MBUNGE WA ZAMANI WA JIMBO LA KAHAMA JAMES LEMBELI KUZUNGUMZA NA WAANDISHI WA HABARI JUMATANO



KAHAMA.

Aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Kahama kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), kuanzia mwaka 2005 hadi 2015, JAMES LEMBELI, siku ya Jumatano atazungumza na Vyombo vya Habari nyumbani kwake kijijini Mseki Bulungwa wilayani Kahama.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari na Msaidizi wake, MIPAWA NG’WANANGOLELWA jana, katika mkutano huo LEMBELI ataelezea ushiriki wake katika ujenzi wa taifa na mustakabali wake katika masuala ya kisiasa.

NG'WANANGOLELWA amesema, LEMBELI ambaye katika kipindi chake cha ubunge alipata umaarufu katika mapambano dhidi ya ufisadi nchini, ameamua kuzungumza na vyombo vya habari baada ya ukimya wa muda mrefu.

Kabla ya kujiunga na siasa mwaka 2005, LEMBELI amewahi kufanya kazi katika taasisi mbalimbali za ndani na nje ya nchi ikiwa ni pamoja na iliyokuwa Jumuiya ya WASHIRIKA, gazeti la Kiongozi, Idhaa ya Kiswahili ya Sauti ya Ujerumani (DW) jijini Berlin na Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA).

Katika hatua nyingine, Waislamu nchini wameombwa kuwaombea viongozi wa Taifa la Tanzania bila kujali itikadi zao ili kuleta amani na kuwafanya viongozi wawe na Heshima na Busara katika kuongoza Watanzania na Taifa kwa ujumla.

Wito huo umetolewa jana na Mkurugenzi wa Kahama Fm JAMES LEMBELI wakati wa futari aliyoiandaa kwaajili ya waumini wa msikiti wa kijiji cha Iboja kata ya Ukune Halmashauri ya Ushetu wilayani Kahama.

Amesema, viongozi wa kiroho katika hali ya kawaida wapo karibu na Mungu hivyo, maombi yao yatafika kwa urahisi kwake mwenyezi Mungu ambaye atashusha neema ya hekima kwa viongozi wa taifa letu na hivyo amani ya nchi yetu kutamalaki.

Ameongeza kuwa kwa kuwa mfungo mtukufu wa Ramadhani ni utekelezaji wa nguzo tano za Uislamu ikiwa ni pamoja na kusali,basi viongozi na waumini kwa ujumla wana wajibu wa kuliombea Taifa letu lizidi kudumisha amani na mshikamano miongoni mwa Watanzania.

Kwa upande wake, Sheikh wa Msikiti wa Kijiji cha Iboja, ATHUMANI MOHAMED amemshukuru LEMBELI kwa moyo wa upendo na ukarimu na kuongeza kuwa LEMBELI kila mwaka amekuwa na utaratibu wa Kuwafuturisha Waislamu wasio na uwezo na kutoa wito kwa watu wengine wenye uwezo kuiga mfano wake.
Share:

No comments:

Post a Comment

IDADI YA WASOMAJI

TUSIKILIZE LIVE KUPITIA TUNEIN

UNGANA NASI FACEBOOK HAPA

10 ZILIZOSOMWA ZAIDI

Labels