katika kuomboleza msiba huu mzito kwa taifa letu. Pia tunatoa pole
kwa majeruhi wote na kuwaombea wapone haraka”.
No comments:
Post a Comment