AFIKISHWA MAHAKAMANI KWA TUHUMA YA WIZI


Na Lilian Katabaro
KAHAMA.

Mkazi wa Kigamboni Jijini DARESALAAM, ABASI JUMA (32) amefkishwa katika Mahakama ya Wilaya ya KAHAMA kwa tuhuma ya wizi wa kuaminika kinyume cha sheria.

Mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama hiyo EVODIA KYARUZI, mwendesha mashitaka wa Polisi EVODIA BAIMO amesema Febuari 15/2013 mtaa wa Malunga, Kahama, JUMA aliiba tani 25 za mchele zenye thamani ya shilingi milioni 50 mali ya PAMBA FESTOS .

BAIMO amesema katika shauri hilo la jinai namba 195/2018 JUMA ametenda kosa hilo kinyume na kifungu namba 27 cha kanuni ya adhabu sura ya 16 marejeo ya mwaka 2002.

BAIMO amesema upelelezi wa shauri hilo haujakamilika na JUMA amerudishwa rumande kwa kukosa dhamana na shauri hilo kutajwa tena Mahakamani hapo June 12 mwaka huu.
Share:

WAFANYABIASHARA WA MABINGWA MSALALA WASEMA ENEO LA SOKO SI RAFIKI KWA BIASHARA ZAO



Na Ndalike Sonda
KAHAMA.

Wafanyabiashara katika soko la Mabingwa Kata ya Bugarama Halmashauri ya MSALALA Wilayani KAHAMA Mkoani SHINYANGA wamesema eneo hilo si rafiki na biashara zao kutokana na kuwa mbali na makazi ya watu hivyo kuwasababishia hasara katika bidhaa zao.

Wakizungumza kwenye kipindi cha Raha ya leo, cha KAHAMA FM, wananchi hao wamesema tangu wahamishiwe katika soko hilo mwaka jana, wateja hawafiki kwa wingi kwani wananunua kwa wachuuzi wanaozungusha biashara katika makazi ya watu.

Mwenyekiti wa soko la hilo, SALOME HAMISI ameiomba halmashauri iboreshe miundombinu ya eneo hilo ikiwamo kuimarisha kituo kikuu cha mabasi cha Halmashauri hiyo na vivutio vingine.

Afisa Mtendaji wa Kata ya Bugarama PRISCA PIUS amesema uongozi wa kata hiyo umekusudia kufungua mnada wa mifugo na mazao katika eneo hilo huku diwani wa viti maalum wa kata hiyo, PRISCA MSOMA amesema ni ufinyu wa bajeti na kwamba wanakusudia kuwarejesha soko la zamani.

Eneo la soko la Mabingwa lipo katika eneo la kituo kikuu cha mabasi cha halmashauri ya Msalala, ambapo tangu kufunguliwa kwake mwaka jana, mabasi yamekuwa hayaegeshi eneo hilo hivyo kusababisha wafanyabiashara waliohamishiwa eneo hilo kuendelea kulalamika.
Share:

MADEREVA BODABODA WATAKIWA KUPEWA ELIMU YA UVAAJI WA KOFIA NGUMU


Na Ndalike/Kijukuu
KAHAMA.

Kutokana na ajali za pikipiki kuendea kujitokeza mara kwa mara Wilayani KAHAMA Mkoani SHINYANGA na kusababisha vifo na majeruhi,waendeshaji wa Pikipiki hasa vijana wametakiwa kupewa elimu ya uvaaji wa kofia ngumu, (helement) ikiwemo kufuata sheria za usalama barabarani.

Hayo yamesemwa na Mkazi wa Bukondamoyo, PANKARASI ITALUMA kwenye mazishi ya mtoto wake LUCAS ITALUMA (30) aliyefariki dunia jana kutokana na ajali pikipiki iliyotokea mwanzoni mwa mwezi wa tano mwaka huu.

Italuma amsema elimu itolewe kwa makundi yote huku akiwataka waendesha pikipiki kuzingatia sheria za usalama barabarani zilizotolewa na jeshi la polisi ili kuepusha ajali zinazoweza kusababisha vifo na majeruhi.

Naye Katekista wa kanisa katoliki kigango cha mtakatifu veronika Bukondamoyo ELADIUS PASCHAL ameitaka jamii kutambua kuwa maisha ya dunia ni mafupi hivyo ni vyema kutenda matendo mema ikiwamo kuwasaidia watu wenye uhitaji.

Wiki iliyopita aliyekuwa mfanyakazi wa idara ya maji na usafi wa mazingira mjini Kahama KUWASA, alifariki dunia kwa ajali ya pikipiki baada ya kuaanguka akiwa katika mwendo kasi na kutovaa kofia ngumu.

Marehemu Lucas Italuma ambaye alikuwa Dereva na fundi wa Magari ameacha mke nawatoto watatu.
Share:

SERIKALI YASHAURIWA KUWEKA MTAALA WA SOMO LA WATU WENYE ULEMAVU WAKIWEMO ALBINO



Na Ndalike Sonda
KAHAMA.

Serikali imeshauriwa kuweka mtaala wa somo la watu wenye ulemavu ukiwemo wenye Ualbino kwenye shule za msingi na sekondari ili kuwawezesha wanafunzi kuelewa haki za walemavu na kuondoa unyanyapaa dhidi yao.

Hayo yameelezwa katika Kata ya Bugarama Halmashauri ya MSALALA Wilayani KAHAMA Mkoani SHINYANGA, na baadhi ya washiriki wa semina ya kutathimini elimu ya watu wenye ualbino iliyoshirikisha washiriki kutoka kata za Bulyanhulu na Bugarama katika Halmashauri hiyo.

Wakichangia katika semina hiyo, DEVOTHA KAPESA na JOYCE LWANJI wamesema serikali ilitazame suala hilo kwani elimu hiyo ni muhimu kwa watoto waweze kuelewa kwamba ulemavu huo ni jambo la kawaida kwa binadamu.

Katibu wa Chama cha watu wenye ualbino Tanzania (TAS) wilaya ya Kahama, SITA MASENYA ameyaomba mashirika, taasisi mbalimbali kuendelea kutoa elimu kwa jamii juu ya watu wenye ualbino ili kujenga uelewa wa kutosha kwa wananchi.

Kufuatana na takwimu za mwaka jana, Wilaya ya Kahama ina watu wenye Ualbino wapatao 96, ambapo imebainika kwamba kukosekana kwa elimu kunasababisha baadhi ya familia kuwaficha watoto wenye ulemavu huo na hata jamii kuwanyanyapaa.


Share:

MGODI WA KABELA ILINDI MJINI KAHAMA WAANZA MIKAKATI YA KUPANDA MITI



Na Ndalike Sonda
KAHAMA.

Mgodi wa Kabela ilindi Gold Mine katika Halmashauri ya mji wa KAHAMA mkoani SHINYANGA umeanza mikakati ya kupanda miti wakati wa kiangazi kwa njia ya kisasa ambapo umwagiliaji wake ukakuwa wa matone.

Akizungumza na KAHAMA FM, Mkuu wa Idara ya Afya na Mazingira katika Mgodi huo, MACHIMU NELSON amesema tayari maandalizi yamekwisha kuanza ikiwamo uchimbaji wa mashimo kwaajili ya upandaji wa miche ya miti.

