Jeshi
la Polisi mkoani hapa limefanikiwa kupata gari lililoibiwa aina ya
Toyota Surf lenye namba za usajili T.996 AGK pamoja na Bastola aina ya
Browning iliyokuwa na risasi Nane ndani ya Magazine.
Akizungumza
na Waandishi wa habari jana mchana Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Arusha
Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Ramadhani Ng’anzi alisema
kwamba tukio la kuibiwa kwa gari hilo lililokuwa linaendeshwa na Bi.
Sarah Cornel (40) Mwalimu wa Sekondari na ni mkazi wa Olasiti jijini
hapa lilitokea Septemba 17 muda wa saa 9:50 Alasiri katika maeneo ya
Stand Ndogo.
“Mara
baada ya kuegesha gari lake maeneo ya Stendi Ndogo alienda madukani kwa
ajili ya kufanya manunuzi aliporudi hakulikuta ndipo alipoelekea kituo
Kikuu cha Polisi kwa ajili ya kutoa taarifa ambayo ilifanyiwa kazi kwa
kuanza kuweka vizuizi maeneo ya barabara kuu na kufanya msako mkali”.
Alisema
wahalifu hao baada ya kuona njia zote zimedhibitiwa waliamua
kulitelekeza gari hilo katika kituo cha Afya Kaloleni kilichopo jijini
hapa ambapo siku ya pili muda saa 05:30 Asubuhi lilipatikana huku
watuhumiwa wakiwa wametoweka na Jeshi hilo linaendelea kufanya uchunguzi
wa Kisayansi ili kuweza kuwabaini.
Mbali
na tukio hilo Polisi mkoani hapa wameweza kupata silaha aina ya bastola
ambayo ilikuwa na risasi nane ndani ya Magazine, Kamanda Ng’anzi
alisema lilitokea Septemba 15 mwaka huu katika kijiji cha Kimyaki
kilichopo tarafa ya Enaboishu wilayani Arumeru.
Alisema
Jeshi hilo lilipata taarifa hiyo toka kwa raia wema ambapo waliwadokeza
kuwapo kwa silaha hiyo ndani ya chumba cha mtu waliyekuwa wanamdhania
mhalifu ndipo askari walikwenda katika eneo hilo na kufanikikwa kupata
silaha hiyo ambayo wanakiri ilikuwa inamilikiwa isivyo halali na Jeshi
hilo linaendelea na msako mkali kumtafuta mtuhumiwa huyo.
Mbali
na mafanikio hayo msako wa Jeshi hilo umeweza kufanikisha kupata mali
mbalimbali zikiwemo TV mbili “flat Screen”, Laptop, Jenereta na vitu
vingine ambavyo vinasadikiwa kuibiwa katika mitaa mbalimbali ya jiji la
Arusha siku za nyuma.
Kwa
upamde wa Usalama barabarani Jeshi hilo limepanga kuanzisha kikosi
maalum kwa ajili ya kuwadhibiti waendesha boda boda wanaovunja sheria
hasa za kubeba abiria zaidi ya mmoja maarufu kama “Mishikashi” na wale
wanaovuka mataa bila kuruhusiwa.
Kamanda
Ng’anzi alisema kikosi hicho kitakuwa na askari ambao watakuwa wanavaa
kiraia na watasambazwa katika maeneo mbalimbali ya jiji la Arusha hali
ambayo anaamini itakomesha tabia ya madereva wa boda boda wanaovunja
sheria kwa makusudi.
No comments:
Post a Comment