KUWASA KAHAMA YAAGIZWA KUFUFUA CHANZO CHA MAJI CHA NYIHOGO


Na Amina Mbwambo
KAHAMA

SERIKALI wilayani KAHAMA imeiagiza Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira mjini Kahama (KUWASA) kuhakikisha inakifufua na kukitunza chanzo cha maji cha Bwawa la Nyihogo ili kitumike wakati chanzo kikuu cha maji kutoka ziwa Victoria kinapopata hitilafu.

Agizo hilo limetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Kahama, FADHILI NKURLU wakati wa zoezi la upandaji miti katika Bwawa hilo la Nyohogo lililofanyika jana chini ya uratibu wa Wakala wa Misitu (TFS), wilayani humo.

Akizungumza wakati wa zoezi hilo, Mwenyekiti wa Bodi ya KUWASA, Meja Mstaafu BAHATI MATALA ameishukuru serikali kwa kulirudisha eneo hilo rasmi chini ya KUWASA na ameahidi kulisimamia na kuliendeleza.

Amesema Mamlaka yake tayari imepanda miti 6100 katika juhudi za kupambana na uharibifu mkubwa wa mazingira uliosababishwa na shughuli za kibinadamu katika Bwawa hilo la Nyihogo.

Jumla ya miche ya miti 500 ilipandwa katika chanzo hicho cha Nyihogo jana, huku kaimu meneja wa TFS wilaya ya Kahama, MOHAMED DOSSA akibainisha kuwa wanatarajia kupanda miti 34,000 katika eneo la mita za mraba 53,125 wilayani humo mwezi huu.

DOSSA ameibanisha kuwa nia ya Wakala wa Misitu ni kuhakikisha wilaya ya Kahama inakuwa na mandhari ya kijani wakati wote.

Takwimu zinaonesha kuwa Tanzania bara ina jumla ya hekta milioni 48.1 za misitu ambayo ni sawa na 55% ya eneo lote la Tanzania bara.
Share:

No comments:

Post a Comment

IDADI YA WASOMAJI

TUSIKILIZE LIVE KUPITIA TUNEIN

UNGANA NASI FACEBOOK HAPA

10 ZILIZOSOMWA ZAIDI

Labels

Blog Archive