Mkurugenzi
Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro, Kayombe Lyoba amewaagiza
wazazi na walezi wenye watoto wanaotarajia kujiunga kidato cha kwanza
mwaka huu kuhakikisha wanakwenda na kiti na meza ili waweze kuingia
darasani.
Hali
hiyo imekuja baada ya halmashauri hiyo kuongeza kasi kwenye ujenzi wa
vyumba vya madarasa ili kila mwanafunzi aliyechaguliwa kuingia kidato
cha kwanza apate fursa ya kuanza masomo.
“Tunawaomba
wazazi na walezi wawezeshe watoto wao kuja na kiti na meza pindi
wanapokuja kuanza masomo Januari 7, kwani tayari tumeshaongeza jitihada
kuhakikisha vyumba vya madarasa vinakuwepo vya kutosha ili asikose
kuingia mwanafunzi hata mmoja,” alisema Lyoba.
Alisema
jumla ya wanafunzi 4,136 wamepokewa na halmashauri iwemeweza kujenga
vyumba vya madarasa 87 na kubakiwa na upungufu wa vyumba 32.
Kwa
upande wake, Mwenyekiti wa halmashauri hiyo, Kibena Kingo alisema mbali
na jitihada za kujenga maabara katika shule zao kuna changamoto ya
uhaba wa walimu wa masomo ya sayansi.
“Halmashauri
yetu ina upungufu wa walimu 41 wa kufundisha masomo ya sayansi, hivyo
tunamwagiza Ofisa Elimu Sekondari kulifuatilia suala hilo kwa ukaribu
ili tuweze kuondokana na changamoto hiyo,” alisisitiza Kingo.
Aidha
Ofisa Elimu Sekondari, Hatujuani Ally alisema Serikali ndiyo inayopanga
walimu na hadi sasa imeweza kuleta walimu wa sayansi katika Shule ya
Sekondari Nelson Mandela, Matombo, Kibogwa na Mvuha na matarajio ni
kuongeza walimu wengi zaidi kwenye shule ambazo zina uhitaji mkubwa.
Ally
aliongeza kwamba Wilaya ya Morogoro kwa sasa ina jumla ya walimu wa
kufundisha masomo ya sayansi 42 huku mahitaji yakiwa ni walimu 83 katika
shule 28 zilizopo.
No comments:
Post a Comment