Serikali imesitisha matangazo yanayohamasisha uzazi wa mpango yanayorushwa kwenye runinga na redio mbalimbali nchini mpaka itakapotangazwa tena.
Sitisho
 hilo limetolewa katika taarifa iliyotolewa na Katibu Mkuu wa Wizara ya 
Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Mpoki Ulisubisya 
kwenda kwa Shirika la Msaada la Marekani (USAID).
Shirika
 hilo ndilo linalofadhili mradi wa Tulonge Afya unaotoa matangazo hayo 
ya kuhamasisha uzazi wa mpango kwenye vyombo vya habari.
Barua
 hiyo iliyosambaa mitandaoni, inaeleza kuwa serikali inatambua mchango 
na juhudi za shirika hilo katika kuboresha uzazi wa mpango.
Inaeleza
 kuwa wizara inakusudia kufanya marejeo ya maudhui yote ya matangazo 
kwenye runinga na redio kwa ajili ya uzazi wa mpango.
“Hivyo
 unaombwa kusimamisha mara moja kutangaza na kuchapisha maudhui yoyote 
yale ya uzazi wa mpango kwenye vyombo vya habari mpaka itakavyoamuliwa 
vinginevyo,” inaeleza taarifa hiyo.
Akiwahutubia
 mamia ya watu Septemba 9, mjini Meatu Mkoani Simiyu, wiki mbili 
zilizopita, Rais John Magufuli alisema Watanzania waendelee kuzaa, 
lakini wachape kazi ili kukidhi mahitaji ya watoto wanaowazaa.
Alisema
 anafahamu Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu angependa kuongelea mambo ya 
uzazi wa mpango, lakini mengine yeye (Magufuli) hakubaliani nayo.
“Najua
 Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu, angependa kuongelea mambo ya uzazi wa 
mpango hapa, lakini mimi mengine huwa sikubaliani nayo sana, 
utapangiwaje kuzaa...kwa hiyo katika kushauriwa mengine tukubali na 
mengine tukatae tutumie msemo wa mzee Jakaya Kikwete ‘Ukiambiwa 
changanya na za kwako’ kuzaa ni muhimu,” alisema.
Katika
 mkutano huo Rais Magufuli aliwaeleza wananchi kuwa katika mataifa ya 
kigeni aliyowahi kuishi hakuwahi kusikia wimbo wa uzazi wa mpango.






No comments:
Post a Comment