Amesema Kutokana na njia hiyo ya umwagiliaji, Miti yote ikayopandwa wakati wa kiangazi itasitawi vizuri na kwamba wanashirikiana na Ofisi ya mkuu wa wilaya katika kutekeleza zoezi hilo.

MACHIMU amewataka wachimbaji wa madini katika mgodi huo pamoja na wananchi wengine kuendelea kutunza miti katika maeneo hayo pamoja na kudumisha suala la usafi katika maeneo yao.

Mwezi Machi mwaka huu, Mkuu wa wilaya ya Kahama FADHILI NKURLU alizundua kampeni ya upandaji wa miti katika Mgodi wa Kabela Ilindi Gold Mine na kuwataka viongozi wa mgodi huo kufanya zoezi hilo kuwa endelevu.
Share:

WAWILI WAINGIA PORI LA AKIBA LA KIGOSI MOYOWOSI BILA KIBALI NA KUKUTWA NA SILAHA



Na Daniel Magwina
KAHAMA.

Wakazi wawili wa kijiji cha Kalenga Wilayani Biharamulo, Mkoani Kagera, SIYAJALI KALOLI (37) na ELIAS DOTTO (20) wamefikishwa katika mahakama ya wilaya ya KAHAMA kwa tuhuma ya kuingia katika Pori la Akiba la Moyowosi - Kigosi na kupatikana na silaha bila kibali.

Mbele ya Hakimu Mkazi wa Mahakama hiyo KENETH MUTEMBEI, mwendesha mashitaka wa Idara ya wanyamapori, INNOCENTI MUTAGWABA amesema Mei 2O mwaka huu saa mbili usiku Washitakiwa waliingia ndani ya Pori hilo bila kibali cha Mkurugenzi wa Wanyamapori.

MUTAGWABA amesema washitakiwa hao pia walikamatwa wakiwa na msumeno ambao walikuwa wanautumia kukatia miti ya kupasulia mbao kinyume cha sheria.

Washitakiwa wote wamekiri kutenda makosa yote mawili kuingia hifadhi bila kibali pamoja na kupatikana na msemeno katika hifadhi kinyume cha sheria

Katika shitaka la pili washitakiwa wanadaiwa kupatikana na silaha kinyume na kifungu namba103 cha sheria ya uhifadhi Wanyamapori namba 5 ya mwaka 2009.

Katika shauri hilo la jinai naimba 190/2018 washitakiwa wametenda kosa la kwanza la kuingia hifadhi bila kibali kinyume na kifungu namba 18 cha sheria ya wanyamapori namba 5 ya mwaka 2009.

Washitakiwa wote wamerudishwa rumande kwa kukosa dhamana hadi shauri hilo litakapo tajwa tena mahakamani hapo Juni 6 mwaka huu.
Share:

AFIKISHWA MAHAKAMANI KWA TUHUMA YA KUKIUKA MASHARTI YA LESENI YA USAFIRISHAJI


Na Paulina Juma
KAHAMA.

Mkazi wa BUZWAGI Wilayani KAHAMA, PIUS LEONARD (27) amefikishwa katika mahakama ya Wilaya ya KAHAMA kwa tuhuma ya kukiuka masharti ya leseni ya usafirishaji kinyume cha sheria.

Mbele ya Hakimu mkazi wa Mahakama hiyo IMAN BATENZI, Mwendesha Mashitaka wa jeshi la Polisi, FELIX MBISE amesema LEONARD ametenda kosa hilo Mei 22 mwaka huu katika kituo kikuu cha mabasi cha mjini Kahama.

FELIX amedai kuwa LEONARD akiwa ni wakala wa kampuni ya basi lenye namba za usajili T 997 TZT linalofanya safari zake kati ya Kahama na Dar es Salaam alishindwa kuwasafirisha abiria wake huku akiwa amekwisha wakatia tiketi.

Katika shauri hilo la jinai namba 616 la mwaka huu LEONARD amefanya kosa hilo kinyume na kifungu namba 22 cha kanuni ya leseni ya usafirishaji wa abiria sura ya 317, marejeo ya mwaka 2002.

LEONARD amekana shitaka hilo na yuko nje kwa dhamana na shitaka hilo limeahirishwa hadi June 6 litakapotajwa tena mahakamani hapo.
Share:

MIMBA NA NDOA ZA UTOTONI CHANGAMOTO KWA WANAFUNZI WILAYANI KAHAMA


Na Salvatory Ntandu
KAHAMA.

Kukosekana kwa Elimu juu ya Masuala ya ndoa na mimba za Utotoni kwenye jamii Wilayani KAHAMA Mkoani SHINYANGA kunawanyima haki ya kupata elimu Wanafunzi chini ya miaka 18 kutokana na baadhi yao kupata ujauzito.

Hayo yamebainishwa na Afisa Ustawi wa Jamii wa Halmashauri ya Mji wa Kahama, ABDURAHMAN NURU wakati akitoa elimu juu ya kupambana na ndoa na mimba za utotoni kwa wazazi katika kata ya Iyenze.

NURU ametahadharisha kwamba ikiwa wazazi hawataacha kuwaozesha watoto wa kike husasani wanafunzi kwa tamaa ya kupata mali watakabiliwa na mkono wa sheria.

Naye Meneja Mradi wa kuzuia ndoa na mimba za utotoni kwa watoto chini ya miaka 18 kutoka shirika lisilo la kiserikali la Rafiki - SDO, ELIUD LAZARO amesema wameamua kutoa elimu hiyo kwa wazazi ili waweze kutoa malezi bora kwa watoto wao.

Kwa upande wake KERILIAN DANFORD ambaye ni miongoni mwa watoto wa kike waliofanikiwa kupata elimu hadi chuo kikuu na sasa ameajiriwa na Shirika hilo la Rafiki – SDO, amewaomba wazazi kuwasomesha watoto wakike ili waweze kutimiza ndoto zao za maisha.

Mkoa wa Shinyanga unaongoza kwa tatizo la ndoa na mimba za utotoni hapa nchiniuikifuatiwa na mikoa ya Geita,Tabora na Simiyu.
Share:

WAFIKISHWA MAHAKAMANI KWA TUHUMA YA MAUAJI


Na Lilian Katabaro
KAHAMA.

Wakazi wawili wa kijiji cha Ibelansua Wilayani KAHAMA Mkoani SHINYANGA, MARTINE MTOBE (30) na GODFREY JULIUS(29) wamefikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya KAHAMA kwa tuhuma ya mauaji.

Mbele ya Hakimu Mkazi wa Mahakama hiyo IMANI BATENZI, mwendesha mashitaka SAADA ADAM amedai March 23 mwaka huu saa tatu usiku katika kijiji cha Nhendya kata ya Ulowa, Halmashauri ya Ushetu washitakiwa walimuua CHAUSIKU REUBEN kwa kutumia panga.

SAADA amesema Washitakiwa wametenda kosa hilo kinyume na kifungu namba 196 sura ya 16 kanuni ya adhabu marejeo ya mwaka 2002.

Katika shauri hilo la jinai namba 09/2018, Washitakiwa hawakutakiwa kujibu chochote kwa sababu Mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza mashauri ya mauaji.

Washitakiwa wamerudishwa rumande na shauri hilo litatajwa tena Mahakamani hapo Mei 5 mwaka huu.
Share:

MFANYAKAZI WA KUWASA KAHAMA AFARIKI KWA AJALI YA PIKIPIKI



Na Daniel Magwina
KAHAMA.

