Serikali
imezitaka halmashauri zote nchini kuhakikisha zinatoa vibali vya ujenzi
wa nyumba ndani ya siku tatu na kazi hiyo isimamiwe na Maofisa Mipango
Miji.
Aidha,
imesisitiza kuwa zoezi la urasimishaji katika maeneo yaliyojengwa
nyumba kiholela lazima yarasimishwe na zoezi hilo halitakiwi kubomoa
nyumba ya mtu yoyote.
Kauli
hiyo imetolewa jana na Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi
William Lukuvi wakati akifungua mkutano wa tano wa Bodi ya Wataalamu wa
Usajili Mipango Miji unaoendeleo katika jiji la Dodoma.
Lukuvi
alisema vibali vya ujenzi wa nyumba katika maeneo mbalimbali lazima
vitolewe aidha katika eneo lililopangwa ama lisilo pangwa na cha msingi
serikali inachotaka ni kuwa na majengo yaliyo katika mpangilio mzuri na
kuongeza kuwa ucheleweshwaji wowote utoaji kibali lazima mhusika
afahamishwe sababu za kucheleweshewa kupatiwa kibali.
Kwa
mujibu wa Lukuvi lengo la Maofisa Mipango Miji kupewa mamlaka ya kutoa
vibali vya ujenzi badala ya wakuu wa idara wa halmashauri husika
linatokana na baadhi yake kuongozwa na watu wasiokuwa na taaluma za
mipango miji jambo linaloweza kuvuruga upangaji miji bora kwenye maeneo.
Pia
ametaka nakala za vibali vya ujenzi vitakavyotolewa na kuhakikisha
nakala hizo za vibali zinaenda pia katika ofisi za maafisa watendaji wa
mitaa kwa kuwa watendaji hao wanapaswa kufahamu ujenzi unaoendelea
katika maeneo yao.
Lukuvi
ameitaka Bodi ya Usajili Mipango Miji kuandaa muongozo utakaosaidia
watendaji wa mitaa kuwa na ufahamu katika kusimamia mipango ya
uendelezaji miji jambo litakalosaidia pia kuepuka ujenzi holela katika
baadhi ya maeneo.
Akigeukia
suala la urasimishaji maeneo yasiyopimwa, Lukuvi alisema pamoja na
zoezi hilo kufanyika nchi nzima lakini hakuna nyumba itakayovunjwa
katika zoezi hilo na kutaka makampuni yote yatakayotaka kufanya kazi ya
urasimishaji kutuma maombi yao kupitia ofisi za wilaya na kuacha kuenda
moja kwa moja kufanya kazi hiyo kupitia kamati maalum za maeneo husika
na kusisitiza kuwa zoezi hilo lazima liratibiwe na Maofisa Mipango Miji.
Katika
hatua nyingine, Lukuvi amepiga marufuku upimaji mashamba katika maeneo
mbalimbali bila ya kupangwa na kubainisha kuwa serikali haitakubali
kadhia hiyo iendelee kushamiri kwani suala hilo linafanya miji kukosa
maeneo ya wazi, mashule, masoko na hospitali.
Salfonce
Kesi Mtafiti na mwalimu katika Chuo cha Ardhi alisema, kwa sasa mambo
mengi ya upangaji miji katika maeneo mbalimbali nchini hayaendi vizuri
kutokana na mipango kufanywa na watu wasio na taaluma ya mipango miji.
Alisema,
ni lazima suala la mipango miji katika maeneo lianze ndipo mipango
mingine ya maendeleo iendelee kama vile huduma za maji, barabara pamoja
na huduma nyingine za jamii.
Mwenyekiti
wa Bodi ya Usajili Mipango Miji Profesa Wilbert Kombe alisema bodi yake
imeanza kuchukua hatua mbalimbali kuhakikisha taaluma ya Mipango Miji
inakuwa na wataalamu wanaozingatia sheria na kuchangia kuwepo miji bora
na iliyopangika na kubainisha kuwa mahali popote sura ya miji ndiyo
inayotoa taswira ya maisha ya eneo husika.