Mkazi wa Nyahanga Mjini KAHAMA na mfanyakazi wa Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira mjini Kahama mkoani shinyanga, REXPIRIUS VICENT (29) amefariki dunia kwa ajali ya pikipiki iliyotokea mapema leo alfajiri katika mtaa wa Igalilimi mjini humo.

Akithibitisha kutokea kwa ajali hiyo mkuu wa kitengo cha usalama barabarani wilayani Kahama DESIDERI KAIGWA amesema kuwa ajali hiyo imehusisha pipipiki aina ya boksa yenye namba za usajili T (40403), aliyokuwa akiendesha Marehemu VICENT.

KAIGWA amesema chanzo cha ajali hiyo ni mwendo kasi wa dereva pamoja na kutokuvaa kofia ngumu na ametoa rai kwa watumiaji wa vyombo vya moto hususani pikipiki kuvaa kofia ngumu ili kuchukua tahadhari pindi ajali inapotokea.

Msemaji wa Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira mji Kahama (KUWASA), JOHN MKAMA pamoja na kueleza jinsi walivyopokea taarifa ya msiba huo amesema taratibu za mazishi zinaendelea kufanyika na kwamba mwili wa marehemu utasafirishwa kuelekea kwao mkoani Kigoma kwa ajili ya mazishi.
Share:

KICHANGA CHAOKOTWA KIKIWA KIMEKUFA NYAKATO WILAYANI KAHAMA


Na Ndalike Sonda
KAHAMA.

Mtoto mchanga wa kiume anayekadiriwa kuwa wa siku ameokotwa akiwa amefariki dunia kandokando ya karavati lililopo Mtaa wa Nyakato Kata ya NYASUBI jirani na kituo cha Mafuta cha Front oil Mjini KAHAMA na mwanamke ambaye hajafahamika majina wala makazi yake.

Kwa mujibu wa mashuhuda wa tukio hilo, Kichanga hicho ambacho kinasadikiwa kimetupwa tangu majira ya asubuhi kimeokotwa majira ya saa tisa alasiri.

Wakizungumza na KAHAMA FM, mashuhuda hao wamesikitishwa na kitendo hicho huku wakiomba hatua kali zichukuliwe dhidi ya mwanamke atakayebainika kutenda unyama huo.

Diwani wa Kata ya Nyasubi, ABEL SHIJA ameiomba jamii kutoa ushirikiano kwa viongozi wa serikali na jeshi la Polisi ambao wanaendelea na uchunguzi wa tukio hilo na na kusema kwamba kitendo cha kutupa mtoto hakina tija kwa jamii.

Jeshi la Polisi wilayani Kahama limefika eneo la tukio na kuuchukua mwili wa kichanga hicho kwaajili ya kwenda kuuhifadhi kwenye chumba cha kuhifadhi maiti katika hospitali ya Mji wa Kahama pamoja na taratibu zingine.

Matukio ya kutelekeza na kutupa watoto katika wilaya ya Kahama yamekuwa yakijitokeza Mara kwa mara ambapo mapema mwezi huu, mtoto mchanga mwingine aliokotwa akiwa mzima katika shamba moja kijiji cha Sungamile kata ya Mwalugulu Halmashauri ya Msalala.
Share:

AFIKISHWA MAHAKAMANI KWA TUHUMA YA WIZI


Na Lilian Katabaro
KAHAMA.

Mkazi wa mtaa wa Mhongolo katika Halmashauri ya Mji wa KAHAMA Mkoani SHINYANGA ALLY SINGA (26) amefikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya KAHAMA kwa tuhuma ya wizi wa kuaminika kinyume cha sheria.

Mbele ya Hakimu Mkazi wa Mahakama hiyo KENETH MUTEMBEI, mwendesha mashitaka wa Jeshi la Poilisi PETER MASAU amesema Mei 4 mwaka huu saa sita mchana maeneo ya uzunguni mjini Kahama, ALLY aliiba pikipiki aina ya SUN LG - MC 450 BRS.

MASAU amesema pikipiki hiyo yenye thamani ya shilingi milioni mbili ni mali ya JUMA MARCO aliyekuwa amemuamini ALLY na kumpa aendeshe kama bodaboda na badala yake akaitumia kwa matumizi yake binafsi.

Katika shauri hilo la jinai namba 188/2018 ALLY ametenda kosa hilo kinyume na kifungu namba 273 sura ya 16 marejeo ya mwaka 2002.

ALLY amekana kutenda kosa hilo na upelelezi wa shauri hilo haujakamilika na mshitakiwa amerudishwa rumande kwa kukosa dhamana na shauri hilo litatajwa tena Mei 31 mwaka huu.
Share:

VYOO CHANGAMOTO MACHIMBO YA DHAHABU YA KALYANGO KAHAMA



Na Ndalike Sonda
KAHAMA.

Idara ya Afya na usafi wa Mazingira katika machimbo ya dhahabu ya Kabela Ilindi, Kata ya Zongomela Wilayani KAHAMA imeiagiza kampuni ya Kalyango Gold Mine kujenga vyoo vingi zaidi ili kuzuia mlipuko wa magonjwa unaoweza kujitokeza.

Akizungumza na KAHAMA FM, Mkuu wa idara ya afya na usafi wa mazingira katika katika machimbo hayo, MACHIMU NELSON amesema idara yake imajizatiti kuhakikisha kila machimbo yanakuwa na vyoo vya kutosha.

Naye Meneja wa Kampuni ya Kalyango Gold Mines, MDAKI SHABAN amesema tayari wameanza kujenga matundu mawili ya vyoo na bafu na kwamba wanaendelea kutenga fedha zaidi kwa ajili ya kuongeza matundu mengine ya vyoo.

Naye Msimamizi wa idara ya Afya na usafi wa mazingira katika machimbo hayo ya dhahabu ya Kabela Ilindi, DANI MUSSA amesema wanaendelea kutoa elimu kwa wananchi waishio kwenye machimbo ili kuimarisha usafi wa mazingira katika machimbo hayo kwa manufaa ya jamii nzima.
Share:

WAZAZI WENYE WATOTO ALBINO WAASWA KUTOWAFICHA


Na Ndalike Sonda
KAHAMA.

Wazazi na walezi wenye watoto wenye ualbino wilayani KAHAMA Mkoani SHINYANGA imetakiwa kutowaficha watoto wao badala yake wawape haki zao za msingi ikiwamo matibabu na elimu bila usiri wowote.

Hayo yameelezwa leo na afisa tatibu wa hospitali ya Mji wa Kahama Dkt. FLORA MWINUKA kwenye kipindi cha raha ya leo kinachorushwa na Kahama fm ambapo amesema bado kuna baadhi ya wazazi wanawaficha watoto wao wenye ualbino licha ya elimu kuendelea kutolewa.

Amesema changamoto hiyo imekuwa ikisababisha unyanyapaa, na kuwanyima haki zao za msingi kama watoto wengine na kwamba jamii iache imani potovu dhidi ya watu wenye ualbino.

Kwa upande wake Katibu wa chama cha watu wenye ualbino Tanzania (TAS) Wilaya ya Kahama SITA MASENYA amesema chama hicho kimekuwa kikitoa elimu kwa jamii ili iwe tayari kuwapokea watu wenye ualbino.

Kwa mujibu wa MASENYA kwa sasa jamii wilayani Kahama imekuwa na uelewa dhidi ya watu wenye ualbino hali ambayo imepunguza matukio ya unyanyapaa na ukatili dhidi ya watu hao katika miaka ya hivi kaaribuni.
Share:

WAZAZI WILAYANI KAHAMA WAHASWA KUPELEKA WATOTO WAO KUFANYIWA TOHARA


Na Salvatory Ntandu
KAHAMA.

Wazazi na walezi wenye watoto wenye umri wa miaka 10 hadi 17 ambao hawafanyiwa tohara Wilayani KAHAMA wameshauriwa kuwapeleka watoto wao katika vituo vinavyotoa huduma hiyo bure wakati huu wa Kampeni maalum ya tohara kwa wanaume.

Wito huo umetolewa na DK LAMECK MIHAYO kutoka Zahanati ya BAKWATA Majengo mjini Kahama katika tathimini ya kampeni ya Tohara kwa wanaume inayoendelea katika Halmashauri ya Mji wa Kahama na Msalala kwa ufadhili wa shirika lisilo la kiserikali la Intrahealth.

Amesema watoto hao peke yao hawatoweza kupatiwa huduma hiyo kwa sababu bado umri wao ni mdogo kuweza kuzingatia maelekezo ya wataalamu wa afya baada ya kufanyiwa tohara.

Nao baadhi ya watoto waliopatiwa huduma hiyo, FURAHA MICHAEL na ERICK SHIJA wamewaomba wazazi kuwapeleka watoto wenzao kupata huduma hiyo ili kujikinga na magonjwa mbalimbali yakiwemo ya ngono kama vile UKIMWI.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya Footprint inayoratibu zoezi hilo, TERENCE MWAKALIKO kiasi cha wanaume 8,400 wanatarajiwa kufanyiwa tohara chini ya kampeni inayoendeshwa katika vituo 10 katika Halmashauri hizo za Kahama mji na Msalala.
Share:

AFIKISHWA MAHAKAMANI KWA TUHUMA ZA UNYANG'ANYI


Na Lilian/Paulina
KAHAMA.

Mkazi wa Mkoa wa Geita CLEMENT KAYANDA (24) amefikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya KAHAMA kwa tuhuma ya unyang’anyi kwa kutumia Silaha aina ya rungu pamoja na panga kinyume cha sheria.

Mbele ya Hakimu Mkazi wa Mahakama hiyo KENETH MUTEMBEI, mwendesha mashitaka wa Polisi PETER MASAU amesema May 5 mwaka huu majira ya saa 10 usiku huko kijiji cha Ilogi, KAYANDA aliiba kaboni gram 300 za kuchenjua dhahabu zenye thamani ya shilingi milioni arubaini mali ya DIANA JILUMBA.

MASAU amesema KAYANDA ametenda kosa hilo kinyume na kifungu namba 287 A cha kanuni ya adhabu sura ya 16 marejeo ya mwaka 2002.

Katika shauri hilo la jinai namba 184/2018 KAYANDA amekana kutenda kosa hilo na amerudishwa rumande kwa kuwa kosa analotuhumiwa halina dhamana na shauri hilo litatajwa tena May 31 mwaka huu.
Share:

WAUMINI WA DINI YA KIISLAM WILAYANI KAHAMA WAASWA KUTUMIA MWEZI MTUKUFU KUKEMEA MAOVU


Na Ndalike Sonda
KAHAMA.

Waumini wa dini ya Kiislamu Wilayani KAHAMA Mkoani SHINYANGA wameaswa kuutumia mwezi Mtukufu wa Ramadhan kukemea matendo maovu ambayo yamekuwa yakijitokeza katika jamii hasa mauaji ya vikongwe pamoja na kuzingatia swala.

Wito huo umetolewa na Shekhe wa Wilaya ya KAHAMA, OMARY DAMKA wakati akizungumza kwenye kipindi cha raha ya leo cha KAHAMA FM kuhusu Mfungo wa Ramadhani ulioanza leo ambapo amesema Waisilam wanapaswa kutenda yaliyo mema ili kupata thawabu.

Aidha SHEKHE DAMKA amewaasa wafanyabiashara wilayani humo kutopandisha bei za bidhaa mbalimbali wakati wa mwezi huu Mtukufu wa Ramadhan badala yake wauze kwa bei ya kwaida ili kuwawezesha Waumini kumudu gharama ya bidhaa zinazohitajika wakati huu wa mfungo.

Mmoja wa waumini wa dini hiyo na mkazi wa Kijiji cha Sangilwa, halmashauri ya mji wa Kahama, SAID HAMAD amesema mwezi Mtukufu wa Ramadhan utawasaidia kuwakumbusha maagizo ya Mtume Muhamad kwa Waisalam wote.

Mwezi mtukufu wa Ramadhan ni nguzo ya nne katika nguzo tano za Uisilam ambapo mwezi huu Waislam ulimwenguni kote huutumia kufunga kwa toba na kufanya mema.
Share:

MAJI YAWA KERO KWA WAKAZI WA BUKONDAMOYO KAHAMA


Na Ndalike Sonda
KAHAMA.

Wakazi wa kitongoji cha Kisiwani mtaa wa Bukondamoyo kata ya Mhungula halmashauri ya Mji wa KAHAMA wanakabiliwa na changamoto ya uhaba wa maji hali ambayo inasababisha kufuata huduma hiyo umbali mrefu pamoja na kutumia maji yasiyo salama.

Kutokana na hali hiyo, wananchi wa kitongoji hicho wameamua kushirikia katika ujenzi wa gati la Maji ya ziwa Viktoria ili kujihakikishia upatikanaji katika eneo hilo.

Wakizungumza na jana kwenye kikao cha kujadilia ujenzi huo, baadhi ya wananchi wamepongeza hatua hiyo na kuwataka wananachi wengine kushirikia kikamilfu katika ujenzi huo.

Mwenyekiti wa Mtaa wa Bukondamoyo NASHON YOHANA amesema ujenzi wa gati katika kitongoji hicho unatarajia kuanza Ijumaa hii na zoezi la kuchimba mtaro litaanza jumatatu wiki ijayo na kwamba hilo litakuwa gati la tano katika mtaa huo.
Share:

WALIMU WA SHULE ZA MSINGI NA SEKONDARI MANISPAA YA SHINYANGA WATAKIWA KUPAMBANA NA VITENDO VYA UKATILI WA KIJINSIA ILI KUTIKOMEZA VITENDO HIVYO KWENYE JAMII



Na Salvatory Ntandu
KAHAMA.

Walimu wa shule za Msingi na sekondari katika manispaa ya SHINYANGA wametakiwa kuwa mstari wa mbele katika kupambana na vitendo vya ukatili wa kijinsia kwa wanafunzi ili kutokomeza vitendo hivyo kwenye jamii.

Wito huo umetolewa na Mkuu wa wilaya ya SHINYANGA, JOSEPHINE MATIRO wakati akifungua warsha maalumu kwa walimu wa Manispaa hiyo yenye lengo la kuwajengea uelewa kuhusu masuala ya jinsia iliyoandaliwa na chuo kikuu huria Tanzania.

Amesema mbinu stahiki za kupambana na ukatili wa kijinsia zitafanikiwa endapo dhana, aina, matokeo na sababu za ukatili zitaeleweka kuanzia ngazi ya msingi hususani shuleni ambapo watoto wanatumia muda mwingi wa maisha yao.

MATIRO amefafanua kuwa walimu hukaa na wanafunzi kwa muda mrefu hivyo wanapaswa kuzijua athari zinazowakumba wanafunzi pindi wanapofanyiwa vitendo hivyo na namna vinyowaathiri kitaaluma.

Mbali na hilo MATIRO amewataka walimu kuweka kanuni na taratibu ambazo zitatoa ulinzi na kusaidia jamii nzima ya shule kuishi kwa amani na kuzingatia usawa ili wanafunzi wawezekufanya vizuri katika mitihani yao.

Kwa upande wake Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania, Kituo cha Shinyanga, PASCHAL MHELUKA amesema lengo la warsha hiyo ni kuwajengea uelewa walimu kuhusu masuala ya jinsia ili wakawafundishe wanafunzi ambao watakuwa mabalozi katika jamii.

Amebainisha kuwa kwa sasa wamewafikia walimu 100 kutoka shule za msingi na sekondari za serikali na binafsi wanaofundisha somo la uraia kwani wanafundisha masuala mtambuka yanayohusu mambo ya jinsia.
Share:

VIONGOZI WA KATA KAHAMA WAAGIZWA KUUNDA VIKUNDI VYA ULINZI SHIRIKISHI KUDHIBITI VIBAKA


Na Amina Mbwambo
KAHAMA.

Serikali Wilayani KAHAMA imewaagiza viongozi wa kata na vijiji kwa kushirikiana na wananchi wa maeneo yao kuanzisha vikundi vya ulinzi shirikishi ili kulisaidia jeshi la polisi kupambana na wimbi la vibaka lililoibuka wilayani humo.

Akizungumza na KAHAMA Fm Mkuu wa Wilaya ya KAHAMA na Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi Wilayani, humo FADHILI NKURLU amewataka wananchi kutokuwa na hofu na watoe taarifa za uhalifu ili kurahisisha operesheni inayoendelea dhidi ya vibaka wilayani humo.

Hivi karibuni, kumeibuka wimbi la vibaka mjini Kahama ambao wamekuwa wakiiba vitu mbalimbali zikiwemo betri za gari, kupora simu za mikononi pamoja na kuvunja nyumba na kuiba samani za ndani hali inayowafanya wananchi kuishi kwa mashaka.

WAKATI HUO HUO serikali wilayani Kahama imetoa onyo kali kwa wamiliki wa bar na vilabu vya pombe wilayani humo ambao wanakiuka taratibu za muda wa kufungua na kufunga sehemu hizo za starehe kulingana na vibali vyao.

Akiwaapisha Wakuu wapya wa mikoa Machi 16, 2016 Ikulu Dar es Salaam, Rais MAGUFULI aliwaagiza kuhakikisha baa zinafunguliwa saa 10 jioni na kufungwa saa 5 usiku, sambamba na kudhibiti mchezo wa pool table kwa kuwa unawadumaza vijana na kushindwa kufanya kazi.
Share:

WAWILI WAFIKISHWA MAHAKANI KWA TUHUMA ZA KUJIPATIA FEDHA KWA NJIA YA UDANGANYIFU


Na Lilian/Paulina
KAHAMA.
 
Wakazi wawili wa wilayani KAHAMA, JUMA MASALAGO (27) na RODA EMMANUEL (29) jana Wamefikishwa katika mahakama ya wilaya hiyo kwa tuhuma ya kujipatia shilingi laki moja kwa njia ya udanganyifu.

Mbele ya hakimu mkazi mfawidhi wa mahakama hiyo, EVODIA KYARUZI Mwendesha mashitaka wa TAKUKURU Kahama KELVIN MURUSURI amesema watuhumiwa hao walikamatwa Mwezi March mwaka huu wilayani Kahama.

MURUSURI amesema MASALAGO na EMMANUEL walitenda kosa hilo mwezi machi mwaka huu ambapo walijipatia shilingi laki 3 ili waweze kumsaidia JOHN MABARA katika kesi yake namba 153/2017 ambayo ipo katika baraza la Ardhi na nyumba wilayani Kahama ili ashinde.

Aidha MASALAGO anashitakiwa kwa kosa jingine kujifanya mtumishi wa serikali katika baraza la Ardhi hivyo March 27 mwaka huu alipatia sehemu ya pesa hizo kiasi cha shilingi laki 104,000/=

Katika shauri hilo la jinai namba 179/2018 MASALAGO amefanya kosa kinyume na kifungu 100 b cha sheria ya kanuni ya adhabu sura ya 16 marejeo ya mwaka 2012.

Aidha EMMANUEL anakabiliwa na shitaka la rushwa kinyume na kifungu 15 na 2 cha sheria ya kuzuia na kupambana na rushwa namba 11 ya mwaka 2007.

MASALAGO amekana kutenda makosa hayo huku EMMANUEL akikiri simu yake kupokea kiasi hicho cha pesa na Shauri hilo limeahirishwa hadi May 29 mwaka huu litakapotajwa tena kwa ajili ya usikilizwaji wa awali na wamerudishwa rumade kwa kukosa dhamana.
Share:

ELIMU YA UZAZI KWA WANAFUNZI MKOANI SHINYANGA YAWA KIKWAZO



Na salvatory ntandu
KAHAMA.

Kukosekana kwa elimu ya Afya ya uzazi na uelewa kuhusu Balehe kwa wanafunzi katika shule za msingi na Sekondari Mkoani SHINYANGA kunasababisha wengi wao kujiingiza katika vishawishi na uasherati wakiwa katika umri mdogo.

Hayo yamebainishwa kwenye kongamano lililojumuisha wanafunzi 120 kutoka shule nane zilizopo katika kata Usanda halmashauri ya wilaya ya Shinyanga (Vijijini) ili kuwajengea uelewa kuhusu masuala ya afya ya uzazi na jinsia yaliotolewa na shirika lisilo la kiserikali la AGAPE.

Akizungumza na wanafunzi hao Afisa wa Mradi wa Elimu ya Afya ya Uzazi na Ujinsia kwa Vijana kutoka AGAPE LUCY MAGANGA amesema elimu hiyo ikitolewa shuleni itawasaidia kujiepusha na tabia hatarishi zinazoweza kusababisha wakapata mimba na magonjwa ya zinaa ukiwemo Ukimwi.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji AGAPE, JOHN MYOLA amesema vitendo vya ukatili dhidi ya watoto vinasababisha ndoto za watoto kutotimia hivyo kuitaka jamii kuungana katika kuhakikisha haki za watoto zinalindwa.

Katika hatua nyingine amewataka wazazi na walezi kutengeneza urafiki na watoto ili kujua matatizo wanayokutana nayo ikiwemo kufanyiwa ukatili na watu wa karibu waliopo katika jamii inayowazunguka.

Naye Afisa Elimu kata ya Usanda ESSERO ASHERY amesema ataendelea kuhamasisha walimu na viongozi mbalimbali kutoa elimu juu ya masuala ya afya ya uzazi na ujinsia kwa vijana.

Nao baadhi ya wanafunzi waliohudhuria Kongamano hilo MUSA RAJAB na JENIFA SHIJA wameiomba serikali kuendelea kutoa elimu hiyo kwa wanafunzi katika shule mbalimbali ili kuwawezesha kutimiza malengo yao katika elimu.
Share:

HOSPITALI YA HALMASHAURI YA MJI WA KAHAMA YAKABILIWA NA CHANGAMOTO YA WATUMISHI


Na Lilian/Paulina
KAHAMA.

Hospitali ya Halmashauri ya Mji wa KAHAMA inakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo uhaba wa watumishi, malimbikizo ya posho na watumishi kutopandishwa madaraja kwa wakati mambo ambayo yanasababisha kushuka kwa ufanisi miongoni mwa watumishi.

Hayo yamebainishwa katika Risala ya Watumishi wa Hospitali hiyo iliyosomwa na Muuguzi SHARIFA MOHAMED katika maadhimisho ya Siku ya Wauguzi inayoadhimishwa duniani kote Mei 12 ya kila mwaka na ambayo imeadhimishwa leo katika Hospitali hiyo.

Akizungumza katika maadhimisho hayo, Afisa Maendeleo ya jamii wa Halmashauri hiyo, ROBERT KWELA amesema hivi sasa wameanza upanuzi wa hospitali hiyo kwa kujenga jengo la upasuaji na la mama na watoto na kwamba changamoto nyingine zinaendelea kufanyiwa kazi.

Katika maadhimisho hayo ambayo yamebeba kauli mbiu isemayo “WAUGUZI NI SAUTI YA UONGOZI NA AFYA NI HAKI YA BINADAMU”, jumla ya Wauguzi 10 waliostaafu katika hospitali hiyo wametunukiwa vyeti maalum vya kutambua mchango wao katika fani hiyo ya uuguzi.
Share:

AFIKISHWA MAHAKAMANI KWA KOSA LA KUMGONGA MTEMBEA KWA MIGUU NA KUSABABISHA KIFO CHAKE


Na Salvatory Ntandu
KAHAMA.

Mkazi wa Majengo Mjini KAHAMA, ALPHONCE MASOLA ambaye ni fundi Magari jana amefikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya KAHAMA kwa tuhuma ya kuendesha gari bila leseni na kumgonga mtembea kwa miguu na kumsababishia kifo.

Mbele ya Hakimu Mkazi wa Makahama hiyo, IMAN BATENZI mwendesha Mashitaka wa Polisi SAADA RASHID, amesema Mei 7 mwaka huu Majira ya saa 5 usiku katika barabara ya Ngaya, MASOLA alimgonga CHRISTIAN PAUL na kusababisha kifo chake .

SAADA amefafanua kuwa MASOLO anakabiliwa na mashitaka mawili ambapo katika shitaka la kwanza anadaiwa kuendesha gari katika barabara ya umma bila ya kuwa na leseni ya Udereva kinyume na kifungu namba 40 (1) na 63 (2) (a) ya sheria ya Usalama barabarani.

Katika shitaka la pili anatuhumiwa kuendesha gari kwa mwendokasi na kushindwa kulimudu na kumgonga mtembea kwa miguu na kusababisha kifo chake kinyume na kifungu namba (19) (1) na 113 cha sheria ya usalama barabarani.

MASOLA ambaye katika ajali hiyo alikuwa akiendesha Toyota Land Cruiser pickup T 404 AFR, amekana kutenda kosa hilo ambapo Shauri hilo namba 28/2018 limeahirishwa hadi Mei 24 mwaka huu na amerudishwa rumande kwa kushindwa kutimiza masharti ya Dhamana.
Share:

CHANGAMOTO YA AFYA, ELIMU VYAWA KERO KWA ALBINO NCHINO


Na Daniel Magwina
KAHAMA.

Imeelezwa kuwa changamoto za Kiafya, Elimu pamoja na Kijamii kuwa ni chanzo kikubwa cha kuendelea kunyanyapaliwa kwa watu wenye ulemavu wa ngozi (Albino), nchini.

Hayo yameelezwa Mjini KAHAMA jana na katibu wa chama cha watu wenye Ualbino (TAS) Wilayani KAHAMA, SITTA GILITU wakati akitoa elimu kwa wanafunzi wa shule ya msingi Nyasubi kuhusu hali ya Ualbino ambapo amesisitiza kuwa mtu mwenye ualbino ni mtu wa kawaida.

SITTA amesema kuwa changamoto zinazowakumba zimeendelea kuwa mwiba kwao na kusababisha baadhi ya wazazi kuwafungia ndani watoto wao wenye ualbino,na kusababisha watoto hao kushidwa kupata elimu na kushiriki shughuli za kijamii na kiuchumi ili kuinua uchumi wa familia zao.

Kwa upande wake mkuu wa shule ya Msingi Nyasubi, ROBISTA ADOLF amekishukuru chama hicho kwa elimu wanayo itoa katika shule mbalimbali na kupiga marufuku kwa mwanafunzi yoyote shuleni hapo kuwaita watu wenye Ualbino majina yasiyofaa.

Ualbino ni hali ya ukosefu wa rangi ya asili katika nywele macho pamoja na ngozi inayowafanya waathirika kushindwa kuhimili mionzi ya jua.
Share:

ZOEZI LA UPIGAJI CHAPA KWA NG'OMBE LAINGIA DOSARI HALMASHAURI YA USHETU


Na Samwel Nyahongo
KAHAMA.

Zoezi la upigaji chapa kwa ng’ombe katika Halmashauri ya USHETU limekuwa tatizo kutokana na chapa zinazotumika kufanyia zoezi hilo kutokua katika ubora na usahihi unaofaa kitendo kinachosababisha ngombe hao kuungua au alama ya chapa hizo kuwahi kufutika.

Akitoa hoja hiyo katika Baraza la Madiwani la robo ya tatu la Halmashauri hiyo Diwani wa kata ya Ukune DAUDI MKOPA amesema upigaji chapa kwa mifugo hiyo imekua ni changamoto kwani chapa hizo hazipo kwenye ubora unaofaa.

MKOPA amesema maboresho ya chapa hizo unahitajika ili kuhakikisha wafugaji hawakwepi zoezi hilo kwa sababu kwamba chapa katika mifugo yao zinafutika, kitendo kitakachofanya wakwepe kulipa kodi kwa ajili ya kuchapa mifugo yao.

Akijibu hoja hiyo Katibu wa Baraza hilo ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo MICHAEL MATOMORA amekiri kuwepo na changamoto hiyo kutokana na namba za chapa hizo kukaribiana kitendo kinachofanya ng’ombe kuungua.

MATOMORA amesema wao kama Halmashauri wameshatoa taarifa wilayani kuomba marekebisho ya chapa hizo ili kuzuia mifugo kuungua.

Katika hatua nyingine MATOMORA amesema kwa wafugaji ambao walipiga chapa na zikafutika, kumbukumbu zipo hivyo wakati wa marudio ya upigaji wa chapa hizo hawatarudia kulipa kodi ya upigaji chapa mara mbili.
Share:

WATENDAJI 35 WA MITAA NA KATA AMBAO WALIKUWA WAMESITISHIWA AJIRA ZAO KUTOKANA NA KUWA NA ELIMU YA DARASA LA SABA WAREJESHWA KAZINI


Na Ndalike Sonda
KAHAMA.

Halmashauri ya Mji wa KAHAMA Mkoani SHINYANGA jana imewarejesha kazini maafisa watendaji 35 wa Mitaa na Kata ambao walikuwa wamesitishiwa ajira zao kutokana na kuwa na elimu ya darasa la Saba.

Akizungumza na KAHAMA FM Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri hiyo, ANDERSON MSUMBA amesema zoezi hilo ni utekelezaji wa agizo la serikali.

Kuhusu malipo ya mishahara yao ambayo walikuwa hawajalipwa tangu watolewe kwenye mfumo wa ajira, MSUMBA amesema kwanza wanawaingiza kwenye mfumo rasmi ili zoezi la kuwalipa liendelee na kwamba kila Mtendaji ataendelea na cheo alichokuwa nacho awali.

Mmoja wa Maafisa watendaji hao, SIMON MABUMBA akizungumza kwa niaba ya wenzake, ameishukuru serikali kwa kuwarudisha kazini ambapo ameahidi watafanyaka kazi ya umma kwa bidii ikiwamo kusimamia kikamilifu miradi mbalimbali ya maendeleo katika maeneo yao ya kazi.

Hivi karibuni serikali iliagiza kurejeshwa kazini maafisa wote watendaji wa Vijiji, Mitaa na Kata waliokuwa wameajiriwa kabla ya mei 20 , 2004, ambao walikuwa wameondolewa kwenye ajira kutokana na kukosa sifa ya kuwa na elimu ya kidato cha nne.
Share:

VYAMA VYA USHIRIKA VILIVOKUFA KATIKA HALMASHAURI YA USHETU VYATAKIWA KUFUFULIWA


Na Samwel Nyahongo
KAHAMA.
 
Vyama vya ushirika vya pamba katika Halmashauri ya USHETU Wilayani KAHAMA vimetakiwa kufufua vyama vyao vilivyokufa katika kata mbalimbali ndani ya halmashauri hiyo kwa lengo la kuwarahisishia wakulima kwani msimu wa pamba umekwisha funguliwa.

Akizungumza katika Mkutano wa Baraza la Madiwani la Halmashauri hiyo Diwani wa kata ya Nyankende DOWA LIMBU amewaomba viongozi wa chama cha ushirika kutafuta njia ya kuwasaidia wakulima wa pamba kwani msimu wa mavuno ya pamba unaendelea.

DOWA amesema njia nzuri ya kuwasaidia wakulima hao ni kuanzisha vituo kwa kila kijiji ili kuwapa wepesi wakulima pamoja kijiji husika kukusanya ushuru wa mapato kutokana na zao hilo.

Akijibu hoja hiyo Afisa Ushirika wa Pamba katika halmashauri hiyo DISMAS KALENGA amesema makampuni yote ya ununuzi wa pamba yatanunua pamba hizo katika vyama vya ushirika kama ilivyopangwa na serikali huku jukumu kubwa walilonalo ni kuhakikisha wanasajili vyama vipya.

Hata hivyo KALENGA amesema watatembelea maeneo ya uzalishaji wa pamba ikiwepo kata ya nyankende kutazama uzalishaji wa pamba na kufungua kituo pamoja na kuajiri wahasibu na makarani kwaajili ya zoezi hilo.

Mkutano wa kawaida wa baraza la madiwani wa robo ya tatu Halmashauri ya Ushetu litaendelea tena kesho mei 09 kujadili changamoto mbalimbali na kupitisha maazimio waliyoazimiana madiwani hao.
Share:

WAKULIMA NA WADAU WA TUMBAKU KAHAMA WASHAURIWA KUJENGA KIWANDA CHA SIGARA HALMASHAURI YA USHETU



Na William Bundala
KAHAMA.
 
Wakulima na wadau wa zao la Tumbaku katika Mkoa wa kitumbaku KAHAMA,Wameshauriwa kujenga kiwanda cha Sigara katika Halmashauri ya USHETU Mkoani SHINYANGA ili kujihakikishia Soko la zao hilo katika siku zijazo.

Wito huo umetolewa na mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, ZAINAB TELLACK wakati wa ufunguzi wa masoko ya Tumbaku uliofanyika katika kata ya Uyogo halmashauri ya Ushetu wilayani KAHAMA.

Bi TELLACK amesema kuwa wakulima wa tumbaku wakiungana wana uwezo mkubwa wa kujenga kiwanda cha Sigara hata cha ukubwa wa kati hatua ambayo amesema itasukuma mbele maendeleo yao binafsi, wilaya ya Kahama na Taifa kwa ujumla.




Sambamba na hayo TELLACK ametoa wito kwa viongozi wa vyama vya Ushirika kuwa waadilifu na waaminifu katika uongozi wao na kuacha tabia ya wizi wa mali za ushirika na kuwanyanyasa wanachama waliowaweka madarakani.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika nchini, Dkt TITUS KAMANI ambaye alikuwa mgeni rasmi katika uzinduzi huo amewataka wakulima wa Tumbaku na Pamba kudumisha ushirika kwani utawasaidia kuweka nguvu ya pamoja katika kufikia mafanikio.

Awali akimkaribisha Mgeni rasmi Mwenyekiti wa Chama kikuu cha Ushirika Kahama (KACU) EMMANUEL CHEREHANI ameiomba Serikali kufikiria upya kuhusu utaratibu wa kununua Tumbaku kwa fedha za kigeni kwani kununua kwa shilingi ya Tanzania kunasababisha wakulima kupoteza Fedha nyingi.

Mkoa wa kitumbaku Kahama umekuwa wa kwanza kufungua masoko ya zao la Tumbaku Nchini ambapo kwa msimu wa mwaka 2017/2018 jumla ya kilo Milioni 8 na Elfu 11 zitauzwa katika mkoa wa kitumbaku Kahama.
Share:

SHIDEFA KAHAMA WAKABIDHIWA BAJAJI ILI KUSAIDIA HUDUMA ZA USAFIRI KWA WAGOJWA



Na Ndalike Sonda
KAHAMA.

Shirika lisilokuwa la Kiserikali la SHIDEPHA + la Mjini KAHAMA limekabidhi pikipiki za magurudumu matatu (bajaji) kwa halmashauri ya Msalala mkoani Shinyanga ili kusaidia huduma za usafiri kwa wagonjwa kwenye zahanati na vituo vya afya vinne vya halmashauri hiyo.

Akikabidhi msaada huo, leo mjini Kahama, Mkurugenzi wa Shirika hilo, VENANCE MZUKA, amesema bajaji hizo, wamezigawa kwenye kituo cha afya Lunguya na Chela , zahanati ya Segese na Isaka na zitasaidia kupambana na ugonjwa wa kifua kikuu na shughuli zingine za afya.

MZUKA amesema Bajaji hizo zinathamani ya shilingi milioni 28 na kwamba wataendelea kusaidia katika sekta hiyo ya afya katika kata mbalimbali za halmashauri ya Msalala.

Mwenyekiti wa halmashauri ya Msalala MIBAKO MABUBU amelishukuru shirika la SHIDEPHA + kwa msaada huo na kwamba utasaidia katika shughuli za usafiri kwenye sekta hiyo na huku akiwataka wadau wengine kuendelea kusaidia sekta ya afya kwa manufaa ya jamii.
Share:

MADIWANI WA HALMASHAURI YA MSALALA WAAZIMIA KUVUNJA MKATABA NA KAMPUNI YA BAHARI PHARMACY NDANI YA SIKU 14


Na Ndalike Sonda
KAHAMA.

Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Msalala wilayani Kahama limeazimia kuvunja mkataba na kampuni ya BAHARI PHAMACY ndani ya siku 14 kuanzia leo baada ya kampuni hiyo kushindwa kutekeleza zabuni ya kusambaza dawa kwenye zahanati na vituo vya afya katika halmashauri hiyo.

Akitangaza hatua hiyo katika kikao cha baraza la Madiwani leo, mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, SIMON BEREGE amesema watazingatia sheria za kuvunja mkataba na mzabuni huyo na kwamba zabuni zijazo zitatolewa kwa muda wa majaribio ili kupima uwezo na utendaji kazi wa mzabuni.

Akizungumza katika kikao hicho, Diwani wa kata ya Isaka, GERALD MWANZIA amesema Mzabuni huyo ameshindwa kuzingatia mkataba unavyoelekeza huku diwani wa kata ya Busangia, ALEXANDER MIHAYO akiitaka serikali kuchukua hatua stahiki.

Naye katibu tawala msaidizi, serikali za mitaa, Mkoa wa Shinyanga, ALPHONCE KASANYI amesema atayafikisha maazimio ya baraza hilo la Madiwani la Halmashauri ya Msalala kwenye ngazi ya mkoa kwaajili ya utekelezaji.
Share:

WAKAZI WA NYAHANGA WILAYANI KAHAMA WAISHAURI SERIKALI KUIMARISHA MITARO INAYOPITISHA MAJI MACHAFU KUWANUSURU NA MAGONJWA YA MLIPUKO


Na Ndalike Sonda
KAHAMA.

Baadhi ya wananchi wa vitongoji vya Maliasili A na B, Kata ya NYAHANGA Halmashauri ya Mji wa KAHAMA wameishauri serikali kuimarisha mitaro ya barabara katika vitongoji hivyo, ili kudhibiti maji ya mvua yasiingie kwenye makazi yao.

Wakizungumza kwenye kipindi cha Raha ya leo, baadhi ya wananchi hao wamesema ili kuzuia maji yasiende kwenye makazi yao ni lazima kujenga mitaro imara kwenye barabara hizo ili kuyaelekeza maji ya mvua yapite bila kuathiri makazi yao.

Wakati huo huo, Wananchi wa kitongoji cha Mlimani Mtaa wa Bukondamoyo mjini Kahama leo wameanza kumwaga vifusi vya changarawe kwenye barabara waliyojitolea kutengeneza ili kuunganisha na barabara kuu ya kwenda Mjini Kahama.

Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Bukondamoyo, JOSHUA YOHANA amesema wanategemea kumwaga tripu saba za changarawe ambazo zimetolewa kwa nguvu za wananchi wa Kitongoji hicho na wadau wengine.
Share:

UBOVU WA MIUNDOMBINU YA BARABARA KATIKA HALMASHAURI YA USHETU YAWA KIKWAZO CHA KUFUNGULIWA KWA MASOKO YA TUMBAKU


Na Daniel Magwina
KAHAMA.

Kuharibika kwa miundo mbinu ya barabara na madaraja katika halmashauri ya USHETU kutokana na mvua kubwa zilizonyesha Wilayani KAHAMA kumesababisha kuchelewa kufunguliwa kwa masoko ya tumbaku tofauti na ilivyo kuwa imepangwa awali

Akizungumza katika kikao maalumu cha Chama kikuu cha Ushirika cha KAHAMA (KACU Mwenyekiti wa chama hicho, EMMANUEL CHARAHANI amesema kuharibika kwa miundo mbinu kumesababisha kusogeza mbele kufunguliwa kwa soko hilo la tumbaku katika mkoa wa Kitumbaku, KAHAMA.

CHEREHANI ameongeza kuwa kusogezwa mbele kwa msimu wa masoko ya tumbaku kunaweza kusababisha ongezeko la riba kwa wanachama na hivyo kupata hasara au kupunguza kabisa faida kwa mkulima.

Nao baadhi ya wakulima wa tumbaku kutoka halmashauri ya ushetu wamezungumzia suala hilo la uharibifu wa miundo mbinu katika kipindi hiki cha mvua zinapoendelea kunyesha jambo ambalo limesababisha washindwe kusafirisha mazao yao.

Akitolewa ufafanuzi changamoto hiyo, mkuu wa wilaya ya Kahama, FADHILI NKURLU amesema licha ya Wakala wa Barabara za mijiji na vijijini (TARURA) kuwa na fedha kwa ajili ya marekebisho ya barabara hizo, changamoto kubwa ni mvua zinazoendelea kunyesha na kuchelewesha marekebisho hayo.

Awali KACU ilikua inatarajia kufungua soko la tumbaku Aprili 24 mwaka huu, lakni kutokana kuharibiwa kwa barabara na mvua zinazoendelea kunyesha wamepanga kufungua soko hilo Mei 10 mwaka huu.
Share:

WAKULIMA WA ZAO LA PAMBA WALIOKOPA WILAYANI KAHAMA WATAKIWA KUUZA PAMBA ZAO KATIKA VYAMA VYA MSINGI ILI KUINGIZWA KWENYE KUMBUKUMBU NA KUJENGA UAMINIFU KATIKA MSIMU UJAO


Na Amina Mbwambo
KAHAMA.

Wito umetolewa kwa wakulima wa zao la pamba waliokopa Wilayani KAHAMA kuhakikisha wanauza pamba zao katika vyama vya msingi na makampuni waliyokopa ili kuingizwa kwenye kumbukumbu na kujenga uaminifu katika msimu ujao.

Akizungumza na kahama fm leo, mwenyekiti wa chama cha ushirika cha Kahama (KACU) ambaye anasimamia zao la pamba na tumbaku, EMANUEL CHARAHANI amesema msimu wa zao la pamba utafunguliwa rasmi kesho na hivyo na kuwataka wakulima.

CHARAHANI amesema pamoja na kufunguliwa kwa msimu huo serikali imeelekeza malipo yote ya pamba kufanyika kwa njia ya benki na hivyo kila mkulima kwa kushirikiana na maafisa ushirika wa maeneo husika ahakikishe anafungua account kwa ajili ya malipo na usalama wa fedha zao.

Akizungumzia mfumo huo mpya wa ununuzi wa pamba, mkuu wa wilaya ya Kahama, FADHILI NKURLU amesema maandalizi yote ya ununuzi wa pamba yamekamilika na amewataka wakurugenzi na maafisa ushirika kuyatambua maeneo yote yatakayotumika katika ununuzi wa pamba na kuyatangaza.

Msimu wa zao la pamba unafunguliwa rasmi kesho Mei mosi ambapo kitaifa utafunguliwa katika wilaya ya Igunga mkoani Tabora ambapo serikali imeiagiza mikoa yote inayolima pamba nchini kuhakikisha ununuzi wa pamba yote unafanyika kwa njia ya account.
Share:

IDADI YA WASOMAJI

TUSIKILIZE LIVE KUPITIA TUNEIN

UNGANA NASI FACEBOOK HAPA

10 ZILIZOSOMWA ZAIDI

Labels

Blog Archive